Tafuta

Papa Francisko: Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee: Ushuhuda wa Imani na Matumaini

Baba Mtakatifu Francisko anasema uzee ni muda uliokubalika wa kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko; unaosimikwa katika furaha na matumaini. Uzee unawasogeza waamini karibu na jirani zao pamoja na Ufalme wa Mungu, zaidi ya uwezo wa nguvu, maneno na misukumo ya ujana, kuelekea ukomavu katika maisha. Wazee washirikishwe katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya 37 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa nchini Canada kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 30 Julai 2022 imenogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo hasa lilikuwa ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa; kwa kuzingatia ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Baba Mtakatifu, kwa niaba ya Mama Kanisa aliomba tena msamaha unaopania kuleta mwanga angavu wa hija ya: toba, wongofu wa ndani, matumaini na upatanisho wa Kitaifa. Nia ni kuleta utakaso wa kumbukumbu na hatimaye, kuendelea kujikita katika uinjilishaji wa kina unaosimikwa katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 3 Agosti 2022 kwenye Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican alirejea tena kwenye hija yake ya kitume nchini Canada, tofauti kabisa na hija ambazo amewahi kuzifanya kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Aligusia kuhusu hija ya upatanisho, kumbukumbu ya tamaduni, mila na desturi njema za watu asilia wa Canada, Upatanisho na Uponyaji wa Kitaifa, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini inayosimikwa katika utamadunisho, ili kupyaisha kumbukumbu, unabii, mahusiano na mafungamano ya dhati kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya.

Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee katika maisha.
Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee katika maisha.

Baba Mtakatifu Francisko tangu Jumatano tarehe 23 Februari 2022 alianzisha mzungumko mpya wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee. Wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 10 Agosti 2022 amesema kwamba, kwa sasa anafikia hatima ya katekesi hizi, kwa kuzama katika Maandiko Matakatifu yanayomwonesha Kristo Yesu kuwa ni njia ya kwenda kwa Baba wa milele, akisema “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.” Yn 14:1-3. Kristo Yesu tayari alikwisha mwambia Mtume Petro kwamba, baadaye atamfuata kule anakokwenda, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu. Kristo Yesu alitambua udhaifu wa imani, ushuhuda na changamoto za ujenzi wa udugu wa kibinadamu miongoni mwao. Huu ni wosia mzito ambao waamini wanapaswa kuufanyia tafakari ya kina! Baba Mtakatifu Francisko anasema uzee ni muda uliokubalika wa kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko; unaosimikwa katika furaha na matumaini. Uzee unawasogeza waamini karibu na jirani zao pamoja na Ufalme wa Mungu, zaidi ya uwezo wa nguvu, maneno na misukumo ya maisha ya ujana, kuelekea ukomavu katika maisha.

Ingependeza kuona kwamba, katika Makanisa mahalia kuna kuwepo na nafasi muhimu inayohusianishwa na huduma hii maalum kwa waamini kumngoja Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu, kwa kuhimiza karama za watu binafsi na zile za kijumuiya kwa ajili ya wazee. Wazee waliokata tamaa kwa kuangalia pia fursa walizokosa katika maisha ni hatari kwa wengine. Wazee wanapaswa kuuishi uzee wao kwa upole na heshima, huku wakiendelea kuthamini maisha na hivyo kufuta dhana potofu la kuona Kanisa linalomezwa na Malimwengu, kwa kudhani kwamba, kwa njia hii linaweza kutawala katika ukamilifu na utimilifu wake. Dhana hii inapaswa kuwekwa kando na kuanza kujielekeza zaidi kwenye Fumbo la Pasaka linalofumbata: mateso, kifo na kupaa kwake mbinguni, jambo ambalo limewezeshwa na Kristo Yesu mwenyewe kwa ajili ya waja wake. Maisha kamwe hayawezi kufumbatwa katika ubinafsi na uchoyo. Waamini wakumbuke kanuni hii kwamba, “Wakati ni bora zaidi kuliko nafasi. Hii ni sheria ya mwanzo wa maisha ya mwanadamu ambayo yanapata hatima yake mbinguni, pembeni mwa Mwenyezi Mungu, milele yote. Duniani ni mahali pa kupyaisha maisha ya mwanadamu, kwa kujifunza kutambua zawadi ya Mungu, kuheshimu wajibu wa kushiriki na kuwawezesha watu kuzaa matunda yanayokusudiwa kutoka kwa kila mtu. Maisha ya hapa duniani iwe ni fursa ya kutekeleza dhamana hii. Tabia ya majigambo na majivuno ya kutaka kusimamisha muda ili kuendeleza ujana, kutaka ujana wa milele, ustawi usiokuwa na kikomo na nguvu kamili bila kuyumba ni uganganyifu wa hali ya juu kabisa na kwamba, hili ni jambo ambalo haliwezekani.

Uzee ni muda wa ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo yenye mvuto.
Uzee ni muda wa ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo yenye mvuto.

Uwepo wa watu duniani ni mchakato wa kuanzisha safari ya maisha inayopata utimilifu wake mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwanadamu katika maisha yake si mkamilifu na ukamilifu huu unapata hatima yake mbele ya Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Uzee ni husogeza karibu tumaini hili na hatima yake. Uzee unatambua fika mapungufu, changamoto na fursa mbalimbali zinazoweza kupatikana. Uzee ni wakati wa kufurahia maisha, kuendelea kupyaisha imani na matumaini. Ulimwengu wa Mwenyezi Mungu ni wakati unaopita vizuizi na vizingiti vyote. Kristo Yesu, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, wakati wa Karamu ya Mwisho, aliwadhihirishia Mitume wake lengo la ukamilifu na utimilifu wa maisha aliposema, “Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.” Mt 26: 29. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mahubiri kuhusu Paradiso yamesheheni: heri, mwanga na upendo, ni haki na kweli, labda kuna haja ya kunogesha kidogo kwa kuongeza maisha kama anavyokaza kusema Kristo Yesu.

Mwishoni mwa katekesi yake, Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuuishi uzee wao wakiwa na matumaini ya kukutana na Mwenyezi Mungu, kama “msamaha” unaofumbatwa katika imani ambayo ni msingi na tumaini la waamini. Rej. 1 Pt 3: 15. Uzee ni safari ya kuelekea kwenye mbingu mpya na nchi mpya, Mji Mtakatifu wa Mungu, yaani Yerusalemu mpya kama inavyochambuliwa na Mtume Yohane katika Kitabu chake cha Ufunuo sura ya 21-22. Uzee ni awamu ya mwisho ya maisha ya mwanadamu inayofaa kutangaza na kushuhudia furaha na kwamba, maisha ni mwanzo wa safari ya utilivu. Maisha bora zaidi bado yanakuja. Sawa na kwenye Mtori, unaambiwa “Dogo kunywa supu, nyama iko chini.”

Papa Katekesi Uzee
10 August 2022, 16:47

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >