Tafuta

Mtakatifu Yosefu: Mlinzi, Msimamizi na Mwombezi wa Kanisa la Kristo!

Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake amejielekeza zaidi kuhusu maana ya Msimamizi, Mlinzi na Mwombezi wa Kanisa la Kiulimwengu, umuhimu wa kulipenda, kulilinda na kutemba pamoja na Kanisa licha ya dhambi na utakatifu wa watoto wake. Mtakatifu Yosefu awasaidie waamini ili waweze kuwa ni watangazaji wa kweli na mashuhuda wa Injili ya Kristo Yesu katika ukweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yalizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na kufungwa rasmi tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ubunifu na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika wa Bwana.

Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Baba Mtakatifu Francisko alianzisha mzunguko wa Katekesi Kuhusu Mtakatifu Yosefu ambaye kimsingi ni msaada, faraja na msimamizi. Baba Mtakatifu amekwisha kugusia kuhusu: Mtakatifu Yosefu na mazingira alimoishi kadiri ya Maandiko Matakatifu; mjini Bethlehemu mahali alipozaliwa Kristo Yesu kama utimilifu wa Unabii. Nazareth ni mahali alipokulia Yesu. Hii ni miji miwili yenye uhusiano wa karibu sana na maisha ya Mtakatifu Yosefu. Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo inaelezea kuhusu Ukoo wa Kristo Yesu: 1: 12-16. Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inamwonesha Mtakatifu Yosefu katika historia ya wokovu. Wainjili wote wanamtambua Yosefu kuwa ni Baba Mlishi wa Kristo Yesu, aliyekuja hapa ulimwenguni kutimiza historia ya Agano Jipya na la milele na kwamba, historia ya wokovu inayojenga mahusiano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Kwa Mwinjili Mathayo, historia ya wokovu inapata chimbuko lake kwa Abrahamu, lakini Mwinjili Luka anakwenda mbali zaidi hadi kufikia asili ya mwanadamu yaani Adamu.

Mtakatifu Yosefu ni mwombezi wa Kanisa
Mtakatifu Yosefu ni mwombezi wa Kanisa

Mwinjili Mathayo anawasaidia waamini kumwelewa Mtakatifu Yosefu, katika hali ya ukimya bila makuu, lakini, kiungo muhimu sana katika historia ya wokovu na moyo wa sala. Kimsingi, Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi kuhusu Mtakatifu Yosefu amekwisha kugusia mazingira alimoishi Mtakatifu Yosefu; Wajibu na dhamana yake katika historia ukombozi. Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mtu wa haki na mchumba wake Bikira Maria. Alikuwa ni mtu mkiya sana, aliyejitahidi kujifunza kwa kusikiliza na hivyo kumwachia Neno wa Mungu nafasi ya kuendelea kukua na kukomaa. Huu ni ukimya uliogeuzwa na kumwilishwa katika matendo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu alizaliwa katika mazingira duni na maskini na kwamba, unyenyekevu ndiyo njia inayowapeleka waamini kwa Mungu Baba wa mbinguni. Mtakatifu Yosefu alijisadaka sana ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu. Akalazimika kukimbilia nchini Misri na kukaa huko kama mkimbizi, kashfa inayoendelea kujitokeza hata katika ulimwengu mamboleo. Mtakatifu Yosefu alidhulumiwa, lakini alionesha ujasiri mkubwa kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kwa hakika Mtakatifu Yosefu alikuwa ni Baba Mlishi wa Yesu. Mwinjili Mathayo anamwelezea Mtakatifu Yosefu kwamba, alikuwa mumewe Mariamu aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo. Mt. 1:16. Mwinjili Luka kwa upande wake anakazia kwamba, Kristo Yesu alipelekwa Hekaluni “kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana” Lk 3:23. Kumbe, Wainjili wanakazia dhamana na nafasi ya Mtakatifu Yosefu kama Baba Mlishi wa Mtoto Yesu. Katika Mapokeo ya Kale, jina la mtu lilikuwa ni muhtasari wa mtu. Kumbe, mtu kubadilisha jina, kulimaanisha mabadiliko katika mtu huyo. Tangu mwanzo, Mtakatifu Yosefu alipashwa habari kuhusu Bikira Maria na kuzaliwa kwa Mtoto ambaye ataitwa Yesu. Jina la Yesu maana yake ni Mungu anaokoa. Yeye ndiye atakaye waokoa watu na dhambi zao. Rej. Mt 1: 21.

