Tafuta

Vatican News
2020.08.05 - Mlipuko wa Beirut. Picha ni Caritas Internationalis ya Lebanon katika harakati za kutoa msaada wa kwanza 2020.08.05 - Mlipuko wa Beirut. Picha ni Caritas Internationalis ya Lebanon katika harakati za kutoa msaada wa kwanza 

Siku ya huduma za kibinadamu Ulimwenguni 2020:Kusaidia jumuiya mahalia!

Kila tarehe 19 Agosti ni siku ya Kimataifa ya huduma za kibinadamu na ofisi ya Caritas internationalis inatoa mwaliko wa kuangazia nafasi msingi ya Jumuiya mahalia ili kuhakikisha majibu ya haraka katika muktadha wa huduma za kibinadamu.Inaomba utolewe msaada mkubwa kwa mashirika ya asasi za kiraia na zaidi ya kidini kama vile Caritas ambao wanatoa msaada mkubwa wa jumuiya mahalia ulimwenguni kote.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Kila tarehe 19 Agosti ya kila mwaka Umoja wa Mataifa unaadhimisha siku ya Kimataifa ya huduma za kibinadamu. Katika fursa hii Caritas internationalis inaangazia umakini kuhusu umuhimu wa jumuiya mahalia  ili kuhakikisha yanatolewa majibu ya haraka katika muktadha wa msaada wa kibinadamu. Caritas intenationalis aidha inaomba utolewe msaada mkubwa kwa mashirika ya asasi za kiraia  na hasa ya kidini kama vile Caritas ambayo inajikita kutoa msaada mkubwa sana na kuongeza nguvu za jumuiya katika maeneo mahalia.

Siku hii ya tarehe 19 Agosti ilitangazwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2008 kama kutoa jibu la shambulizi la kigaidi lililokuwa limetokea miaka mitano kabla, yaani kunako 2003 katika Mtaa ulio na Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko Baghdad, nchini Iraq na kusababisha vifo vya watu 22 miongoni mwao alikuwemo mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq Sergio Vieira de Mello. Siku hii kwa hakika ni kutaka kuangazai zaidi ulinzi na usalama wa wafanyakazi wanaotoa huduma za kibinadamu sambamba na utu wao kwenye maeneo mengi  yenye mizozo na kinzani ulimwenguni.

Mtu mmoja kati ya watu 45 ulimwenguni anahitaji msaada

Siku ya kimataifa ya huduma za kibinadamu  aidha inawakumbuka wale  wote ulimwenguni wanaofanya kazi katika maeneo magumu sana, yenye kuwa na majenga tofauti kama vile tememeko, vita, mafuriko na majanga mengine ya asili na yasiyo ya asili. Kwa mwaka huu 2020, siku hii inaadhimishwa katika muktadha  wa janga la Covid-19 ambalo limeathiri na linaendelea kuleta matatizo makubwa na pia milipuko ambao umeangamiza jiji la Beirut nchini Lebanon. Katika wakati huu wa kihistoria Caritas internationalis inabainisha kuwa mfumo wa kibinadamu wa kimataifa umejaribiwa vikali sana kuliko hapo awali, na mtu mmoja katika kila watu 45 ulimwenguni anahitaji msaada. Katika siku hii jumuiya  ya kimataifa inakumbuka ukarimu wa maelfu ya wahudumu wa kibinadamu, masikini na hasa walionusurika kwa majanga, wanaotamani kuishi kwa hadhi, kwa mujibu wa Aloysius John, katibu mkuu wa Caritas internationalis, ambaye anaonesha ukaribu wake kwa nchi zote ulimwengu .

Kutenga fedha kwa  ajili ya mashirika ya asasi za kiraia

Caritas internationalis  vile vile katika muktadha  wa siku hii , inashauri serikali na jamuiya ya kibinadamu kimataifa kutenga fedha kwa kiwango kikubwa ili kuimarishaji asasi za kiraia na miundo yao  msingi; kutenga fedha maalum kwa ajili ya uwezeshaji wa jamuiya za maeneo mahalia na kuiruhusu kuchukua hatua stahiki hasa inapotokea  tukio la majanga. Caritas internationalis aidha inaomba kwamba serikali zote na jamuiya ya kibinadamu kimataifa zizingatie uwezeshaji wa mashirika ya asasi za kiraia, hasa mashirika ya  kidini ambayo hufanya kazi sana karibu na watu wa  jamuiya mahalia. Kwa maana hiyo ni muhimu kwamba mashirika haya yawe na rasilimali muhimu ili waweze kuandaa jamuiya mahalia katika kujibu kwa kujitegemea dharura zinapotokea.

19 August 2020, 10:17