Tafuta

Wanafunzi wa Shahada Chuo Kikuu Katoliki cha Kiethiopia cha Mtakatifu Thomas wa Akwino. Wanafunzi wa Shahada Chuo Kikuu Katoliki cha Kiethiopia cha Mtakatifu Thomas wa Akwino. 

Siku ya Kimataifa ya Elimu 2024 imejikita kukabiliana na kauli za chuki

Kila tarehe 24 Januari ya kila mwaka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) hufanya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Elimu.Kwa mwaka huu lengo ni kuakisi jukumu muhimu la elimu na walimu katika kukabiliana na kauli za chuki,jambo ambalo limekithiri katika miaka ya hivi karibuni kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limetumia maadhimisho ya mwaka 2024 ya Siku ya Kimataifa ya Elimu kuakisi jukumu muhimu la elimu na walimu katika kukabiliana na kauli za chuki, jambo ambalo limekithiri katika miaka ya hivi karibuni kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii na hivyo kuharibu muundo wa jamii duniani.  UNESCO kama  shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika moja kwa moja na jukumu la kuratibu maadhimisho ya siku ya  kimataifa ya elimu inayodhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Januari, limebainisha kuwa  ulimwengu unashuhudia ongezeko la migogoro inayoambatana na ongezeko la kutisha la ubaguzi, ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni, na kauli za chuki. Na kwa kuwa madhara  haya yanavuka mipaka yoyote ya kijiografia, jinsia, rangi, dini, siasa, nje ya mtandao na mtandaoni elimu ni msingi wa kufanikisha kupambana na hali hiyo.

Elimu kwa ajili ya amani ya kudumu

Kwa mujibu wa Audrey Azoulay na ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO kupitia ujumbe wake maalum kwa siku hii akifafanua kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni “Elimu kwa ajili ya amani ya kudumu” alisema, “kwa sababu kama chuki inaanza kwa maneno, basi amani inaanza na elimu. Tunachojifunza hubadilisha jinsi tunavyouona ulimwengu na huathiri jinsi tunavyowatendea wengine. Kwa hivyo alisisitiza kuwa elimu lazima iwe kiini cha juhudi zetu za kufikia na kudumisha amani ya ulimwengu.” Alisisitiza kwamba, “katika siku hii, kujitolea kwako kutetea haki ya elimu bora ambayo inatambua haki za binadamu za kila mtu inamaanisha kujitolea kwa mustakabali wa amani kwa wote, ambapo kila mtu anaweza kuishi maisha ya utu, kwa kuelewana na heshima.”

Mafunzo yaliyotolewa na Unesco kwa walimu

Ili mawazo haya yawafikie watu wengi zaidi ulimwenguni, UNESCO  katika afla hiyo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani iliwakutanisha wadau wa elimu kutoka ulimwenguni ili kujadili mchango muhimu wa elimu katika kufikia amani endelevu duniani. Pia  limefanya mafunzo kwa njia ya mtandaoni ya siku moja kwa maelfu ya walimu kutoka ulimwenguni kote kuhusu utatuzi wa kauli za chuki, ambayo yamewapa zana za kutambua vyema, kukabiliana na kuzuia matukio ya kauli za chuki. Mafunzo haya ni sehemu ya hatua ya UNESCO kusaidia Nchi Wanachama na wataalamu wake wa elimu kushughulikia kauli za chuki kupitia elimu.

Siku ya Elimi Kimataifa 24 Januari 2024
25 January 2024, 18:48