Tafuta

Katekesi: Shauku ya Uinjilishaji: Ushuhuda wa Padre Matteo Ricci

Padre Matteo Ricci, SJ ni mfano wa ari na mwamko wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini China ambaye alitumia ujuzi wake wa hisabati na unajimu ili kutamadunisha Injili nchini China. Huu ni mwaliko wa kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda unaojengwa kwenye urafiki wa kijamii na majadiliano ya kidugu, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni mfano bora katika kutangaza na kushuhudia imani tendaji katika uhalisia wa maisha ya waamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume. Rej. Mt 9:9-13. Hii ndiyo tema inayoongoza Mzunguko Mpya wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 11 Januari 2023. Hii ni tema ya dharura na madhubuti kwa maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwa, jumuiya ya waamini inazaliwa kwa sababu ya utume na umisionari, huku ikisukumwa na Roho Mtakatifu, waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Huu ndio mwelekeo na dira ya utume na maisha ya Kikristo, vinginevyo, Wakristo wanaweza kujikuta wakijitafuta wao wenyewe katika ubinafsi wao. Bila ya kuwa na shauku ya uinjilishaji, imani itadhohofu na hatimaye, kunyauka na utume ndicho kiini cha maisha ya mwamini. Kumbe, mzunguko mpya wa katekesi ni kutaka kupyaisha shauku ya uinjilishaji kwa kuzama zaidi katika Maandiko Matakatifu sanjari na Mafundisho Tanzu ya Mama Kanisa ili kuchota amana na utajiri wa ari, mwamko na bidii ya kitume. Katika mzunguko huu wa Katekesi, Baba Mtakatifu anasema, atajitahidi kuweka mbele ya waamini mifano hai na baadhi ya mashuhuda wa imani, walioamsha shauku ya Habari Njema ya Wokovu, ili wawasaidie waamini kuwasha tena ule moto wa Roho Mtakatifu, ili hatimaye, uweze kuzijaza nyoyo za waamini wote mapendo. Ni katika muktadha huu, wakristo wanapaswa kujitahidi katika maisha yao ya kila siku kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Kristo Yesu unaoganga, kuponya na kuwaokoa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Ushuhuda wa uinjilishaji kadiri ya Padre Matteo Ricci
Ushuhuda wa uinjilishaji kadiri ya Padre Matteo Ricci

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni ameelezea ushuhuda wa Mtakatifu Francisko Xsaveri aliyetenda yote katika hali ya ufukara, ujasiri na shauku ya kutangaza, kuishi na kuieneza Injili. Huu ni mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kusoma alama za nyakati na kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa maisha: wawe na jicho linaloyaangalia mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu, tayari kuinjilisha huku wakiiga mfano wa Mtakatifu Francisko Xsaveri. Mwenyezi Mungu apende kuwajalia furaha ya kuinjilisha ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, chemchemi ya furaha, ari na moyo mkuu katika mchakato wa Uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 31 Mei 2023 imenogeshwa na Waraka wa Kwanza wa Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho: “Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi. Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria), ili niwapate walio chini ya sheria. Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria. Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu. Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine.” 1Kor 9:19-23.

Padre Matteo Ricci: Majadiliano, Urafiki wa kijamii na utamadunisho
Padre Matteo Ricci: Majadiliano, Urafiki wa kijamii na utamadunisho