Mtakatifu Yosefu anaonesha kwamba, kitendo cha kuasili watoto ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa kibaba na kimama. Baba Mtakatifu Francisko amemwelezea Mtakatifu Yosefu kuwa ni Baba Mwenye Huruma, shuhuda amini wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; aliyejitaabiisha katika malezi, makuzi na elimu kwa Mtoto Yesu. Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mtu wa ndoto, nyenzo iliyotumiwa na Mwenyezi Mungu kuwasiliana na waja wake. Kwa njia ya ndoto aliweza kutambulishwa kuhusu Fumbo la Umwilisho, akaokoa maisha ya Mtoto Yesu kwa kukimbilia Misri, kielelezo cha ujasiri wa wazazi unaosimikwa katika sala na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu amechambua kuhusu Mtakatifu Yosefu na Ushirika wa Watakatifu mintarafu Maandiko Matakatifu, Sala na Ibada kwa Mtakatifu Yosefu, ambaye katika historia ya Kanisa amekuwa ni msaada mkubwa kwa watu wa Mungu.

Ushirika wa Watakatifu “Sanctorum communio” ni sehemu ya kiri ya imani ya Kanisa kwa kutambua ushirika wa mema ndani ya Kanisa kunakofanyika kwa njia ya Sakramenti za Kanisa pamoja na kuchota katika hazina ya pamoja. Huu ni ushirika wa mambo matakatifu na ushirika kati ya watakatifu. Ni ushirika wa imani, Sakramenti za Kanisa, Karama katika mchakato wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Ni ushirika wa upendo unaosimikwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Ibada ya Kanisa kwa watakatifu wa Mungu, au visakramenti na hasa zaidi kwa Bikira Maria, ni kwamba, imani ya Kanisa inawaelekeza waamini kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Kristo Yesu unaofumbatwa katika kiungo cha ushirika wa watakatifu. KKK 946-962.

Mtakatifu Yosefu Mlinzi na Mwombezi wa Kanisa
Mtakatifu Yosefu Mlinzi na Mwombezi wa Kanisa

Kimsingi Kanisa ni Jumuiya ya watakatifu na wa dhambi wanaojitahidi kutubu na kumwongokea Mungu. Utakatifu ni matokeo ya huruma na upendo wa Mungu uliofunuliwa katika Kristo Yesu, anayetakatifuza kwa kuwapenda waja wake na hivyo kuwakomboa kutoka katika udhaifu wao wa kibinadamu. Kwa njia ya Kristo Yesu, wote wanafanyika kuwa ni sehemu ya viungo vyake. Kumbe, furaha, mateso na mahangaiko ya mwanajumuiya mmmoja ni mahangaiko na mateso ya Kanisa zima. Ushirika wa watakatifu ni kiungo cha nguvu kiasi kwamba, hata kifo hakiwezi kuwatenganisha. Ushirika wa watakatifu ni muungano wa Kanisa la Mbinguni na Duniani. Kanisa lina Ibada ya pekee kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na kwa Mtakatifu Yosefu. Waamini wanakimbilia sana ulinzi na tunza ya Bikira Maria na ya Mtakatifu Yosefu kwa sababu ya dhamana na utume wao kwa Kristo Yesu. Ushirika wa watakatifu unawawezesha waamini kujisikia kwamba, wanao walinzi na waombezi mbinguni, wanaoweza kuzungumza nao mubashara. Watakatifu ni mifano bora ya maisha na tunu msingi za Kikristo, ndiyo maana waamini wanakimbilia, kuomba ulinzi na maombezi yao.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 16 Februari 2022 amehitimisha Mzunguko wa Katekesi kuhusu Mtakatifu Yosefu aliyetangazwa kuwa ni Msimamizi, Mlinzi na Mwombezi wa Kanisa la Kiulimwengu. Sehemu hii ya Katekesi imenogeshwa na Neno la Mungu kutoka katika Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 2: 13-15: Kukimbilia Misri. “Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu.” Baba Mtakatifu katika Katekesi yake amejielekeza zaidi kuhusu maana ya Msimamizi, Mlinzi na Mwombezi wa Kanisa la Kiulimwengu, umuhimu wa kulipenda, kulilinda na kutemba pamoja na Kanisa licha ya dhambi na utakatifu wa watoto wake.

Mtakatifu Yosefu awasaidie waamini ili waweze kuwa ni watangazaji wa kweli na mashuhuda wa Injili ya Kristo Yesu. Imegota Miaka 150 Tangu Mwenyeheri Pio IX alipomtangaza Mtakatifu Yosefu Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu.” Cheche za Neno la Mungu zinamwonesha Mtakatifu Yosefu kuwa ni mhusika mkuu wa ulinzi na tunza ya Mtoto Yesu pamoja na Mama yake Bikira Maria; amana na utajiri wa imani ya Kanisa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanapomtafakari Bikira Maria katika maisha ya hadhara ya Kristo Yesu wanasema, Bikira Maria aliendelea mbele katika hija ya imani, alihifadhi kwa uaminifu muungano wake na Mwanawe mpendwa Kristo Yesu, mpaka kufika penye Msalaba. Rej. Yn 19: 25, ambapo alisimama imara, kwa mpango wa Mungu; aliteswa kikatili pamoja na Mwanawe wa pekee, na alijiunganisha kwa moyo wake wa kimama na sadaka yake. Rej. Lumen gentium, 58. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni kielelezo cha Kanisa. Kristo Yesu ni Mtu kweli na Mungu kweli. Bikira Maria ni mwanafunzi wa kwanza na Mama wa Kristo Yesu na Mtakatifu Yosefu ni Mlinzi wa Familia Takatifu.

