Tafuta

Amani Ya Bwana Ni Zawadi Ya Fumbo La Pasaka Ya Bwana

Amani ni zawadi ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Hii ni amani ambayo imetundikwa katika upya wa maisha; katika upole na unyenyekevu wa moyo. Kristo Yesu alikwisha kuwaambia wafuasi wake kwamba “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapayo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo” Yn 14:27. Tafuteni amani ya kweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dominika ya Matawi, Kanisa limeadhimisha Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa utukufu aliyeingia mjini Yerusalemu. Ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Kuingia kwa Kristo Yesu mjini Yerusalemu kunaonesha ujio wa Ufalme wa Mungu: Ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anakumbusha kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu. Dominika ya Matawi, ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, ambamo Mama Kanisa anatafakari mafumbo makuu ya ukombozi wa mwanadamu. Kristo Yesu anaingia mjini Yerusalemu na kupokelewa kwa shangwe kuu, huku watoto wa Wayahudi wakitandaza nguo zao njiani, huku wakipiga kelele na kusema, “Ndiye Mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu.” Lk 19:38. Watu wanashangilia kwa kumwona Mfalme mpya akiingia mjini Yerusalemu, ndiye atakayewaletea amani na utukufu; atakayewaokoa watu wake kutoka mikononi mwa utawala wa Kirumi. Kimsingi hawa ni watu waliokuwa na ndoto ya amani jamii na kumwona Kristo Yesu kuwa ni kielelezo cha amani hii waliyokuwa wanaitamani. Walitambua nguvu na uweza wa kuwalisha wenye njaa pamoja na kutenda miujiza na ishara kuu zilizoonesha maajabu ya Mungu ndani mwake; na kwa njia hii, angeweza kuwaletea watu wake haki na amani!

Dominika ya Matawi ni Mwanzo wa Juma Kuu
Dominika ya Matawi ni Mwanzo wa Juma Kuu

Amani ni zawadi ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Hii ni amani ambayo imetundikwa katika upya wa maisha; katika upole na unyenyekevu wa moyo. Kristo Yesu alikwisha kuwaambia wafuasi wake kwamba “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapayo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo” Yn 14:27. Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 13 Aprili 2022, kama sehemu ya maandalizi ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana kwa mwaka 2022. Amani inayotolewa na Kristo Yesu wakati wa Sherehe ya Pasaka ni amani ambayo ni kinyume kabisa cha matumizi ya nguvu, wala ushindi wa kulazimisha. Amani ya Kristo Yesu inajikita katika njia ya upole, Msalaba na huduma. Kwa hakika Kristo Yesu amechukua, maovu, dhambi na kifo cha mwanadamu. Amani ya Kristo ni kielelezo cha sadaka na majitoleo yake binafsi. Ni amani ambayo inakita mizizi yake katika upole na ujasiri, lakini ni amani ambayo si rahisi kupokeleka na walimwengu. Kristo Yesu alipokelewa kwa shangwe kuu na umati mkubwa wa watu waliofurika na kujipanga njiani. Lakini anapokamatwa na kushtakiwa kwa uwongo ni umati ule ule unaogeuka na kuanza kupiga tena kelele wakisema “Mwondoe mwondoe Msulubishe.”

Kristo Yesu anashutumiwa kwa kupingana na Kaisari aliyekuwa ni Mfalme mwenye nguvu na mamlaka makubwa katika ulimwengu wa nyakati zake. Kaisari alikuwa na uwezo kabisa wa kumwachia huru Kristo Yesu, lakini akaamua kutumia nguvu kubwa zaidi kama njia ya kutatua matatizo yaliyojitokeza na wala hakutamani kuona amani kutoka kwa Kristo Yesu inatawala. Kristo Yesu akakubali kuvikwa mavazi mekundu alama ya utukufu na sifa na hatimaye, kupokea hukumu ya maisha yake. Hivi ndivyo mambo yanavyokwenda, na hivyo kukosekana kwa amani ya kweli. Leo hii katika ulimwengu mamboleo historia inajirudia tena na tena kwa kuendeleza kile kishawishi cha kuwa na amani isiyo ya kweli. Hii ni amani ambayo kimsingi inatundikwa katika nguvu na madaraka ya kijeshi, inayowaelekeza watu kwenye chuki na uhasama na matokeo yake ni kumsaliti Mwenyezi Mungu. Aliulizwa maswali mengi, lakini hakujibu chochote, kimya kikuu kikatawala. Walidhani amani ya Kristo Yesu inasimikwa katika nguvu na mabavu dhidi ya watu wengine. Baba Mtakatifu Francisko anasema, silaha za Injili ya Kristo Yesu zinafumbatwa katika: Sala, huruma, msamaha na upendo kwa jirani. Na hivi ndivyo amani ya Kristo Yesu inavyotangazwa na kushuhudiwa ulimwenguni. Vita, machafuko na kinzani zinazoendelea sehemu mbalimbali za dunia ni kinyume kabisa na ni kashfa kubwa dhidi ya Pasaka ya Bwana. Kristo Yesu kabla ya kuhitimisha Pasaka yake ya Mwisho, aliwaambia wafuasi wake kutofadhaika mioyoni mwao na wala wasiwe na woga. Hii ni kutokana na ukweli kwamba nguvu na mamlaka za watawala wa ulimwenguni huu mara nyingi zimetumika kusababisha uharibifu na maafa kwa watu na mali zao.

Amani ya Bwana ni Zawadi ya Fumbo la Pasaka.
Amani ya Bwana ni Zawadi ya Fumbo la Pasaka.

Lakini, amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ni kwa ajili ya ujenzi wa historia ya mwanadamu inayopata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya moyo wa binadamu, kwa wale wanaoipokea na kuiambata. Ni katika mantiki hii, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Pasaka ni Sherehe ya kweli ya Mungu na mwanadamu, kwa sababu, hii ni Pasaka ambayo Kristo Yesu ameitolea sadaka kwa mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Ndiyo maana ile Siku ya kwanza ya Juma alipowatokea wafuasi wake aliwaambia “Amani iwe kwenu” Yn 20: 20.21. Pasaka katika asili yake maana yake kwa Lugha la Kilatini: Pasqua, Pascha, "Kupita juu” Kwa lugha ya Kigiriki πάσχα (pascha), na kwa Kiharamayo פסח (pesach). Huu ni mwaliko wa pekee kwa Pasaka ya Mwaka 2022 kupita juu ya miungu wa dunia hii na kumwendea Mungu wa kweli; ni mwaliko wa kutoka katika chuki na uhasama ni kuanza kujikita katika upendo unaowaweka huru; badala ya kutegemea amani inayofumbatwa kwenye mtutu wa bunduki, watu wa Mungu waanze kujielekeza katika ushuhuda wa amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawaalika waaamini kusimama mbele ya Msalaba, chemchemi ya amani na wamwombe Kristo Yesu aweze kuwakirimia amani katika nyoyo zao, amani kwa ajili ya ulimwengu.

Pasaka ya Bwana
13 April 2022, 14:52

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >