Tafuta

Mzunguko Wa Katekesi Waraka Mtume Paulo Kwa Wagalatia: Hitimisho!!

Mzunguko wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko Kuhusu Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia umehitimishwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu ambayo ni mawaidha na baraka ikisema: “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio! Amina

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Novemba 2021 amehitimisha mzunguko wa Katekesi kuhusu Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia. Ni katekesi ya jinsi ambavyo Wakristo wanavyopaswa kuishi kikamilifu imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Utume wa Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma.” Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi ya Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia ametafakari kwa kina kuhusu: Ushuhuda wa Mtume Paulo, Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu, Wito wa Mtume Paulo kutoka kwa Mungu, jinsi alivyolitesa Kanisa na jinsi ambavyo neema ya Mungu ilivyomwezesha kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Maadui wa Mtume Paulo walijikita zaidi katika mapokeo na Torati na kusahau upya ulioletwa na Injili ya Kristo Yesu! Hakuna Injili mpya isipokuwa ile iliyotangazwa na kushuhudiwa na Mitume wa Yesu! Mtume Paulo anapozungumzia kuhusu Sheria anakazia: Sheria ya Musa pamoja na Amri Kumi za Mungu, msingi wa Agano kati ya Mwenyezi Mungu na Waisraeli. Baba Mtakatifu Francisko amekwisha kutafakari pia kuhusu hatari zinazoweza kuibuka kutokana na utekelezaji wa Torati katika misingi ya uhuru kamili, hali inayoweza kupelekea baadhi ya waamini kuwa wanafiki kwa kuogopa kukutana na ukweli!

Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwa kushirikiana Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani  limechapisha Tamko la Pamoja Kuhusu Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki. Hii ni hatua muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Tarehe 3 Januari 2021, Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri kwa pamoja yamefanya kumbukumbu ya miaka 500 tangu Martin Luther alipotengwa rasmi na Kanisa Katoliki. Kwa pamoja, Makanisa haya yanapenda kutangaza nia ya kufanya hija ya upendo na mshikamano kutoka kwenye kinzani kuelekea kwenye umoja kamili wa Wakristo. Tamko la Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki la tarehe 31 Oktoba 1999 lilikuwa na: Utangulizi, Ujumbe wa Biblia juu ya Kuhesabiwa Haki, Mafundisho ya Kuhesabiwa haki kama suala la kiekumene; Ufahamu na maelezo ya pamoja juu ya kuhesabiwa haki. Tamko lilifafanua kuhusu udhaifu wa binadamu, msamaha wa dhambi na kufanyika wenye haki; kuhesabiwa haki kwa njia ya imani na neema. Lilimwangalia aliyehesabiwa haki kama mtu mkosefu; Sheria na Injili; Uhakikisho wa wokovu; Matendo mema ya mtu aliye hesabiwa haki sanjari na umuhimu na lengo la maafikiano yaliyofikiwa. Baba Mtakatifu katika Katekesi yake, mwishoni, ametafakari kuhusu uhuru wa kweli ambao Kristo Yesu amewakirimia waja wake kama zawadi inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, binadamu amekombolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti, mwaliko wa kutambua na kutembea katika ukweli na imani!

Ikumbukwe kwamba, uhuru wa Kikristo ni chachu ya ukombozi ulimwenguni na unapata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Baba Takatifu Francisko ametafakari pia kuhusu Tunda la Roho kama anavyofafanua Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Wagalatia 5: 22-24. “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.” Mtakatifu Paulo Mtume alitangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka ya Kristo yaani: mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Kiini cha wokovu na imani ni mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Anatoa ufafanuzi huu kwa kuwawekea mbele yao Kristo Mfufuka akisema “Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa? Gal 3:1. Mwishoni, Baba Mtakatifu aliwataka waamini kutembea kadiri ya mwanga wa Roho Mtakatifu, kama walivyofanya wafuasi wa kwanza wa Kristo Yesu!

Mzunguko wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko Kuhusu Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia umehitimishwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu ambayo ni mawaidha na baraka ikisema: “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.” Gal 6:9-10.18. Kwa hakika maudhui ya Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia anasema hili ni Neno la Mungu ambalo ni chemchemi isiyonyauka kamwe. Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa amezungumza kama mwinjilishaji, mwanataalimungu mahiri na kama mchungaji. Mtakatifu Inyasi wa Antiokia anasema kuna Mwalimu mmoja tu aliyezungumza na alichosema kilifanyika; lakini mambo aliyofanya katika ukimya kwa hakika yanamstahili Baba. Yeyote aliye na Neno la Yesu anaweza pia kusikiliza ukimya wake.

Mtakatifu Paulo Mtume amefanikiwa kuupatia ukimya wa Kristo Yesu maneno. Amefanikiwa kuwaonesha waamini upya na hatimaye kugundua ufunuo wa Kristo Yesu. Amejitambulisha kuwa ni mwanataalimungu wa kweli, aliyetafakari Fumbo la maisha ya Kristo Yesu na akaweza kuwarithisha wengine kwa kutumia akili yake yenye ubunifu mkubwa. Amefanikiwa kutekeleza dhamana na utume wake wa kichungaji ndani ya Jumuiya ambayo ilikuwa imepoteza dira na mwelekeo wa maisha. Amefanikiwa kutumia mbinu na mikakati mbalimbali kama vile: Kejeli, ukali, upole… amekazia mamlaka yake kama Mtume pamoja na kushuhudia udhaifu katika tabia yake. Moyoni mwake, nguvu ya Roho Mtakatifu imepenya sana ndani mwake: kukutana kwake na Kristo Yesu Mfufuka, kumpelekea kutekwa na hivyo kuleta mageuzi makubwa katika maisha yake, akajitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya kutangaza na kuihubiri Injili. Mtakatifu Paulo Mtume hakuwahi kufikiria Ukristo wenye tabia za uwongo, zisizo na ukimya wala na nguvu, kinyume chake. Alitetea uhuru ulioletwa na Kristo Yesu kwa shauku ambayo hadi sasa inasonga mbele haswa ikiwa kama waamini wanafikiri na kutafakari juu ya mateso na upweke ambao alilazimika kuvumilia. Alikuwa amejiridhisha kwamba, alikuwa ameitiwa wito ambao haungeweza kutekelezwa na wengine.

Mtume Paulo aliwafafanulia waamini wa Galatia na kuwakumbusha kwamba hata wao wameitwa kuwa ni sehemu uhuru huu unaovunjilia mbali mifumo na aina zote za utumwa na hivyo kuwawezesha waaamini kuwa warithi wa ahadi ya kale yaani watoto wa Mungu kwa njia ya Kristo! Mtume Paulo amekazia kuhusu uhuru wa kweli unaosimikwa katika upendo kwa kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Injili ya upendo. Haya ndiyo maisha kadiri ya mwanga wa Roho Mtakatifu anayetimiliza Sheria iliyotolewa na Mwenyezi Mungu kwa Waisraeli na hivyo kuwakinga na uwezo wa kuanguka tena katika utumwa wa dhambi. Kishawishi kikubwa ni kukata tamaa na kutaka kurudi nyuma. Wakristo wakumbuke daima upya wa maisha ulioletwa na Kristo Yesu ambao kimsingi ndio utimilifu wa sheria! Roho Mtakatifu awawezeshe waamini kuishi kwa ukamilifu uhuru wao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hatima ya Katekesi kuhusu Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia inaweza kusaidia kuleta ari na mwamko mpya, unaowasukuma kufuata mara moja njia ya uhuru, ili kutembea katika mwanga wa Roho Mtakatifu. Lakini kwa upande mwingine, waamini wanatambua pia udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, kiasi cha kushindwa kuwa wanyenyekevu kwa kumsikiliza Roho Mtakatifu na kutenda kadiri anavyotaka. Huu ni mwanzo wa kuchoka na hatimaye, ari na mwamko mpya kupotea. Hapa waamini wanajihisi kukatishwa tamaa, kuwa wanyonge, kujisikia kutengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii na hatimaye, kumezwa na malimwengu.

Lakini waamini wanakumbushwa kwamba, imani kwa Kristo Yesu ni sawa kama Yesu yuko katika mashua ya maisha yao. Anasikiliza shutuma, mateso na mahangaiko ya waja wake, yumo, lakini waamini wanaweza kudhani kwamba, Kristo Yesu, “ameuchapa usingizi” na kamwe hajali hata kidogo! Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, waamini wamwamshe Kristo Yesu na kutenda kadiri walivyoambiwa. Ni kwa kumwamsha Yesu kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, hapo ndipo waamini wanaweza kuona mambo kwa jicho la Kristo Yesu, kwa sababu ana uwezo wa kuangalia zaidi ya dhoruba iliyoko mbele yao. Kwa kuuangalia Uso wake mwanana, wanaweza kuwa na matumaini, ambayo kwa kuwa peke yao, ni vigumu sana kuweza kuona mbali. Tena waamini wasichoke katika kutenda mema, daima wajiaminishe chini ya tunza na maongozi ya Roho Mtakatifu anayekuja kuwainua kutoka katika unyonge wao na kuwapatia msaada wanaohitaji. Huu ni mwaliko kwa waamini kujifunza kumwita mara kwa mara Roho Mtakatifu, kwa kutumia sala za mishale, kwa maneno ya kawaida katika mzunguko wa siku. Kuna sala ambazo waamini wamezoea kuzisali yaani: Sala kuu ya Baba Yetu wa Mbinguni, Salam Maria na nyinginezo. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kujenga utamaduni wa kutembea na Biblia, ili waweze kujisomea na kulitafakari Neno la Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha waamini ile Sala ya Kanisa wakati wa Sherehe ya Pentekoste. Sekwensia ya Roho Mtakatifu inabeba utajiri mkubwa wa mahusiano kati ya Roho Mtakatifu na mwamini kama” Baba wa maskini, mwanga wa nyoyo za watu na faraja kwa watu. Sekwensia ya Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya kuzima kiu ya mahitaji ya binadamu! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali sala hii mara kwa mara wanapopata nafasi, ili waweze kutembea katika mwanga wa Roho Mtakatifu, katika uhuru na furaha ya kweli!

Uje Roho Mtakatifu Tuangaze toka Mbingu, Roho zetu kwa mwangao.

Uje Baba wa maskini Uje mtoa wa vipaji, Uje mwanga wa mioyo.

Ee Mfariji mwema sana Ee rafiki mwanana, Ewe Raha mustarehe.

Kwenye kazi u-pumziko kwenye joto Burudisho, Umfutaji wa machozi.

Ewe mwanga wenye heri uwajaze waamini, Neema yako mioyoni.

Bila nguvu yako wewe mwanadamu hana kitu, Kwake yote yana kosa.

Osha machafuko yetu panyeshee pakavu petu, Na kuponya majeraha.

Ulegeze ukaidi pasha moto ubaridi, Nyoosha upotovu wetu.

Wape waamini wako wenye tumaini kwako, Paji zako zote saba.

Wape tuzo ya fadhila wape mwisho bila ila, Wape heri ya milele.

Amina Aleluya Amina Aleluya, Amina Aleluya.

Paulo Mtume
10 November 2021, 15:44

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >