Tafuta

Mamia na makumi elfu huko DRC wakikimbia makazi yao. Mamia na makumi elfu huko DRC wakikimbia makazi yao.  (AFP or licensors)

DRC/Save the Children:karibia watoto78,000 wamekimbia na familia

Save the Children,inaripoti kuwa takriban watoto 78,000 wameyakimbia makazi yao na familia kuharibiwa huku ghasia zikiongezeka huko DRC.Shirika linataka mifumo iliyopangwa na thabiti,kufunguliwa mashtaka wanaohusika na unyanyasaji,kuheshimu sheria za kimataifa na haki za binadamu ili kuhakikisha ulinzi wa watoto.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Tangu tarehe 2 Februari 2024 huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imeanza tena mapigano kati ya Wanajeshi (FARDC) na M23, kundi lisilo la kiserikali lenye silaha, ambalo limewalazimu takriban watu 150,000, zaidi ya nusu ya watoto (kariba 78,000) kutelekeza nyumba zao. Wazazi waliripoti kuwa watoto wengi wametenganishwa na familia zao kutokana na ukatili huo, lakini idadi ya watoto waliopotea bado haijajulikana. Familia, wakati huo huo, zinatafuta hifadhi katika kambi za wakimbizi, makanisani, shuleni na kwa familia zinazowapokea. Kufikia sasa, maelfu ya watu wanasafiri kwenda Goma, mji mkuu wa mkoa, kutafuta usalama. Matumizi ya mizinga, ndege zisizo na rubani na vilipuzi katika eneo la mashariki mwa DRC yanaua na kujeruhi raia na kuharibu au karibu kuharibu miundombinu muhimu.

Watu wengi wanakimbia ghasia Nchini DRC na wanaoteseka ni watoto
Watu wengi wanakimbia ghasia Nchini DRC na wanaoteseka ni watoto

Hii ndiyo picha mbaya ya nchi ambayo  Shirika la Saidia Watoto (Save the Children) limeripoti tarehe 9 Februari 2024 ambalo ni shirika la kimataifa ambalo limekuwa likipambania  kwa zaidi ya miaka 100 kuokoa wavulana na wasichana katika hatari na kuwahakikishia siku zijazo. Kulingana na vyanzo vya habari vya ndani, watu 19 waliuawa na wengine 27 kujeruhiwa katika ghasia hizo, wakiwemo wasichana watatu. Mnamo tarehe 7 Februari 2024  soko lilirushiwa  na risasi zilizoanguka katika ua wa shule na karibu na hospitali. Shule zote katika eneo hilo zimefungwa kwa sasa.

DRC kwa muda mrefu imekuwa ikishuhudia migogoro ya mzunguko, machafuko na wimbi la wakimbizi. Leo, hii zaidi ya watu milioni 25 wanahitaji sana misaada ya kibinadamu ili kuishi na zaidi ya milioni saba wameyahama makazi yao. Wimbi la sasa la ghasia linakuja baada ya mwaka wenye msukosuko na milipuko mikali ya migogoro iliyozuka mnamo mwaka wa 2023, wakati mapigano yaliyoenea mashariki mwa nchi hiyo kati ya makundi mbalimbali yalisababisha zaidi ya watu milioni 1 kuyahama makazi yao, wakiwemo watoto wasiopungua 500,000. Kulingana na  Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), mwishoni mwa 2023, Kivu Kaskazini pekee ilikuwa na zaidi ya wakimbizi wa ndani milioni 2.4.

Watoto wakiwa migongoni na mikononi kutembea wakikimbia vita
Watoto wakiwa migongoni na mikononi kutembea wakikimbia vita

Watoto huko Mashariki mwa DRC wanaishi  na jinamizi lingine. Ghasia za ghafla zilizozuka mwishoni mwa juma ziliwatenganisha watoto na familia zao na kuwaondoa kwa nguvu kutoka nyumba zao. Familia sasa zinatafuta kimbilio shuleni, makanisani na hospitalini, zikitumaini kutokumbwa na mzozo huo. Wakati huo huo, familia za wenyeji, ambazo tayari zimekonda, zinaongezeka katika mgogoro huu unaozidi kuwakaribisha watu zaidi,” alisema Greg Ramm, Mkurugenzi wa Save the Children nchini DRC.

Shirika la Save the Children linatoa wito wa kuwepo kwa mifumo iliyopangwa zaidi na thabiti ili wahusika wa uhalifu dhidi ya watoto wachukuliwe hatua na kuwataka wale wote wanaohusika na ukatili huo kuheshimu sheria za kimataifa na haki za binadamu ili kuhakikisha ulinzi wa watoto wadogo zaidi. Hivi sasa, watoto na familia zao wanaona ni vigumu kupata huduma muhimu kwa ajili ya ulinzi na maisha yao. Njia pekee salama ya kufikia idadi ya watu waliohamishwa ni kwa njia ya bahari.

Watu wanateseka sana nchini DRC
Watu wanateseka sana nchini DRC

Shirika la Save the Children limekuwa likifanya kazi nchini DRC tangu mwaka 1994 ili kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu yanayohusishwa na kuwasili kwa wakimbizi na kuhama kwa watu kutokana na migogoro ya silaha katika majimbo ya mashariki. Aidha Shirika hilo limeongeza mwitikio wake wa kibinadamu ili kusaidia mifumo iliyopo ya utunzaji, kutoa mafunzo kwa viongozi wa eneo hilo na jamii ili kuzuia na kukabiliana na unyonyaji na unyanyasaji, na pia kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kupitia kliniki zinazohamishika. Shirika pia linasaidia watoto kupata elimu ya msingi kwa kujenga madarasa, kutoa mafunzo kwa walimu na kusambaza vifaa vya elimu.

09 February 2024, 13:51