Tafuta

Papa Francisko akumbuka watu wa Ethiopia na Libia Papa Francisko akumbuka watu wa Ethiopia na Libia 

Francisko aomba amani kwa ajili ya Ethiopia na Libia

Bada ya Sala ya Malaika wa Bwana,Papa Francisko mawazo yake ni kwa kile kinachoendelea nchini Ethiopia na kushauri mazungumzo ili kuzuia vishawishi vya mapigano ya kisilaha.Kwa ajili ya Libia ili mateso ya watu yaweze kuisha na kusitisha moto huo wa kidumu.Amekumbusha waathiriwa wa dhoruba kali huko Amerika ya Kati na kusali kwa ajili ya marehemu na majeruhi.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Papa Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 8 Novemba 2020, kwa mahujaji na waamini waliokusanyika katika uwanja wa Mtakatifu Petro, ameonesha masikitiko na wasiwasi wake kwa kile kinachoendelea nchini Ethiopia. Anawaomba wasukumize mbali vishawishi vya mapigano ya kisilaha na kuwaalika wote kusali kwa ajili ya kuheshimiana kidugu na kuwa na mazungumzo  ili kutafuta amani.

Amani nchini Libia

Wazo jingine la Papa Francisko limeelekezwa hata  juu ya amani nchini Libia. Amekumbusha juu ya Mkutano ambao umeanza Jumapili, jijini Tunisi, mahali ambapo linafanyika Jukwa la mazungumzo ya kisiasa kuhusu Libia na ambayo yanahusu sehemu zote mbili. “Kutokana na umuhimu wa tukio hilo, "ninatumaini kwa dhati kwamba katika wakati huu nyeti suluhisho la mateso marefu ya watu wa Libia lipatikane na kwamba makubaliano ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano ya kudumu yataheshimiwa na kutekelezwa. Tuwaombee wajumbe wa mkutano huo, kwa ajili ya amani na utulivu wa nchi ya Libia”, Papa Francisko amewasihi .

Dhoruba Amerika ya Kati

Katika sala ya Papa Francisko pia imeelekeza kwa watu wa Amerika ya Kati ambao wamekumbwa na dhoruba kali iitwayo Eta, ambayo kwa siku za hivi karibuni imesababisha vifo na madhara makubwa katika eneo ambalo tayari linateseka sana kwa sababu ya janga la corona. Eta, sasa imepungua ukali wake wa kitropiki, lakini imesababisha vifo vya watu 200 na wengine kupotea na waathiriwa walio wengi zaidi wameorodheshwa nchini Guatemala. “Bwana apokee roho za marehemu na awape nguvu familia zao na kuwasaidia wale ambao wamejaribiwa zaidi kama vile hata wale ambao wanaendelea kutoa msaada wa kuwasaidia”, Papa amesema.

Kijana Mwenyeheri mpya

Hata hivyo Papa Francisko awali ya yote amekumbuka tukio la kutangazwa kwa mwenye heri, tukio ambalo limefanyika huko Barcellona nchini Uhispania, Jumamosi tarehe 7 Novemba 2020 kwa  kijana Juan Roig y Diggle, mlei na mfiadini aliyeuawa akiwa na umri wa miaka 19 tu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. “Alikuwa ni shuhuda wa Kristo katika mazingira ya kazi na akabaki mwaminifu hadi zawadi ya mwisho ya kutoa maisha. Mfano wake, uweze kuigwa na wote hasa vijana  ile shauku ya kuishi kwa ukamilifu wa wito Krikristo” Papa ameshauri.

Siku ya kumshukuru Mungu nchini Italia

Papa Francisko amekumbusha hata Siku ya Kumshukuru Mungu nchini Italia  iliyofanyika Jumapili 8 Novemba ambayo mwaka huu imeongozwa na mada ya maji. "Maji ni muhimu kwa kilimo; ni muhimu pia kwa maisha! Niko karibu kwa maombi na upendo kwa ulimwengu wa vijijini, hasa kwa wakulima wadogo. Kazi yao ni muhimu zaidi kuliko wakati huu wowote wa mgogoro. Ninashiriki na maaskofu wa Italia ambao wanashauri kulinda maji kama wema wa pamoja na ambao lazima kuheshimu matumizi yake ya lazima kwa ajili ya mstakabali wa ulimwengu”, amesisitiza Papa Francisko.

08 November 2020, 15:22