Tafuta

Katekesi Kuhusu Maana na Thamani Ya Uzee: Fumbo la Kifo!

Papa Francisko: Haya ni maono ya Nabii Danieli yanayochotwa tena na Mwinjili Yohane katika Kitabu chake cha Ufunuo na kumweka Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni: Masiha, Kuhani na Mfalme; Alfa na Omega na kwamba, nyakati zote ni zake, Alikuwa amekufa, lakini amefufuka sasa yu hai milele yote. Ni mshindi dhidi ya hofu ya kifo na uchungu wa moyo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tangu Jumatano tarehe 23 Februari 2022 alianzisha mzunguko wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee ambazo kwa sasa zinafikia hatima yake kwa kuzama katika Maandiko Matakatifu yanayomwonesha Kristo Yesu kuwa ni njia ya kwenda kwa Baba wa milele, akisema “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.” Yn 14:1-3. Kristo Yesu tayari alikwisha mwambia Mtume Petro kwamba, baadaye atamfuata kule anakokwenda, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu. Kristo Yesu alitambua udhaifu wa imani, ushuhuda na changamoto za ujenzi wa udugu wa kibinadamu miongoni mwao. Huu ni wosia mzito ambao waamini wanapaswa kuufanyia tafakari ya kina! Baba Mtakatifu Francisko anasema uzee ni muda uliokubalika wa kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko; unaosimikwa katika furaha na matumaini. Uzee unawasogeza waamini karibu na jirani zao pamoja na ushiriki mkalifu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu, zaidi ya uwezo wa nguvu, maneno na misukumo ya maisha ya ujana, kuelekea ukomavu katika maisha.

Kristo Yesu ni Alfa na Omega, Nyakazi zote ni zake.
Kristo Yesu ni Alfa na Omega, Nyakazi zote ni zake.

Ifuatayo ni Ndoto ya Nabii Danieli: Hukumu mbele ya Mzee wa Kale: “Nikatazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa.” Dan 7:9-10. Hii ni sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyonogesha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 17 Agosti 2022 Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee, akikazia zaidi kuhusu “Siku za uzee kama uhakika wa maisha yasiyokuwa na mwisho.” Haya ni maono ya Nabii Danieli yanayochotwa tena na Mwinjili Yohane katika Kitabu chake cha Ufunuo na kumweka Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni: Masiha, Kuhani na Mfalme; Alfa na Omega na kwamba, nyakati zote ni zake, Alikuwa amekufa, lakini amefufuka sasa yu hai milele yote. Ni mshindi dhidi ya hofu ya kifo na uchungu wa moyo.

Huu ni ufunuo unaofafanua mzunguko wa maisha ya mwanadamu, historia ya Mwenyezi Mungu pamoja na kazi ya uumbaji yote haya yakifungwa pamoja katika uzee. Katika katekesi yake, Baba Mtakatifu amejielekeza zaidi kuhusu uzee kama ushuhuda na baraka kwa watoto; ni kielelezo cha agano kati ya wazee na watoto na kwamba, kifo ni mwanzo wa maisha ya uzima wa milele. Maono kuhusu uzee huwasilisha hisia za nguvu, heshima, uzuri na haiba na Neno linalotumika kuelezea “Uzee” katika Maandiko Matakatifu ni “Zaqen” maana yake “Ndevu, nywele nyeupe” ishara ya uzee, kumbukumbu endelevu na uwepo wa milele. Hii ni picha inayoheshimiwa sana kwenye Maandiko Matakatifu na Nabii Danieli anasema, huyu ndiye yule “Mzee wa Siku, kielelezo cha umilele wa Mwenyezi Mungu. Makanisa ya Mashariki, kila mwaka ifikapo tarehe 2 Februari yanaadhimisha Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni. Na hii ni moja ya Sikukuu kumi na mbili zinazoadhimishwa katika Mwaka wa Liturujia ya Kanisa. Huu ni mkutano kati ya Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ambaye ni Mwana wa Baba wa Milele na Binadamu wanaowakilishwa na Mzee Simeoni na Anna. Kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria wa Trastevere, Jimbo kuu la Roma, kuna picha nzuri sana inayoonesha tukio hili la kihistoria.

Uzee unapata utimilifu wake katika kazi ya uumbaji
Uzee unapata utimilifu wake katika kazi ya uumbaji

Katika Liturujia ya Madhehebu ya Kibizantina, Askofu anasali pamoja na Mzee Simeoni akisema: “Huyu ndiye aliyezaliwa na Bikira Maria: Yeye ni Neno wa Mungu, Ni Mungu kweli kutoka kwa Mungu, Aliyezaliwa bila kuumbwa ili kumkomboa mwanadamu. Kristo Yesu ni mlango wa mbinguni, Neno wa Baba wa milele na Mungu kweli ambaye kwa kadiri ya sheria alitolewa Hekaluni na Bikira Maria mbele ya wazee Simeoni na Anna. Mzee Simeoni akambeba Mtoto Yesu mikononi mwake.” Haya ni maneno yanayochota utajiri wake kutoka kwenye kiri ya imani ya Mitaguso mikuu minne ya kwanza inayodhihirisha ile imani ya uekumene wa Makanisa yote. Mzee Simeoni ni kielelezo cha uzee mkamilifu na wenye kutukuka, anampokea Mtoto Yesu kielelezo makini cha watoto wote wanaozaliwa ulimwenguni kama zawadi safi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni kielelezo cha mshikamano wa udugu wa Kristo Yesu na watu wote kwani ni Mwana aliyezaliwa katika urafiki wa karibu na Mwenyezi Mungu, tangu milele yote. Hii ni ishara ya uzee unaofumbatwa na kupata utimilifu wake katika kazi ya uumbaji na hatimaye, utaweza kung’ara kama ilivyokuwa ishara ya Simeoni na Anna, waliobahatika kuonana na Masiha wa Bwana, kabla ya kupatwa na mauti.

Watoto ni zawadi safi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Watoto ni zawadi safi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, uzee ni ushuhuda na baraka kwa watoto, ni mwanzo mwema, unaonesha uzuri na ugumu katika fumbo la maisha ya mwanadamu yanayodumu milele yote na wala hakuna anayeweza “kuyafyekelea mbali” hata kifo chenyewe kimeshikishwa adabu! Ushuhuda wa wazee anasema Baba Mtakatifu Francisko ni wa kuaminika kwa watoto, hii ni kazi njema inayoweza kutekelezwa na wazee ambao ni chemchemi ya baraka. Ni kiungo cha umri wa maisha ya mwanadamu na kipimo cha nyakati. Hii ni changamoto ya kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya mwanadamu. Kristo Yesu, Neno wa Baba wa Milele ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, Nyakati zote ni zake. Kumbe, hakuna mtu awaye yote anayeweza kutengwa na nguvu, ukaribu na upendo wake wa daima. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mshikamano kati ya wazee na watoto utaokoa familia ya kibinadamu. Wazee wanahimizwa kuwa kweli ni mashuhuda wa neema na baraka ya uzee. Fumbo la kifo ni gumu kuweza kupokelewa katika maisha ya mwanadamu, lakini ni hatua inayofunga sehemu ya maisha na kufungua mlango wa maisha ya uzima wa milele. Vijana na wazee wajenge na kudumisha majadiliano katika ukweli, huku wakichota neema na baraka kutoka kwa wazee, kwani kwa hakika wazee wenye hekima na busara ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu.

Papa Uzee na Kifo
17 August 2022, 15:38

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >