Tafuta

 Askofu  Mattew Hassan Kukah, wa Jimbo la Sokoto (Nigeria) Askofu Mattew Hassan Kukah, wa Jimbo la Sokoto (Nigeria) 

Nigeria:Tuendeleze kilimo ili kuwapa watu wetu hadhi,asema Askofu wa Sokoto

Katika ujumbe wa Pasaka wa Askofu Kukah wa Jimbo Katoliki la Sokoto nchini Nigeria akitazama hali halisi ya nchi aliorodhesha kile alichosema ni maovu ambayo taifa la Nigeria lazima likabiliane nayo ili kuponya kuwanzia na “upungufu wa chakula, ufisadi,upendeleo na ukosefu wa usalama.”

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Hakuna mtu anayepaswa kupanga foleni ili kupata usaidizi wakati hatuko vitani,” alisema hayo Askofu Matthew Hassan Kukah, wa Jimbo katoliki la  Sokoto nchini Nigeria , katika ujumbe wake wa Pasaka, alioupatia mada ya “Ni wakati wa kupona.” Kwa mujibu wa Habari za Kimisionari FIDES, zinabainisha kuwa katika  ujumbe wake, Askofu Kukah aliorodhesha anachosema ni maovu ambayo taifa la Nigeria lazima likabiliane nayo ili kuponya kuanzia na “upungufu wa chakula, ufisadi, upendeleo na ukosefu wa usalama.” Kuhusu hoja ya kwanza, askofu wa Sokoto alisema: “Tuwarudishe watu wetu kwenye mashamba yao na tuandae mpango wa kimataifa wa kilimo ili kuirejesha nchi yetu kwenye njia ya heshima na hadhi ya binadamu.”

Ombi la Askofu Kukah lilifafanuliwa na ukweli kwamba uwezo mkubwa wa kilimo wa Nigeria hautumiwi ipasavyo kiasi kwamba kulingana na Mpango wa shirika la Chakula Duniani (WFP) “Wanigeria milioni 26.5 watakabiliwa na njaa kali katika msimu wa mavuno  kati ya Juni na Agosti 2024. Hili ni ongezeko la kushangaza ikilinganishwa na watu milioni 18.6 ambao wanalikabiliwa na uhaba wa chakula mwishoni mwa  mwaka 2023,” WFP ilisisitiza. Ukosefu wa usalama unaosababishwa na vikundi vya kijihadi na magenge ya wahalifu katika eneo la kaskazini-mashariki umewalazimu mamilioni ya watu kuacha mashamba walimokuwa wakiendesha kilimo cha kujikimu. Zaidi ya hayo ni mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ukame na mafuriko. Hata hivyo, tatizo la msingi la uwekezaji duni katika sekta ya kilimo katika mfumo wa kiuchumi unaotawaliwa na uuzaji wa mafuta nje ya nchi bado. Mapato ya mafuta yanahimiza uagizaji wa chakula kutoka nje ya nchi zaidi ya uwekezaji katika sekta ya kilimo ya ndani.

Kutokana na hali hiyo, Nigeria, ambayo ina hekta milioni 70.8 za ardhi ya kilimo, inayolimwa kwa mahindi, mihogo, viazi vitamu, mtama na mpunga, haiwezi kujitegemea kulisha wakazi wake milioni 220. Uzalishaji wa mpunga nchini Nigeria ulipanda kutoka tani milioni 3.7 mwaka 2017 hadi tani milioni 4.0 mwaka 2018. Pamoja na hayo, ni asilimia 57 tu ya tani milioni 6.7 za mchele zinazotumiwa kila mwaka nchini Nigeria zinazozalishwa nchini, na hivyo kusababisha upungufu wa karibu tani milioni 3, ambazo huingizwa nchini au kutoroshwa kinyume cha sheria. Nigeria inaagiza chakula cha dola bilioni 10 kila mwaka kutoka Umoja wa Ulaya, Asia, Marekani, Amerika Kusini na Afrika Kusini. Kuna mipango ya kuboresha kilimo cha Nigeria ambacho kinawakilisha karibu 23% ya pato la taifa na kuajiri karibu 70% ya wafanyakazi. Mipango hiyo ni pamoja na kupitishwa kwa mbinu za kisasa za kilimo kwa kutumia mbegu bora. Mwisho, hata hivyo, huzalishwa na makampuni kadhaa duniani kote ambayo yanatumia kikamilifu  kimataifa juu ya uzalishaji wa chakula.

Askofu wa Sokoto nchini Nigeria na wasi wasi wa watu wake
06 April 2024, 15:23