Tafuta

Katekesi Kuhusu Maana na Thamani Uzee: Maisha Marefu: Alama na Fursa

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Maana na Thamani ya Uzee ameongozwa na tema kuhusu: Maisha marefu: Ni alama na fursa ya kutafakari kuhusu maana ya maisha; Mwingiliano kati ya vijana na wazee; madhara ya janga la UVIKO-19 pamoja na maisha ya mwanadamu kuwa ni marefu. Yote haya yatafakariwe kama sehemu pia ya historia ya kazi ya Uumbaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mzungumko mpya wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee, Jumatano tarehe 2 Machi 2022 umenogeshwa na sehemu ya Neno la Mungu linaonesha orodha ya wazawa wa Adamu: “Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya; mwanamume na mwanamke aliwaumba, akawabariki akawaita jina lao Adamu, siku ile walipoumbwa. Adamu akaishi miaka mia na thelathini, akazaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita jina lake Sethi. Siku za Adamu baada ya kumzaa Sethi zilikuwa miaka mia nane, akazaa wana, waume na wake. Siku zote za Adamu alizoishi ni miaka mia kenda na thelathini, naye akafa.” Mwa 5: 1-5. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Maana na Thamani ya Uzee ameongozwa na tema kuhusu: Maisha marefu: Ni alama na fursa ya kutafakari kuhusu maana ya maisha; Mwingiliano kati ya vijana na wazee; madhara ya janga la UVIKO-19 pamoja na maisha ya mwanadamu kuwa ni marefu. Sehemu ya Maandiko Matakatifu imebainisha kuhusu maisha marefu kadiri ya Maandiko Matakatfu ni kama njia ya kurithisha maisha ya mwanadamu mintarafu kazi ya Uumbaji.

Majadiliano kati ya marika mbalimbali ni muhimu kwa mafungamano ya kijamii
Majadiliano kati ya marika mbalimbali ni muhimu kwa mafungamano ya kijamii

Huu ni mwanzo wa historia ya kazi ya uumbaji inayomtambua Mwenyezi Mungu kuwa ni chemchemi ya roho na maisha ya mwanadamu kwa kuwa na dhamiri hai pamoja na uhuru; mang’amuzi na uwajibikaji mpana. Maisha ya mwanadamu yanakita mizizi yake katika sura na mfano wa Mungu; udhaifu wake wa kibinadamu na hatimaye, kifo. Haya ni mambo msingi ambayo mwaamini anapaswa kuyafahamu. Muda mrefu kiasi hiki unamwezesha mwanadamu kukuza na kuboresha maisha yake ya kiroho. Huu ni mwaliko wa kuangalia tena maana ya maisha na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza hasa katika nyakati hizi. Maisha marefu yamewawezesha wanadamu kuwa na kumbukumbu kubwa ya tamaduni zake, tayari kukabiliana na yale mapya yanayojitokeza kwa kutambua kwamba, kwa sasa muda wa kurithisha tunu na amana hizi ni kidogo na umwilishaji wake unahitaji uvumilivu mkubwa. Mwendokasi unaonekana kuwakanganya wengi, kiasi cha kuwaacha watu wengi wakiwa wananingia kwenye ombwe, kiasi cha kukosa virutubisho vinavyotakiwa. Vijana wa kizazi kipya anasema Baba Mtakatifu Francisko ni wahanga wa mwendokasi unaopimwa kwa saa, lakini muda wa kuishi unahitaji maboresho makubwa. Maisha marefu yanawawezesha watu kupata uzoefu mpana zaidi na kuona pia hasara ya kuishi kwa muda mfupi.

Uzee unawataka watu kwenda taratibu, kwa kutambua amana na thamani ya maisha bila ya haraka kwani hakuna hata sababu msingi za kufanya hivyo. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, ameamua kuanzisha Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani inayoadhimishwa Dominika ya mwisho ya Mwezi Julai ya kila mwaka. Lengo ni kujenga na kuimarisha mafungamano ya marika kati ya wazee, vijana na watoto, ili kusaidiana na hatimaye, kurithishana amana na utajiri wa maisha yao kwa ajili ya mafao mapana ya familia ya binadamu. Huu ni mchakato unaopania kukuza na kudumisha majadiliano ya kina kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, vinginevyo kuna hatari kubwa kwa wazee kutengwa na hivyo vijana kukosa mizizi ya amana na utajiri kutoka kwa wazee, matokeo yake, vijana wanaweza kukengeuka. Mwingiliano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee ni muhimu sana kwa ajili ya wakazi wa dunia hii, kwani wote wanageuka kuwa ni chemchemi ya nguvu inayoonekana na ile isiyoonekana.

Mshikamano upendo na urafiki ni muhimu sana katika jamii.
Mshikamano upendo na urafiki ni muhimu sana katika jamii.

Mwendokasi ni hatari sana kwa maisha. Kuna haja kwa wazazi na walezi kupoteza muda kwa kuzungumza na watoto wao, ili kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia. Wazee wajitahidi kupoteza muda kwa kuzungumza na vijana wa kizazi kipya ili kuwasaidia kuona maana halisi ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yamevuruga mshikamano, upendo na urafiki kati ya wazee na wajukuu wao. Upendo unapaswa kunogesha mahusiano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, kwa kutambua kwamba, haraka haraka haina baraka. Upendo wa dhati unarithishwa polepole katika maisha na hatimaye, wazee nao wanajiandaa polepole kuungana na Mwenyezi Mungu, kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Leo hii, takwimu zinaonesha kwamba, binadamu ana uwezo wa kuishi muda mrefu zaidi ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita.

Maana halisi ya maisha inafumbatwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi pale mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango na mapenzi ya Mungu. Mwishoni mwa Katekesi yake Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ili kutambua maana na thamani ya uzee, waamini hawana budi kuomba hekima na nguvu kutoka kwa Roho Mtakatifu ili kila mtu awezwe kutambua na kuthamini mwendo wake wa maisha. Vijana na wazee wajenge utamaduni wa kujadiliana, ili kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa maisha. Vinginevyo, wazee watajikuta wametengwa na hatimaye, kutumbukia katika ugonjwa wa sonona na huo ni mwanzo wa kuelekea kaburini. Mwenyezi Mungu awajalie wazee na vijana kupata uwiano, mwingiliano, mshikamano na mafungamano ya dhati kati ya watoto, vijana na wazee ili wote waweze kujikita katika maisha kwa ajili ya majadiliano ya kweli.

Katekesi Uzee

 

02 March 2022, 16:53

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >