Tafuta

Katekesi: Shauku ya Uinjilishaji, Bidii ya Kitume ya Waamini: Utangazaji na Ushuhuda!

Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake Jumatano tarehe 13 Desemba 2023 amegusia kuhusu Mazingira ambamo Kristo Yesu alitenda miujiza yake; Anawaalika wafuasi wake “kufunguka” ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kuwashirikisha wengine upendo wa Mungu; Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni wavuvi wa watu. Wabatizwa wote wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume. Rej. Mt 9:9-13. Hii ndiyo tema inayoongoza Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 11 Januari 2023 na kuhitimishwa tarehe 13 Desemba 2023. Hii ni tema ya dharura na madhubuti kwa maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwa, jumuiya ya waamini inazaliwa kwa sababu ya utume na umisionari, huku ikisukumwa na Roho Mtakatifu, inatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Huu ndio mwelekeo na dira ya utume na maisha ya Kikristo, vinginevyo, Wakristo wanaweza kujikuta wakijitafuta wao wenyewe katika ubinafsi wao. Bila ya kuwa na shauku ya uinjilishaji, imani itadhohofu na hatimaye, kunyauka na utume ndicho kiini cha maisha ya mwamini. Kumbe, mzunguko huu wa katekesi ni kutaka kupyaisha shauku ya uinjilishaji kwa kuzama zaidi katika Maandiko Matakatifu sanjari na Mafundisho Tanzu ya Mama Kanisa ili kuchota amana na utajiri wa ari, mwamko na bidii ya kitume. Katika mzunguko huu wa Katekesi, Baba Mtakatifu amejitahidi kuweka mbele ya waamini mifano hai na baadhi ya mashuhuda wa imani, walioamsha shauku ya Habari Njema ya Wokovu, ili wawasaidie waamini kuwasha tena ule moto wa Roho Mtakatifu, ili hatimaye, uweze kuzijaza nyoyo za waamini wote mapendo. Ni katika muktadha huu, wakristo wanapaswa kujitahidi katika maisha yao ya kila siku kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Kristo Yesu; upendo unaoganga, kuponya na kuwaokoa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu
Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu

Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 13 Desemba 2023 imenogeshwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu ambayo Kristo Yesu anamponya kiziwi. “Akatoka tena katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.” Mk 7: 31-37. Baba Mtakatifu katika Katekesi yake amegusia kuhusu Mazingira ambamo Kristo Yesu alitenda miujiza yake; Anawaalika wafuasi wake “kufunguka” ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kuwashirikisha wengine upendo wa Mungu; Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni wavuvi wa watu. Katika mzunguko wa Katekesi kuhusu Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume. Rej. Mt 9:9-13, Baba Mtakatifu anasema, alijikita zaidi katika Neno la Mungu ili kukuza na kuhamasisha shauku ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. “Efatha” maana yake ni “Funguka” neno linalotumiwa na Padre wakati wa kutoa Sakramenti ya Ubatizo. Naye husema “Bwana Yesu, aliyefanya viziwi wasikie na bubu waseme, akujalie uweze kusikia kwa masikio Neno lake, na kuungama kwa mdomo imani ya Kikristo, kwa sifa na utukufu wa Mungu Baba. Amina.” Haya ni maneno yanayotoka kwa Kristo Yesu alipomponya yule kiziwi aliyekuwa anaishi katika maeneo ya Wapagani na wala si Wayahudi. Kristo Yesu akiwa ameambatana na Mitume aliweza kuwaponya viziwi na bubu wakaweza kuzungumza tena.

Katekesi kuhusu shauku ya uinjilishaji, bidii ya kitume ya mwamini
Katekesi kuhusu shauku ya uinjilishaji, bidii ya kitume ya mwamini

Kiziwi na Bubu katika Maandiko Matakatifu ni mtu yule asiyeweza kusikia, kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu katika maisha yake. Mwinjili Marko anaonesha neno jingine muhimu sana katika maisha na utume wa Kristo Yesu nalo ni “Efatha, yaani Funguka.” Huu ni mwaliko kwa waamini kumfungulia Kristo Yesu masikio na midogo yao ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hiki ndicho kiini cha Sakramenti ya Ubatizo, mwaliko kwa kila Mbatizwa ili aweze kufunguka mbele ya Injili, tayari kuitangaza na kuishuhudia kwa njia ya matendo mema, adili na matakatifu; sanjari na huduma kwa jirani na wahitaji zaidi. Funguka ni wito na mwaliko kwa waamini wote anasema Baba Mtakatifu Francisko. Mwishoni mwa Injili, kila mwamini anakabidhiwa dhamana, wito na utume wa kwenda ulimwenguni kote kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ni mwaliko kwa Wakristo, kama Kanisa kuomba neema na baraka za toba na wongofu wa kichungaji na kimisionari, kama ilivyokuwa kwa Mtume Petro na wenzake, walivyoitwa kuacha nyavu zao na kumfuasa Kristo Yesu ili waweze kuwa ni wavuvi wa watu, kwa kumpenda Kristo Yesu, tayari kuwachunga na kuwalisha kondoo wake. Jambo la msingi kwa waamini ni kujiuliza ikiwa kama kweli wana upendo wa dhati kwa Kristo Yesu, kiasi hata cha kusikia shauku ya kumtangaza na kumshuhudia; kwa kujibidiisha kukutana naye katika: Neno, Sakramenti na Maisha ya Sala. Je, kama waamini wanajisikia kutoka katika undani wa maisha yao, ile furaha ya Injili inayoleta mageuzi na maboresho katika maisha? Huu ni mwaliko wa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha
Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha

Mwishoni mwa Katekesi yake, Baba Mtakatifu ametoa wito kwa Israeli na Palestina kusitisha mapigano mara moja, kwani kuna watu wengi wanaoteseka kutokana na vita inayoendelea huko Ukanda wa Gaza. Anawahimiza wahusika wakuu katika vita hii kurejea tena kwenye mazungumzo pamoja na kuweka mikakati itakayosaidia mateka na wafungwa wa kivita kuachiliwa huru mara moja, ili kuendeleza matumaini yaliyojitokeza baada ya siku za hivi karibuni kusitisha vita. Kwa hakika, anasema Baba Mtakatifu Francisko haya ni mateso makubwa kwa Waisraeli na Wapalestina.

Papa Ushuhuda wa Injili
13 December 2023, 15:43

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >