Tafuta

Katekesi Kuhusu Fadhila na Mizizi ya Dhambi: Huzuni Na Majonzi Moyoni

Huzuni inayomwilishwa katika mchakato wa wongofu wa ndani inaweza kuwa ni chemchemi ya furaha na kwamba, waamini wanaalikwa kusimama kidete kupambana na huzuni, kwa sababu hii ni kazi ya Shetani, Ibilisi. Mtume Paulo anafafanua kuhusu huzuni kwa kusema: “Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.” 2 Kor 7: 10. Huzuni inaweza kuwa ni sehemu ya maradhi ya moyo! Chunga!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK. 1803-1803. Kuna fadhila tatu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Desemba 2023 alianza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo. Katika mzunguko huu wa Katekesi, Baba Mtakatifu amekwisha kuchambua kuhusu: Dhambi na vishawishi vya dhambi, ulafi, tamaa mbaya pamoja na gadhabu. Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 7 Februari 2024 imenogeshwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu “Hata lini nifanye mashauri nafsini mwangu, nikihuzunika moyoni mchana kutwa? Hata lini adui yangu atukuke juu yangu? Naam, nimwimbie Bwana, kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu. Zab 13: 2-3.6. Katika katekesi hii, Baba Mtakatifu amefafanua kuhusu huzuni.

Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi:huzuni moyoni
Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi:huzuni moyoni

Baba Mtakatifu anasema, upweke hasi, huzuni na majonzi moyoni, bila ya mtu kupata kishawishi cha kukimbia uhalisia wa maisha, inaweza kuwa ni fursa kwa mwamini kukua na kukomaa katika undani wa maisha yake. Hali kama hii inahitaji mwamini awe makini na aendelee kujikita katika hali ya unyenyekevu; mambo msingi hata katika maisha ya kiroho. Kinyume cha maelezo haya, mwamini anaweza kujikuta anapoteza utu na heshima yake kama binadamu. Huzuni inayomwilishwa katika mchakato wa wongofu wa ndani inaweza kuwa ni chemchemi ya furaha na kwamba, waamini wanaalikwa kusimama kidete kupambana na huzuni, kwa sababu hii ni kazi ya Shetani, Ibilisi. Mtume Paulo anafafanua kuhusu huzuni kwa kusema: “Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.” 2 Kor 7: 10. Hii ni huzuni inayomletea mwamini wokovu, kama ilivyokuwa katika simulizi la Baba mwenye huruma na Mwana Mpotevu aliyetubu kutoka moyoni mwake, akaondoka na kurejea nyumbani kwa Baba yake. Hii ni neema ya Mungu iliyomwezesha kutambua dhambi zake na hivyo kuhuzunika moyoni mwake kwa sababu alikuwa amepoteza utakatifu wa maisha kadiri ya mpango wa Mungu. Huzuni pia inaweza kuwa ni sehemu ya maradhi ya kiroho yanayopata chimbuko lake katika sakafu ya moyo wa mwanadamu, kiasi kwamba, hamu pamoja na matumaini yanapotea kama ndoto ya asubuhi. Hii ndiyo hali iliyowatokea wale Wafuasi wa Emau kiasi cha kusema, “Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo.” Lk 24:21. Huzuni hii inatokana na kumkosa Kristo Yesu, kiasi cha kuyeyusha matumaini yaliyokuwa yamechanua kutoka katika sakafu ya nyoyo zao na hivyo kuwakatisha tamaa, hali hii inaweza kumtumbukiza mtu katika ugonjwa wa sonona na uchungu moyoni. Baba Mtakatifu anasema, haya ni mang’amuzi ya watu wote. Lakini baada ya muda, mtu anaweza kujiwekea tena matumaini.

Huzuni ni chemchemi ya toba na wongofu wa ndani
Huzuni ni chemchemi ya toba na wongofu wa ndani

Baba Mtakatifu anasema, huzuni ni kama raha ya kutopenda, kuwa na furaha kwamba jambo hili halijatokea, ni sawa na kumung’unya peremende chungu. Huzuni ni raha ya kutokuwa na raha. Mtawa Evagrius anasema kwamba maovu yote yanalenga raha, hata iwe ya muda mfupi vipi, ilhali huzuni hufurahia kinyume chake: kubatizwa katika maumivu yasiyoisha. Maombolezo yanayodumu muda mrefu sio kawaida ya maisha ya kiroho kama ulivyo uchungu, chuki na uhasama ni mambo ambayo hayana afya kwa maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko ni kuponya udhaifu huu na kuanza kujielekeza kwa yale yajayo mbeleni. Mababa wa Jangwani walielezea huzuni kama mdudu anaye wamongonyoa na kuwaondoa wale wanaokaribishwa. Jambo la msingi kwa waamini ni kujiuliza Je, hii ni huzuni nzuri au huzuni mbaya. Usisahau kwamba huzuni inaweza kuwa kitu kibaya sana kinacho mpelekea mtu kwenye tamaa na uchoyo na hivyo kumtumbukiza mwamini katika ubinafsi hali ambayo ni ngumu kuweza kupona. Kristo Mfufuka ni chemchemi ya ukombozi wa mwanadamu. Imani huondoa woga, na ufufuo wa Kristo huondoa huzuni kama jiwe kutoka kaburini. Kila siku ya Kikristo ni zoezi la ufufuo. Georges Bernanos, katika riwaya yake maarufu ya “Diary of a Country Priest,” Padre wa parokia ya Torcy anasema hivi: «Kanisa lina furaha, furaha hiyo yote ambayo imehifadhiwa kwa ulimwengu huu wa huzuni. Ulichofanya dhidi yake, ulifanya dhidi ya furaha." Na mwandishi mwingine Mfaransa, León Bloy, alituachia msemo huo wa ajabu: «Kuna huzuni moja tu, […] ile ya kutokuwa watakatifu». Roho wa Yesu mfufuka atusaidie kushinda huzuni kwa utakatifu.

Papa Francisko amefafanua maana ya huzuni na majonzi moyoni.
Papa Francisko amefafanua maana ya huzuni na majonzi moyoni.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii ya Katekesi kuwashukuru na kuwapongeza Watawa wa Shirika la “Le Pie Discepole di Divin Maestro” wanaoadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwao. Amempongeza Askofu mkuu mstaafu Giovanni Tani wa Jimbo kuu la Urbino-Urbania-Sant'Angelo in Vado kwa kuandamana na Mapadre wanaoadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre, iwe ni fursa ya kupyaisha sadaka na majitoleo yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Amewaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka na kuwaombea waathirika wa vita sehemu mbalimbali za dunia kwa sababu vita ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu. Waamini waendelee kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Katekesi hii imehudhuriwa pia na mahujaji kutoka Tanzania ambao tayari wamekwisha kutembelea Madhabahu ya Lourdes, Ufaransa, Roma na Assisi na “San Giovanni Rotondo” mahali yaliko masalia ya Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina, mfano bora wa maisha ya sala, unyenyekevu na hekima! Huyu ni Mtakatifu aliyekuwa na imani na matumaini thabiti kwa Mwenyezi Mungu; akajitoa na kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya watu wake; akalipenda na kuliheshimu Kanisa licha ya matatizo na changamoto zote alizokumbana nazo katika maisha na utume wake.

Katekesi Huzuni
07 February 2024, 15:18

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >