UN:Majira ya baridi kali zaidi kwa mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao
Na Angella rwezaula – Vatican.
Sio tu mabomu ambayo huua katika nchi zilizo kwenye vita, lakini pia baridi. Inatokea katika Ukanda wa Gaza ambapo watoto kadhaa wachanga wamekufa kutokana na baridi pamoja na utapiamlo na ukosefu wa madawa. Hali ambayo pia huathiri maeneo mengine ya dunia: msimu wa baridi hunaleta hatari kubwa kwa maisha ya mamilioni ya wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao. Kwa wengi wao, hii inabadilika kuwa moja ya msimu wa baridi mbaya zaidi kuwahi kutokea. Mamia ya maelfu ya familia hawawezi kujikinga na halijoto ya baridi, hawana nguo na blanketi wakati wa baridi, na hawana hata rasilimali za kutosha kulipa kodi ya nyumba au kununua chakula na dawa.
Msaada wa msimu wa baridi
Kutokana na muktadha huo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi linachangisha fedha kwa haraka ili kutoa msaada wa haraka wa kuokoa maisha kwa wakimbizi na watu waliohamishwa makazi yao, kwa kampeni inayoitwa ‘Another Winter Away from Home’ yaani Msimu mwingine wa baridi nje ya nyumbani. Na Nchi nane zinahusika kuanzia na :Afghanistan, Pakistan, Misri, Syria, Jordan, Lebanon, Ukraine na Moldova. "Idadi ya watu wanaokimbia vita, ghasia na mateso duniani imefikia rekodi mpya: tunazungumzia zaidi ya wanaume, wanawake na watoto milioni 120, idadi ambayo imeongezeka karibu mara mbili katika miaka 10 iliyopita." Aliyezungumza hayo ni Bwana Filippo Ungaro, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (Unhacr-Italia. Wengi wa watu hao hawana makao, nyumba inayoweza kuwapa joto, au mahitaji ya kimsingi.
Ugumu wa waliohamishwa
Sehemu kubwa ya watu hawa ni wanawake na watoto, "watu walio hatarini sana ambao wanapaswa kuwakilisha mustakabali wa watoto wao na, badala yake, kubaki wamenaswa katika mzunguko wa umaskini ambao unajirudia kila mara." Mwaka jana(2024), wakala huo ulijibu dharura 43 za wakimbizi katika nchi 29, huku kukiwa na mzozo wa kimataifa ambao, kulingana na Ungaro, unasababisha “kutokuaminiana kwa sheria na ushirikiano wa kimataifa. Ni muhimu kupata mzizi wa matatizo, lazima tujaribu kujibu kwa kutumia mbinu na utamaduni wa amani, kujaribu kupunguza mateso ya raia.”
Maeneo ya Mpaka
Na zaidi ya hayo sio nchi zilizoathiriwa moja kwa moja na migogoro tu, lakini pia nchi jirani zinapitia matatizo haya kwa ndani. Tangu kuanza kwa hali hiyo nchini Lebanon, watu 557,000 wamevuka mpaka na kuingia Syria, wakiwa wamechoka na katika mazingira magumu. Familia za Syria zinazokaribisha familia zinazokimbia ghasia majumbani mwao zinakabiliwa zenyewe na umaskini na njaa. Nchini Afghanistan, raia wanateseka kutokana na kuzorota kwa uchumi kwa kiasi kikubwa na matokeo ya miongo kadhaa ya migogoro na majanga ya asili ambayo yanaonekana katika nchi jirani ya Pakistan. Baada ya kupita hatua ya kusikitisha ya siku elfu moja za vita nchini Ukrainia, mamilioni ya wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao wamekaribishwa nchini Moldova. "Tunapozungumza kuhusu matukio ya uhamaji lazima kila wakati tuzingatie mfumo wa kimataifa wa hali hiyo. Nchi nyingi zinazohifadhi wakimbizi nazo ziko katika hali ngumu. Uangalifu zaidi wa kisiasa na maslahi makubwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa yanahitajika."