Padre Matteo Ricci, SJ ni mfano wa ari na mwamko wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini China na ambaye alitumia ujuzi wake wa hisabati na unajimu ili kutamadunisha Injili nchini China. Huu ni mwaliko wa kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda unaojengwa kwenye urafiki wa kijamii na majadiliano ya kidugu, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa waja wake. Padre Matteo Ricci ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia imani tendaji. Alizaliwa tarehe 6 Oktoba 1552 huko Macerata nchini Italia. Akafariki dunia tarehe 11 Mei 1610 huko Peking, nchini China. Tarehe 17 Desemba 2022 akatangazwa kuwa ni Mtumishi wa Mungu. Alisoma kwenye shule za Wayesuit, akabahatika kujiunga nao na ndoto yake kubwa ilikuwa ni kwenda kufanya utume wa kimisionari huko Mashariki ya Mbali. Baada ya juhudi za Mtakatifu Francisko Xsaveri na wamisionari wenzake 25 kutaka kuingia nchini China, kugonga mwamba, Padre Matteo Ricci alijiandaa kikamilifu zaidi. Akajizatiti katika kusoma lugha ya Kichina pamoja na tamaduni zao, akabahatika kuishi miaka 18 akitangaza na kushuhudia Injili Kusini mwa China. Hii ni safari iliyomchukua hatua 4 kabla ya kuwasili jijini Peking. Kutokana na uvumilivu, udumivu na imani thabiti, Padre Matteo Ricci akafanikiwa kuvuka matatizo na changamoto, matatizo, kutoaminika pamoja na upinzani. Padre Matteo Ricci alijikita katika majadiliano ya kidini na ujenzi wa urafiki wa kijamii, mambo yaliyowawezesha watu wengi kumfungulia nyoyo zao na hivyo kupokea imani ya Kikristo. Alijitamadunisha, akaamua kuishi maisha ya kichina, akajifunza kwa dhati kabisa lugha ya Kichina; “akajipinda” kusoma machapisho ya Kichina, ili kuweza kufanya majadiliano ya kidini na kitamaduni.

Padre Matteo Ricci alijiandaa kwa ajili ya uinjilishaji China.
Padre Matteo Ricci alijiandaa kwa ajili ya uinjilishaji China.

Tangu karne ya kwanza, Kanisa lilijitahidi kufanya majadiliano ya kidini pamoja na utamadunisho wa utamaduni wa Kigiriki. Padre Matteo Ricci alikuwa amejiandaa vyema kitaaluma na kisayansi, kiasi cha kukonga nyoyo za wasomi wa Kichina, bila kusahau ramani yake ya dunia. Hapa kulikuwa na maboresho makubwa ya sayansi na tamaduni kati ya Mashariki na Magharibi, kielelezo cha ufanisi mkubwa, kielelezo makini cha majadiliano katika ufariki wa kijamii. Haya ni matokeo ya ushirikiano mkubwa kati ya Padre Matteo Ricci na watu mashuhuri kama vile “Dokta Paolo: Xu Guangqi pamoja na “Dokta Leone: Li Zhizao.” Ari na mwamko wa Padre Matteo Ricci ulikuwa ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na imani ya Kikristo inayosimikwa katika majadiliano ya kisayansi na wanasayansi; alitangaza na kushuhudia kanuni maadili na utu wema, yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na dunia, bila kusahau Mafundisho tanzu ya Kanisa. Padre Matteo Ricci akatangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya kitawa na kimisionari hata kwa njia ya sala, mahubiri na matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika hali ya unyenyekevu wa Kiinjili. Mahubiri na mtindo wake wa maisha, ulikuwa ni ushuhuda wa imani tendaji, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni wainjilishaji kwa njia ya mifano bora ya maisha yao. Mwishoni mwa maisha yake ya hapa duniani, alijawa furaha ya ajabu ya kutaka kukutana na Muumba wake, lakini alisikitika kuacha utume wake wa uinjilishaji na huduma ambayo bado angeifanya kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kama ilivyokuwa kwa Mtume Paulo, Mwalimu wa Mataifa. Padre Matteo Ricci, akafariki dunia kunako mwaka 1610 akiwa na umri wa miaka 57. Ameacha amana na urithi mkubwa wa ari na mwamko wa kimisionari; upendo kwa watu wa Mungu nchini China na ushuhuda angavu kama Padre, Mmisionari na Mkristo. Mnajimu aliyebobea, aliyefanikiwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo nchini China. Ameonesha udumifu katika maisha na wito wake wa kumfuasa Kristo Yesu!

Padre Matteo Ricci

 

 

 

 

31 May 2023, 15:09

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >