Tafuta

Vatican News

Katekesi Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia: Mtume Kweli

Papa amekazia kuhusu: Ushuhuda wa Mtume Paulo, Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu, Wito wake kutoka kwa Mungu, Jinsi alivyolitesa Kanisa na jinsi ambavyo neema ya Mungu imewezesha kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia ni katekesi ya jinsi ambavyo Wakristo wanavyopaswa kuishi kikamilifu imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kumaliza Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, ameanza Katekesi Kuhusu Waraka Wa Mtume Paulo kwa Wagalatia. Ni Waraka unaowawezesha waamini kumfahamu zaidi Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa na tema msingi katika maisha na utume wake, zinazoremba uzuri wa Injili. Anakazia toba na wongofu wa ndani na jinsi alivyoyasadaka maisha yake kwa ajili ya huduma ya Injili na Kristo Yesu. Anazungumzia mambo msingi katika imani kwa kujikita zaidi kuhusu: uhuru, neema ya kuishi kikamilifu kama Mkristo. Huu ni Waraka unaogusa mambo tete hata katika nyakati hizi, kana kwamba, ni Waraka ulioandikwa kwa ajili ya waamini katika mapambazuko ya Millenia na Tatu ya Ukristo. Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anatoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema, uliomwezesha kutembelea Jumuiya ya Wagalatia walau mara mbili, kwakati wa safari zake za kimisionari. Kuna mambo mengi ambayo hayana majibu ya moja kwa moja. Paulo alikuwa ni Mtume kweli kweli!

Anuani, msingi na muhtasari wa Injili ya Paulo unabubujika kutoka katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu: “Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu), na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia; Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu… Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba nililitesa Kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu… Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake…” Gal 1:1.13.15-16.

Hii ni sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyonogesha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 30 Juni 2021 kwenye Uwanja wa Mtakatifu Damas mjini Vatican. Baba Mtakatifu amekazia kuhusu: Ushuhuda wa Mtume Paulo, Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu, Wito wake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Jinsi alivyolitesa Kanisa la Mungu na jinsi ambavyo neema ya Mungu imewezesha kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia ni katekesi ya jinsi ambavyo Wakristo wanavyopaswa kuishi kikamilifu imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika Waraka huu, anawakumbusha Wagalatia mateso aliyokumbana nayo, upendo wake kwao na matumaini yake kwamba, Wagalatia watafuata njia ya kweli ili kudumisha umoja, ukweli wa Kiinjili na neema ya imani. Huu ni wasi wasi wa Mtume Paulo, muasisi wa jumuiya ya imani anayekazia umuhimu wa kujikita katika upya wa Injili waliyoipokea kutoka kwake, ili kujenga msingi wa utambulisho wao!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mtume Paulo alikuwa na ufahamu mkubwa wa Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu. Katika mawazo yake, anapaa zaidi na kuwaonesha waamini jinsi ya kufikiri na kutenda, wanapokabiliana na matatizo na changamoto za mipasuko ya kiimani ndani ya jumuiya. Mwishoni mwa Waraka huu, anazungumzia kuhusu Sheria na Msalaba wa Kristo na wale wote ambao wamekuwa ni viumbe wapya kwani wanachukua mwilini mwao chapa ya Kristo Yesu! Kutahiriwa kadiri ya mila na desturi za Kiyahudi lilikuwa ni jambo muhimu na utambulisho wao. Ni katika muktadha huu, Paulo Mtume aliamua kuzama zaidi ili kuubainisha ukweli wa Injili na uhuru wa Wakristo kama sehemu muhimu sana ya utambulisho wao. Mtume Paulo katika ufafanuzi wake, hakubaki juu juu tu, bali aliamua kuzama ndani zaidi ili hatimaye, kupata suluhisho la kudumu.

Mtume Paulo anasema: “Maana, sasa Je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumwa wa Kristo.” Gal 1:10. Mtume Paulo anasikia ndani mwake umuhimu wa kuwakumbusha Wagalatia kwamba, kuhusu wito wake kwamba, unapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, ni mtume kweli kweli. Anawasilimua jinsi alivyotubu na kumwongokea Mungu baada ya kukutana mubashara na Kristo Yesu Mfufuka alipokuwa njiani kuelekea Dameski. Rej. Mdo 9:1-9. Mtume Paulo anawadadavulia kuhusu historia ya maisha yake ya hapo awali akisema: “Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake”. Gal 1: 13-14.

Anakazia kuhusu kufuata mapokeo ya baba zake na kwamba, alisimamia sheria kwa nguvu zote. Anatambua kwamba, aliliudhi na kuliharibu Kanisa, lakini neema na huruma ya Mungu imemletea wongofu ambao sasa unafahamika na wengi. Mtume Paulo anasema, “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1:22-23. Hiki ni kielelezo cha toba na wongofu wa ndani, kiini na ukweli wa historia ya wito wake, sasa anatangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, huku akiwa ni mtu huru kabisa! Anakiri dhambi zake kutoka katika sakafu ya moyo wake na hivyo kujaliwa uhuru wa ndani kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Historia hii inaonesha mshangao mkubwa wa Paulo ambaye sasa ni Mtume wa Kristo Yesu! Lakini Mwenyezi Mungu, alimtenga tangu tumboni mwa mama yake, akamwita kwa neema yake, alipoona vema akamdhihirisha Mwanawe mpendwa Kristo Yesu ndani yake, ili awatangazie na kuwashuhudia Mataifa Habari Njema ya Wokovu.

Mwenyezi Mungu anasema Baba Mtakatifu Francisko anamwita mtu kadiri ya hali na mazingira yake ambayo wakati mwingine, huwashangaza wanadamu. Hakuna jambo linalotendeka kwa bahati mbaya, bali kila kitu ni sehemu ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, changamoto kwa waamini ni kutekeleza mapenzi ya Mungu na kutekeleza utume ambao Mwenyezi Mungu amemwandalia kila mtu. Kwa njia ya neema na baraka zake, Mwenyezi Mungu anawaita waja wake, kumbe, ni vyema ikiwa kama watatambua neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao, kiasi cha kuwaletea mabadiliko makubwa katika maisha, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kikristo kwa watu wa Mataifa. Neema ya Mungu ilete toba na wongofu wa ndani kwa wadhambi; ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu, ili hatimaye, waweze kuona njia mpya ambao Mwenyezi Mungu amewaandalia waja wake!

Mtume Paulo

 

 

30 June 2021, 16:12

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >