Tafuta

Vatican News
Kusafisha mikono kabla ya kuingia Kanisani nchini Kenya Kusafisha mikono kabla ya kuingia Kanisani nchini Kenya  (AFP or licensors)

KENYA #coronavirus:Baraza la maaskofu waomba uwazi kuhusu mfuko wa fedha kwa ajili ya covid-19!

Katika fursa ya sikukuu ya Mchungaji mwema sambamba ya Siku ya 57 ya Kuombea Miito ya Kanisa,Jumapili Mei 3,Baraza la Maaskofu nchini Kenya wameomba uwazi katika kuratibu mfuko wa fedha kwa ajili ya mapambano ya virusi vya corona au covid-19.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican News

Kwa mujibu wa taarifa katoliki za Afrika,inabainisha kwamba katika fursa ya Sikukuu ya Mchungaji Mwema,sambamba na Siku ya Kuombea Miito, ya Kanisa, Dominika tarehe 3 Mei 2020, Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Kenya (KCCB) mara baada ya Misa iliyokuwa inatangazwa moja kwa moja na runinga, Askofu John Oballa, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Kenya (KCCB), kwa niaba ya Baraza zima wakati wa kusoma taarifa hiyo wameonesha wazi wazi juu ya wasiwasi  katika kuratibu matumizi vibaya ya mfuko uliowekwa kwa ajili ya kupambana na janga la virusi vya corona au covi-19.

Maaskofu wanasema, "Kama Kanisa, tunafahamu hatua mbali mbali zilizochukuliwa na serikali ili kudhibiti kuenea kwa janga hili katika nchi yetu. Walakini, tuna wasiwasi juu ya habari kwamba fedha kadhaa zilizokusudiwa kwa ugonjwa huo zimetumika vibaya”. Askofu Oballa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume kwa ajili ya Haki na Amani  ya (kccb),ameiomba serikali kuhakikisha kuwa mfuko wa fedha unatumika kupambana na janga la virusi na ili kuweza kurudisha nchi katika hali ya kawaida.

Aidha askofu Oballa katika kusoma taarifa hiyo, kwa niaba ya Baraza zima la Maaskofu, ameshauri serikali ya Kenya kusaidia miundo ya majengo ya kidini ambayo sehemu kubwa inatumika kuhudumia idadi ya watu katika maeneo ambayo ni magumu kuyafikia. Hiyo ikiwa ni pamoja nao katika usambazaji wa vifaa vya kinga binafsi na kuwaruhusu wafanyakazi wao wa afya kupata matibabu ya Covid-19 ya serikali na vifaa vya karantini.

Hatimaye Baraza la Maaskofu wametoa mwaaliko kwa Wakenya  wote kuungana pamoja katika sala na kuwa na mshikamano na wale walio mstari wa mbele katika kupambana na virusi vya corona na wanajitoa maisha ili kuokoa maisha ya wengine.

05 May 2020, 17:42