Tafuta

Katekesi Kuhusu Fadhila na Mizizi ya Dhambi: Fadhila ya Nguvu

Fadhila ya nguvu ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 10 Aprili 2024. Amekazia kuhusu nguvu iliyoko ndani na nje ya mtu mwenyewe; maadui wa nje na changamoto za maovu katika ulimwengu mamboleo, mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kujifunza fadhila ya nguvu iliyoshuhudiwa na kutangazwa na watakatifu wa Mungu. Wakristo wahakikishe kwamba, wanatumia fadhila ya nguvu kutenda mema na haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mizizi ya dhambi, vilema vikuu vya dhambi au vichwa vya dhambi ni orodha ya maovu ambayo tangu zamani za Mababa wa Kanisa katika kanuni maadili ya Ukristo yanahesabiwa kumuelekeza binadamu kutenda dhambi nyingine, hata kubwa zaidi. Mizizi ya dhambi iko saba nayo ni: Majivuno, uzembe, kijicho, hasira, uroho, utovu wa kiasi na uzinzi, si dhambi kuu kuliko zote; lakini ndivyo vilema tunavyovielekea kwanza na ndivyo vinavyomsogeza mwanadamu mbali zaidi na Mwenyezi Mungu na hivyo kumtumbukiza katika makosa makubwa zaidi kama vile: uzushi, uasi wa dini, kukata tamaa na hatimaye, kumchukia Mungu. Mtu hafikii uovu mkubwa mara moja, bali polepole na hatua kwa hatua.  “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Flp 4:8. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK 1803-1803. Kuna fadhila tatu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo.

Nguvu ni fadhila adili inayothibitisha ushupavu katika magumu
Nguvu ni fadhila adili inayothibitisha ushupavu katika magumu

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Desemba 2023 alianza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo. Baba Mtakatifu amekwisha kuchambua mizizi hii ya dhambi hatua kwa hatua na kwamba, tiba ya uvivu ni uvumilivu wa kiimani. Amezungumzia pia kuhusu wivu, utepetevu, uchoyo, majivuno na sasa ameanza kutafakari kuhusu fadhila. Kuna fadhila kuu nne zinazotenda kazi kama bawaba ndiyo maana zinaitwa “Kuu.” Fadhila nyingine zote zajikusanya kuzizunguka nazo ni: Busara, haki, nguvu na kiasi. Kama mtu anapenda haki, basi fadhila ni matunda ya juhudi yake; kwani hufundisha kiasi na ufahamu, na haki na ushujaa. Fadhila hizi zasifiwa katika matini mbalimbali za Maandiko Matakatifu kwa majina mengine. Rej. KKK 1805. Mababa wa Kanisa wanasema, Busara ni fadhila inayoiandaa akili ya kawaida kupambanua katika mazingira yote mema yetu ya kweli na kuchagua njia zitakiwazo kuyapata. “Mtu mwenye busara huangalia sana aendavyo. Iweni na akili, mkeshe katika sala. Busara ni sheria sahihi ya utendaji ameandika Mtakatifu Thoma wa Akwino, akimfuata Aristotle. Busara isichanganwe na hofu au woga, wala hila au udanganyifu. Hekima huitwa “Auriga virtutum” yaani “Mwendesha fadhila; huongoza fadhila nyingine kwa kuweka sheria na kipimo. Ni busara inayoongoza mara moja hukumu ya dhamiri. Mtu mwenye busara huamua na kuongoza mwenendo wake kulingana na hukumu hiyo. Kwa msaada wa fadhila hii tunatumia misingi ya maadili katika masuala ya pekee bila kosa na kushinda mashaka ya mema ya kupata, na mabaya ya kuepuka. Rej. KKK. 1806. Baba Mtakatifu amekwisha kugusia pia fadhila ya subira katika maisha na utume wa Kristo Yesu.

Papa anawaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea amani ya kudumu
Papa anawaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea amani ya kudumu

Haki ni fadhila ya kibinadamu na Mababa wa Kanisa wanasema, haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mungu na jirani iliyo haki yao. Haki kwa Mungu huitwa “Fadhila ya Kimungu.” Haki kwa watu yaelekeza kuheshimu haki za kila mmoja, huanzisha mapatano katika mahusiano ya kibinadamu yanayoendeleza usawa kuhusu watu, mali ya Jumuiya. Mtu mwenye haki, anayetajwa mara nyingi katika Maandiko Matakatifu hutofautishwa kwa kawaida ya mawazo yake, unyofu wa mwenendo wake kwa jamii. “Usimpendelee mtu maskini, wala kumstaajabia mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. Ninyi akina bwana, wapeni watumwa wenu yaliyo haki na adili, mkijua kuwa ninyi nanyi mna Bwana mbinguni.” KKK 1807. Fadhila ya haki inajulikana pia kwa lugha ya Kilatini kama “Unicuique suum.” Baba Mtakatifu kuhusu fadhila ya haki, amekazia kuhusu fadhila mbadala zinazowawezesha watu kuishi kwa amani, mtu wa haki daima yuko tayari kuomba msamaha, ni shuhuda wa kanuni maadili na utu wema, kwa hakika watu wa haki ni wachache sana ndani ya jamii, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuwa ni watu wa haki. Katika maisha ya jamii, kila mtu anapaswa kutendewa kwa haki sanjari na kuheshimu utu wake wake. Fadhila ya haki inadai fadhila nyingine kama: ukarimu, heshima, shukrani, urafiki, uaminifu na kwamba hizi fadhila zinazochangia kuishi pamoja kwa watu vizuri.