Lipendeni na jitahidini kulilinda Kanisa la Kristo kwa utakatifu wa maisha
Lipendeni na jitahidini kulilinda Kanisa la Kristo kwa utakatifu wa maisha

Hiki ni kielelezo cha chimbuko la wito wa Kikristo yaani: Ulinzi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kujikita katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Ni mwaliko wa kuendelea kulinda akili, moyo na kazi za binadamu. Wito wa Mkristo baada ya kupokea imani, anawajibika kulinda na kudumisha Injili ya uhai, kwake na kwa jirani zake pamoja na kuendeleza maisha na utume wa Kanisa. Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai alizaliwa katika hali na mazingira ya umaskini mkubwa. Kumbe, alihitaji kupewa: ulinzi, hifadhi na usalama, dhamana iliyotekelezwa na Mtakatifu Yosefu, Msimamizi, Mlinzi na Mwombezi wa Kanisa la Kiulimwengu. Mtakatifu Yosefu kwa kuendelea kumlinda Mtoto Yesu na Mama yake Bikira maria, anatoa mwaliko kwa waamini kulipenda Kanisa na kuendelea kumpenda Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo huu unapaswa kumwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji kama Kristo Yesu anavyosema: “Amini, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.” Mt 25: 40.

Maskini na wote wenye kuteseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, wanapaswa kulindwa na kutunzwa kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu, ambaye ni mlinzi wa maskini, wakimbizi na wale wote waliovunjika na kupondeka moyo. Waamini wajifunze kumpenda Kristo Yesu, Bikira Maria, Sakramenti za Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wake. Waamini wajifunze kuwapenda na kuwaheshimu maskini pamoja na Parokia zao, kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu Mlinzi na Mwombezi wa Kanisa la Kiulimwengu. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwa kusema, kwamba, Kanisa linaundwa na watakatifu pamoja na wadhambi wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuonja huruma na upendo wake wa daima. Waamini watambue mapungufu na dhambi zao, wawe tayari kutubu na kumwongokea Mungu, ili kumpenda na kumhudumia katika ukweli na utakatifu wa maisha. Huu ni mwaliko wa kulilinda, kulipenda na kutembea na Kanisa, daima waamini wamwombe Mtakatifu Yosefu, ili waweze kupata ujasiri wa kusimama kidete pamoja na Kanisa. Hasa mahali ambapo kuna kashfa, ili ukweli uweze kufahamika, haki kutendeka na msamaha kutolewa, tayari kuanza tena upya katika hali ya unyenyekevu.

Waamini wamkimbilie Mtakatifu Yosefu kuomba msaada pale ambapo Wakristo wanadhulumiwa na kunyanyaswa, ili aweze kuwaombea nguvu na ujasiri wa kusimama kidete kutangaza na kushuhudia upendo wa Injili; awasaidie kuwa ni alama ya upendo na mshikamano na watu maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wawe mstari wa mbele katika huduma kwa wasiokuwa na ulinzi, watoto yatima na wale wote wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; wagonjwa na wale wanaonyanyasika. Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, kuna umati mkubwa wa watakatifu wa Mungu waliokimbilia ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu katika maisha yao kama: Msimamizi, Mlinzi, Mwombezi na Baba. Mwishoni mwa mzunguko wa Katekesi Kuhusu Mtakatifu Yosefu Msimamizi, Mlinzi na Mwombezi wa Kanisa, Baba Mtakatifu amemwomba, ili aweze kuliombea Kanisa, na hasa kwa wale wote wanaoteseka. Salam Mtakatifu Yosefu, Mlinzi wa Mkombozi na Mume wa Bikira Maria. Kwako Mwenyezi Mungu alikukabidhi Mwanawe; Ndani yako Bikira Maria aliweka imani yake; Pamoja nawe Kristo Yesu alifanyika mwanadamu. Ee MtakatifuYosefu, jioneshe kuwa Baba kwetu pia, na utuongoze katika njia ya uzima. Utuombee neema, rehema na ujasiri, na utulinde na maovu yote. Amina.

Mt Yosefu
16 February 2022, 15:37

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >