Marekani:Siku ya maombi iliyoandaliwa na maaskofu katika maadhimisho ya miaka 75 ya bomu la atomiki
Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican
Katika fursa ya maadhimisho ya miaka 75 tangu kulipuka mabomu ya nyuklia ya Hiroshima na Nagasaki, mnamo tarehe 6 na 9 Agosti, maaskofu wa Marekani wanawaalika Wakatoliki wote na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki, Jumapili tarehe 9 Agosti 2020, katika siku maalum ya maombi, tafakari na kujikita katika kuchukua hatua dhidi ya kusitishwa kwa silaha za kinyuklia. Siku hiyo itaadhimishwa sambamba na Siku kumi za Maombi kwa ajili ya Amani. Ni tukio la kila mwaka lilioanzishwa na Kanisa huko Japan tangu mwezi 1981. Karne ya XXI inaendelea kushuhudia mzozo wa kijiografia na watendaji wa serikali na wasio wa serikali wakitumia silaha za kisasa na mmomonyoko wa mfumo wa kisheria wa kimataifa juu ya udhibiti wa silaha, wanaandika katika barua kutoka Tume ya Kimataifa ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu wa Marekani (Usccb).
Wito wa Papa dhidi ya utumiaji na silaha za nyuklia
Maaskofu wa Marekani kwa mara nyingine tena wanasisitiza wito wao kuhusu shinikizo dhidi ya kuongezeka kwa nyuklia, kwa maneno mazito yaliyosemwa na Papa Francisko huko Nagasaki na Hiroshima wakati wa ziara yake ya kitume ya Japan kunako tarehe 24 Novemba 2019. Nafasi hiyo iliwekwa wazi tena mwezi Februari na Tume hiyo hiyo ya Baraza la Maaskofu wa Marekani ambayo ilizindua tena wito wa Papa dhidi ya utumiaji na silaha za nyuklia. Jukumu hili la uwajibika, walikuwa wamesisitiza Tume ya Haki na Amani, kuwa inatoa uzito wa dhamiri kwa mataifa ambayo yana silaha za atomiki, kama vile Marekani ambayo lazima zichukue hatua ya kupunguza,na mataifa yale ambayo hayana na ambayo lazima yaachane na jaribio la kutaka kuipata ili kifungu VI cha Mkataba usio na Nyuklia uwe ndiyo chombo bora cha kuondoa kabisa.
Miaka kumbukizi la miaka 75 ya kulipuka kwa bomu la atomiki
Japan inajiandaa kukumbuka miaka 75 tangu bomu la kwanza la kinyuklia kudondoshwa Hiroshima, kisa kilichoilazimisha Japan kusalimu amri na kumalizika vita vikuu vya pili vya Dunia. Katika Hospitali nchini Japan bado mpaka leo hii zinawatibu maelfu ya wahanga walionusurika na shambulio la bomu hilo la nyuklia. Tarehe 9 Agosti bomu jengine la nyuklia huko lilidondoshwa karibu na mji wa bandari wa Nagasaki, watu 70 elfu waliuawa. Mashambulio hayo mawili ya mabomu ya nyuklia ndiyo ilikuwa chanzo cha kusalim amri Japan tarehe 15 Agosti 1945 na kumalizika vita vikuu vya pili vya dunia.
Papa aliomba kuacha kabisa sihala za atomiki
Papa Francisko alipotembelea nchi hiyo aliitaka dunia kuachana kabisa na silaha za atomiki wakati wa hotuba yake mjini Nagasaki Japan, mji ulioshambuliwa kwa mabomu ya nyuklia mwishoni mwa vita vikuu vya pili vya dunia ambayo haitasahulika kamwe! Katika hotuba yake aidha Papa Francisko akiwa katika eneo la uwanja wa kumbukumbu ya mabomu ya atomiki mjini Nagasaki huku mvua ikinyesha alisema: “Eneo hili linatufanya kutambua maumivu na maovu ambayo sisi binadamu tunaweza kufanyiana”. Kabla ya hotuba yake, Papa Francisko alitoa heshima zake kwa wahanga wa shambulio la Marekani la bomu la kinyuklia mwaka 1945 katika mji huo wa kusini magharibi nchini Japan, na kuwauwa watu wapatao 74,000, ikiwa ni pamoja na maelfu ya wakatoliki.
Kuwa na silaha za maangamzi siyo suluhisho
Akiendelea na hotuba yake alisema: “Hapa katika mji huu ambao ulishuhudia kwa hakika tukio la maafa ya kibinadamu na mazingira kutokana na shambulio la nyuklia, juhudi zetu kuzungumzia dhidi ya mashindano ya silaha hazitatosha. Moja kati ya kile ambacho moyo wa binadamu unachopenda zaidi ni usalama, amani na uthabiti. Kuwa na silaha za nyuklia na silaha nyingine za maangamizi siyo jibu la hisia hizi katika moyo wa binadamu unavyopenda, kiukweli kila mara binadamu anajaribu kuzuwia hilo”. Amani na uthabiti wa kimataifa hayalingani na majaribio ya kujenga juu ya hofu ya uharibifu wa pamoja ama kitisho cha maangamizi ya jumla alisema Papa Francisko. “Nikiwa naamini kuwa dunia bila silaha za kinyuklia inawezekana na ni muhimu, nawataka viongozi wa kisiasa kutosahau kuwa silaha hizi haziwezi kutulinda kutokana na kitisho cha hivi sasa katika usalama wa kitaifa na kimataifa. Tunahitaji kutafakari athari ya maafa ya uwepo wake, hususan kutokana na mtazamo wa kiutu na mazingira, za na kukataa kuongeza hofu ya kimazingira, kutokuaminiana na uhasama unaochochewa na nadharia za nyuklia.”
Bado wanahakati wa kupinga silaha za kinyuklia wanaendelea
Papa alifanya mkutano Hiroshima kwa ajili ya amani pia akakutana na wahanga wa tetemeko la ardhi la mwaka 2011, tsunami na maafa ya nyuklia kaskazini mashariki mwa Japan. Ziara yake ilikuwa ya kwanza kufanywa na Papa nchini Japan baada ya muda wa miaka 38. Mwaka 1981, Papa John Paulo II alikwenda Hiroshima, Nagasaki na Tokyo. Papa Francisko alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutia saini na kuidhinisha mkataba wa kuzuwia silaha za kinyuklia, ambao uliidhinishwa na mataifa 122 mwezi Julai 2017. Mkataba huo hata hivyo bado haujaanza kutumika kwa kuwa haujaidhinishwa na mataifa 50 ambayo yanatakiwa kutia saini. Wanaharakati wa kupinga silaha za kinyuklia bado wanaendelea kuitaka Japan, ambayo ni nchi pekee iliyoathirika na mashambulizi ya silaha za atomiki, kutia saini na kuidhinisha mkataba huo haraka iwezekanavyo. Shambulio la mji wa Nagasaki tarehe 9 Agosti 1945, lilikuja siku tatu baada ya shambulio la kwanza la bomu la atomiki lililodondoshwa na ndege ya mashambulizi ya B-29 ya Marekani na kuripuliwa katika mji wa Hiroshima na kusababisha watu 140,000 kuuwawa.