Nigeria#Coronavirus:Makanisa yamefungwa kipindi hiki lakini siyo mioyoni mwetu!
Na Sr. Angela Rezaula – Vatican
Katika Misa ya Dominika ya Huruma ya Mungu Jumapili 19 Aprili 2020 kwa upande wa Kanisa Kuu la Abuja nchini Nigeria iliyotangazwa moja kwa moja kwa waamini kupitia ukurasa wao wa Facebook, Askofu Mkuu Ignatius Kaigama, wa Jimbo Kuu hilo alisema kuwa “Virusi vya corona vimesababaisha kufungwa makanisa yetu lakini mioyo yetu lazima ibaki imefunguliwa kwa imani na matumaini katika Ufufuko, Huruma ya Mungu na katika upendo wa mmoja na mwingine”.
Askofu Mkuu wa Abuja aliwaalika waamini kubaki wameungana kiroho hata kama wametengana kimwili. “Kanisa siyo mihimili ya majengo tu" lakini pia watambue kuwa wao ni “hekalu la roho Mtakatifu”. Askofu Mkuu kwa kutazama kupindi hiki cha vizuizi katika dharura hii ya kiafya amethibitisha kuwa havikuweza kuwazuia kuadhimisha kwa furaha hata Pasaka hii maalum. Licha ya usambaaji wa virusi vya corona na kupigisha magoti ulimwengu mzima, “havikuwa na uwezo wa kugandisha au kuzika imani yetu na licha ya umbali uliopo wa kijamii haukuweza kuondoa msimamo wa Kanisa na kuondoa ule upendo kwa wengine kama ilivyokuwa ikijitokeza kwa wakristo wa kwanza”.
Askofu Mkuu Kaigama vile vile amebainisha ni kwa jinsi gani kipindi hiki licha ya kuwa na ugumu lakini imekuwa kama fursa ya kibinadamu. Hii ina maana kwamba kipindi hiki cha pekee kimetoa fursa kwa wakristo kuanza kwa upya namna ya kupenda na kusaidiana mmoja na mwingine; kukuza na kutunza ule ukimya wakati wa tafakari na kuwa na maisha ya kina zaidi ndani ya mioyo huku wakijisomea zaidi Neno la Mungu na kusali kwa kina. Kwa maneno mengine Askofu Mkuu anabainisha ni kama “kuonyesha ile sababu ya imani yetu kwa ngazi iliyo ya juu zaidi”.
Kwa kufafanua anabainisha kuwa ni kwamba suala la kuabudu sio la kijuu juu, lakini ni matendo hai, ya dhati ambayo “Yesu alitufundisha juu ya upendo, amani, huduma na msamaha”. Kwa maana hiyo ndipo alitoa wito wa kuwa na mshikamano hasa kwa wale wanao hitaji zaidi katika nyakati hizi ngumu. Hasa akiwaomba wanajimbo kuu kusaidia wanageria wengi ambao katika kipindi hiki wamebaki bila msaada kutokana na janga la corona.