Fadhila ya nguvu huwezesha kushinda hofu
Fadhila ya nguvu huwezesha kushinda hofu

Nguvu ni fadhila adili inayothibitisha ushupavu katika magumu na uthabiti katika kufuata mema. Yaimarisha uamuzi wa kushindana na vishawishi, kushinda vikwazo vya maisha adili. Fadhila ya nguvu huwezesha kushinda hofu, hata hofu ya kifo; na kukabiliana na majaribu, na madhulumu. Yamwandaa mtu kuwa tayari hata kujikatalia na kutoa sadaka ya uzima wake kwa ajili ya kutetea haki. Bwana ni nguvu yangu na wimbo wangu. Ulimwenguni mnayo dhiki, lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu. Rej. KKK 1808. Fadhila ya nguvu ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 10 Aprili 2024. Amekazia kuhusu nguvu iliyoko ndani na nje ya mtu mwenyewe; maadui wa nje na changamoto za maovu katika ulimwengu mamboleo, mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kujifunza fadhila ya nguvu iliyoshuhudiwa na kutangazwa na watakatifu wa Mungu. Baba Mtakatifu anasema, ari na matamanio si lazima yawe ni mabaki ya dhambi, lakini hayana budi kuelimishwa, kuelekezwa na kusafishwa kwa maji ya Ubatizo na moto wa Roho Mtakatifu. Wakristo hawana budi kuhakikisha kwamba, wanatumia fadhila ya nguvu kwa ajili ya kutenda mema, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu aliyeonesha hisia zake za kibinadamu wakati wa kifo cha rafiki yake Lazaro alitokwa na machozi na nafsi yake yenye utashi na shauku iling’aa katika baadhi ya maneno yake kama pale anaposema “Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi? Rej. Lk12:49; na pale alipowafukuza wafanyabiashara kutoka kutoka Hekaluni. Rej. Mt 21: 12-13.

Fadhila ya nguvu iwasaidie waamini kutenda mema
Fadhila ya nguvu iwasaidie waamini kutenda mema

Baba Mtakatifu Francisko akifafanua kuhusu fadhila ya nguvu anasema fadhila hii inawasaidia waamini kuzaa matunda mema maishani. Wanafalsafa wa Kigiriki na Wanataalimungu wa Kikristo walitambua mwelekeo wa fadhila ya nguvu iliyoko ndani na nje ya mtu mwenyewe. Fadhila hii inamwezesha mwamini kushinda maadui wa ndani ambao ni: wasiwasi, uchungu, hofu na hatia; nguvu hizi pia zisiporatibiwa vyema, zinaweza kumdumaza mwamini na hatimaye kushindwa hata kabla ya kuanza kukabiliana na changamoto zilizoko mbele yake. Kumbe, kuna haja ya kutambua kwanza kabisa maadui wa ndani kwani ushujaa ni ushindi wa kwanza dhidi ya mtu mwenyewe. Waamini kwa nguvu ya ndani wanaweza kushinda changamoto nyingi lakini watambue kwamba Mwenyezi Mungu yuko upande wao kuwalinda kwani Yeye ni ngao na silaha zao. Pamoja na majaribu na maadui wa ndani, kuna maadui wa nje, ambao ni majaribu ya maisha, mateso, magumu ambayo mwamini hayataraji na hivyo huwashangaza na wakati mwingine, mwamini anaweza kujikuta akiwa amekumbwa na mawimbi mazito na hivyo kujikuta akiwa amebwagwa chini. Fadhila ya nguvu na ujasiri, huwafanya waamini kuwa Mabaharia wastahimilivu, ambao hawaogopi wala kukata tamaa. Ujasiri ni sifa ya msingi kwa sababu inachukua kwa uzito changamoto ya uovu duniani. Mtu anajifanya kuwa haipo, kwamba kila kitu kiko sawa, kwamba mapenzi ya mwanadamu wakati mwingine sio kipofu, kwamba nguvu za giza zinazoleta kifo hazisumbuki katika historia. Lakini inatosha kupitia kitabu cha historia, au kwa bahati mbaya hata magazeti, ili kugundua ukatili ambao binadamu kwa sehemu kubwa ni waathirika wakuu wa: vurugu, utumwa, ukandamizaji na unyonyaji wa maskini, madonda ambayo bado yanavuja damu.

Fadhila ya nguvu humwezesha mwamini kushinda maadui wa ndani na nje.
Fadhila ya nguvu humwezesha mwamini kushinda maadui wa ndani na nje.

Fadhila ya nguvu na utu wema, huwafanya waamini kusimama kidete dhidi ya mambo yote haya. Tabia ya mwanadamu kupenda mno starehe na anasa. Kumekuwepo na maendeleo hafifu juu ya matumizi ya kikaboni, jambo ambalo linaonekana kana kwamba, hakuna haja ya kupambana na wakati mwingine, binadamu anahisi mambo ya kale ya Manabii. Lakini watu wasio na raha na maono ni nadra sana katika Ulimwengu mamboleo. Kuna hitajika mtu wa kuwashtua wengine, ili waweze kuamka na kuanzisha mapambano. Huu ni wakati wa kugundua tena Injili ya nguvu ya Yesu na hivyo kujifunza kama ilivyokuwa kwa watakatifu wa Mungu kutoa ushuhuda wao.

Fadhila ya Nguvu
10 April 2024, 17:57

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >