Tafuta

Katekesi Kuhusu Mtakatifu Yosefu: Ushirika Wa Watakatifu: Kanisa

Ushirika wa Watakatifu ni sehemu ya kiri ya imani ya Kanisa kwa kutambua ushirika wa mema ndani ya Kanisa kunakofanyika kwa njia ya Sakramenti pamoja na kuchota katika hazina ya pamoja. Huu ni ushirika wa mambo matakatifu na ushirika kati ya watakatifu. Ni ushirika wa imani, Sakramenti za Kanisa. Ni ushirika wa upendo katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. USHIRIKA.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yalizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na kufungwa rasmi tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ubunifu na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika wa Bwana.

Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Baba Mtakatifu Francisko alianzisha mzunguko wa Katekesi Kuhusu Mtakatifu Yosefu ambaye kimsingi ni msaada, faraja na msimamizi. Baba Mtakatifu amekwisha kugusia kuhusu: Mtakatifu Yosefu na mazingira alimoishi kadiri ya Maandiko Matakatifu; mjini Bethlehemu mahali alipozaliwa Kristo Yesu kama utimilifu wa Unabii. Nazareth ni mahali alipokulia Yesu. Hii ni miji miwili yenye uhusiano wa karibu sana na maisha ya Mtakatifu Yosefu. Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo inaelezea kuhusu Ukoo wa Kristo Yesu: 1: 12-16. Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inamwonesha Mtakatifu Yosefu katika historia ya wokovu. Wainjili wote wanamtambua Yosefu kuwa ni Baba Mlishi wa Kristo Yesu, aliyekuja hapa ulimwenguni kutimiza historia ya Agano Jipya na la milele na kwamba, historia ya wokovu inayojenga mahusiano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Kwa Mwinjili Mathayo, historia ya wokovu inapata chimbuko lake kwa Abrahamu, lakini Mwinjili Luka anakwenda mbali zaidi hadi kufikia asili ya mwanadamu yaani Adamu.

Ushirika wa Watakatifu sehemu ya kiri ya imani ya Kanisa
Ushirika wa Watakatifu sehemu ya kiri ya imani ya Kanisa

Mwinjili Mathayo anawasaidia waamini kumwelewa Mtakatifu Yosefu, katika hali ya ukimya bila makuu, lakini, kiungo muhimu sana katika historia ya wokovu na moyo wa sala. Kimsingi, Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi kuhusu Mtakatifu Yosefu amekwisha kugusia mazingira alimoishi Mtakatifu Yosefu; Wajibu na dhamana yake katika historia ukombozi. Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mtu wa haki na mchumba wake Bikira Maria. Alikuwa ni mtu mkiya sana, aliyejitahidi kujifunza kwa kusikiliza na hivyo kumwachia Neno wa Mungu nafasi ya kuendelea kukua na kukomaa. Huu ni ukimya uliogeuzwa na kumwilishwa katika matendo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu alizaliwa katika mazingira duni na maskini na kwamba, unyenyekevu ndiyo njia inayowapeleka waamini kwa Mungu Baba wa mbinguni. Mtakatifu Yosefu alijisadaka sana ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu. Akalazimika kukimbilia nchini Misri na kukaa huko kama mkimbizi, kashfa inayoendelea kujitokeza hata katika ulimwengu mamboleo. Mtakatifu Yosefu alidhulumiwa, lakini alionesha ujasiri mkubwa kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kwa hakika Mtakatifu Yosefu alikuwa ni Baba Mlishi wa Yesu. Mwinjili Mathayo anamwelezea Mtakatifu Yosefu kwamba, alikuwa mumewe Mariamu aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo. Mt. 1:16. Mwinjili Luka kwa upande wake anakazia kwamba, Kristo Yesu alipelekwa Hekaluni “kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana” Lk 3:23. Kumbe, Wainjili wanakazia dhamana na nafasi ya Mtakatifu Yosefu kama Baba Mlishi wa Mtoto Yesu. Katika Mapokeo ya Kale, jina la mtu lilikuwa ni muhtsari wa mtu. Kumbe, mtu kubadilisha jina, kulimaanisha mabadiliko katika mtu huyo. Tangu mwanzo, Mtakatifu Yosefu alipashwa habari kuhusu Bikira Maria na kuzaliwa kwa Mtoto ambaye ataitwa Yesu. Jina la Yesu maana yake ni Mungu anaokoa. Yeye ndiye atakaye waokoa watu na dhambi zao. Rej. Mt 1: 21. Mtakatifu Yosefu anaonesha kwamba, kitendo cha kuasili watoto ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa kibaba na kimama. Baba Mtakatifu Francisko amemwelezea Mtakatifu Yosefu kuwa ni Baba Mwenye Huruma, shuhuda amini wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; aliyejitaabiisha katika malezi, makuzi na elimu kwa Mtoto Yesu.

Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mtu wa ndoto, nyenzo iliyotumiwa na Mwenyezi Mungu kuwasiliana na waja wake. Kwa njia ya ndoto aliweza kutambulishwa kuhusu Fumbo la Umwilisho, akaokoa maisha ya Mtoto Yesu kwa kukimbilia Misri, kielelezo cha ujasiri wa wazazi unaosimikwa katika sala na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 2 Februari 2022 imenogeshwa na Neno la Mungu kutoka katika Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho 12: 12-13: Viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja: “Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.” Baba Mtakatifu amechambua kuhusu Mtakatifu Yosefu na Ushirika wa Watakatifu mintarafu Maandiko Matakatifu, Sala na Ibada kwa Mtakatifu Yosefu, ambaye katika historia ya Kanisa amekuwa ni msaada mkubwa kwa watu wa Mungu.

Ushirika wa Watakatifu sehemu ya kiri ya imani ya Kanisa
Ushirika wa Watakatifu sehemu ya kiri ya imani ya Kanisa

Ushirika wa Watakatifu “Sanctorum communio” ni sehemu ya kiri ya imani ya Kanisa kwa kutambua ushirika wa mema ndani ya Kanisa kunakofanyika kwa njia ya Sakramenti za Kanisa pamoja na kuchota katika hazina ya pamoja. Huu ni ushirika wa mambo matakatifu na ushirika kati ya watakatifu. Ni ushirika wa imani, Sakramenti za Kanisa, Karama katika mchakato wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Ni ushirika wa upendo unaosimikwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Ibada ya Kanisa kwa watakatifu wa Mungu, au visakramenti na hasa zaidi kwa Bikira Maria, ni kwamba, imani ya Kanisa inawaelekeza waamini kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Kristo Yesu unaofumbatwa katika kiungo cha ushirika wa watakatifu. KKK 946-962.

Kimsingi Kanisa ni Jumuiya ya watakatifu na wa dhambi wanaojitahidi kutubu na kumwongokea Mungu. Utakatifu ni matokeo ya huruma na upendo wa Mungu uliofunuliwa katika Kristo Yesu, anayetakatifuza kwa kuwapenda waja wake na hivyo kuwakomboa kutoka katika udhaifu wao wa kibinadamu. Kwa njia ya Kristo Yesu, wote wanafanyika kuwa ni sehemu ya viungo vyake. Kumbe, furaha, mateso na mahangaiko ya mwanajumuiya mmmoja ni mahangaiko na mateso ya Kanisa zima. Ushirika wa watakatifu ni kiungo cha nguvu kiasi kwamba, hata kifo hakiwezi kuwatenganisha. Ushirika wa watakatifu ni muungano wa Kanisa la Mbinguni na Duniani. Kanisa lina Ibada ya pekee kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na kwa Mtakatifu Yosefu. Waamini wanakimbilia sana ulinzi na tunza ya Bikira Maria na ya Mtakatifu Yosefu kwa sababu ya dhamana na utume wao kwa Kristo Yesu. Ushirika wa watakatifu unawawezesha waamini kujisikia kwamba, wanao walinzi na waombezi mbinguni, wanaoweza kuzungumza nao mubashara. Watakatifu ni mifano bora ya maisha na tunu msingi za Kikristo, ndiyo maana waamini wanakimbilia, kuomba ulinzi na maombezi yao.

Baba Mtakatifu Francisko amependa kuhitimisha Katekesi kuhusu Mtakatifu Yosefu na Ushirika wa watakatifu kwa sala ya Mtakatifu Yosefu ambayo amekuwa akiisali kwa takribani miaka 40 iliyopita. Hii ni sala ambayo inafumbatwa katika changamoto za maisha na utume wa Mtakatifu Yosefu, aliyepewa uwezo wa kufanya mambo yasiyowezekana yawezekane. Waamini wanamwomba ili aweze kuwasaidia nyakati za uchungu na ugumu wa maisha, kwa kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza yake, ili ziweze kupata suluhisho la furaha. Waamini wanapenda kuweka matumaini yao yote kwa Mtakatifu Yosefu, kwa kutambua kwamba, anaweza kila jambo kwa njia ya Kristo Yesu na Bikira Maria, changamoto kubwa kwa Mtakatifu Yosefu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kusali kwa ajili ya kumwombea mtu mmoja anayeonekana kuwa na changamoto za kiafya, kisaikolojia na kiimani, ili aweze kupata nafuu katika mateso yake. Sala ya pamoja na ni ushuhuda wa ushirika wa watakatifu.

Ushirika wa Watakatifu

 

02 February 2022, 16:49

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >