Tafuta

Ili kuepuka ubadhirifu wa fedha ya umma kuna haja kwa watanzania kujenga utamaduni wa uadilifu na uaminifu kwa kuhakikisha kwamba fedha inayokusanywa inatumika kadiri ilivyokusudiwa. Ili kuepuka ubadhirifu wa fedha ya umma kuna haja kwa watanzania kujenga utamaduni wa uadilifu na uaminifu kwa kuhakikisha kwamba fedha inayokusanywa inatumika kadiri ilivyokusudiwa.  

Matumizi ya Fedha ya Umma Yanahitaji: Uaminifu na Uadilifu Mkubwa

Waziri mkuu wa Tanzania amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Kamati ya Ulinzi ya Mkoa huo wawasake watu 72 waliohusika na upotevu wa fedha za Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ili wazirudishe na kuchukuliwa hatua za kinidhamu. “RC na KU yako pitieni ripoti ya ukaguzi maalum uliofanywa na CAG kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa fedha hapa Mbozi na muwashirikishe madiwani. Watu hao watafutwe walipe hela zetu na wachukuliwe hatua za kinidhamu,”

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Songwe, Tanzania.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Kamati ya Ulinzi ya Mkoa huo wawasake watu 72 waliohusika na upotevu wa fedha za Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ili wazirudishe na kuchukuliwa hatua za kinidhamu. “RC na KU yako pitieni ripoti ya ukaguzi maalum uliofanywa na CAG kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa fedha hapa Mbozi na muwashirikishe madiwani. Watu hao watafutwe walipe hela zetu na wachukuliwe hatua za kinidhamu,” alisema. Ametoa agizo hilo Ijumaa, Novemba 24, 2023, wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Halmashauri ya Mbozi, Madiwani kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo. Akizungumzia mapato na matumizi ya Halmashauri hiyo, Waziri Mkuu alisisitiza suala la uaminifu miongoni mwa watumishi wa umma hasa wa vitengo vya manunuzi na uhasibu ambapo alisema taarifa hiyo imebainisha uwepo wa wizi wa wazi katika manunuzi. “Mojawapo ya masuala yaliyojitokeza kwenye taarifa hiyo ni manunuzi ya vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 406 bila risiti. Haiwezekani kabisa kwamba sisi tukaenda kufanya manunuzi lakini hatudai risiti wakati tunajua ni hela ya Serikali.” Akizungumzia tuhuma za ujenzi wa shule ya sekondari ya Kisimani, watumishi hao walibadilisha ramani bila idhini kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na kusababisha gharama za ujenzi zipande. “Tulikuwa na ramani ya awali kwa gharama ya sh. milioni 466 lakini ninyi mkabadilisha ramani na kuongeza sh. milioni 206 lakini timu ilipoenda kukagua eneo la mradi, ilibaini uwepo wa nyufa, fremu za milango kupinda na kupishana na venti 28 kutowekewa nondo wala vioo.”

Waziri mkuu ataka ripoti ya CAG MBozi ifanyiwe kazi mara moja.
Waziri mkuu ataka ripoti ya CAG MBozi ifanyiwe kazi mara moja.

Akibainisha makosa mengine, Waziri Mkuu alisema taarifa hiyo imeonesha kuwa kuna upotevu wa sh. 292,375,419.93 za makusanyo yaliyoainishwa katika Mfumo wa Mapato (LGRCIS) lakini hazikuwasilishwa benki.“Kati ya hizo, shilingi 90, ,578.14 zilikusanywa lakini hazikuwasilishwa benki na wakusanyaji 44; shilingi 66,821,913.26 zilikuwa ni miamala iliyoingizwa kimakosa katika mfumo huo; shilingi 65,570,298.61 kutofafanuliwa kutokana na wakusanyaji 28 ambao ni mawakala na Watendaji wa Vijiji kutowasilisha ufafanuzi; shilingi 64,182,729.91 ziliwasilishwa benki na wahusika wakati ukaguzi maalum unaendelea na shilingi 5,129,900 ziliwasilishwa katika akaunti ya amana ya Halmashauri badala ya akaunti  ya mapato.” Akitoa mifano zaidi, Waziri Mkuu alisema: “Kuna wakala alikusanya sh.15,310,500.00 lakini yeye akapeleka benki sh. 310,500.00 tu na ile sh. milioni 15 ameweka mfukoni, haikubaliki. Mwingine alikusanya 2,357,100.00 akapeleka benki sh. 875,300.00 na sh. Milioni 1.481,800.00 amekula. Wa tatu alikusanya sh. 12,597,020.00 akapeleka benki sh. 101,500.00, na wa nne alikusanya sh.18,902,710.00 akapeleka benki sh. 13,725,510.00 na pesa ilibakia ya sh.5,177,200 ameila. Hawa mnawajua na baadhi yao ni watendaji wa vijiji. Watafutwe na warudishe hizi fedha.” Alisema upotevu mwingine wa fedha ulitokana na mauzo ya kahawa za wakulima ambapo mzigo wa kahawa wenye thamani ya sh. bilioni 1.18 umepotea. “Halmashauri hii inafanya kazi kwa karibu na Bodi ya Kahawa. Kahawa za wakulima zilipotea lakini pia mlishindwa kusimamia ushuru wa zaidi ya sh. milioni 75 ambao ulipaswa kulipwa na bodi hiyo na kuingia Halmashauri.” Aliwasisitiza watumishi hao watambue kuwa kazi ya makusanyo ya mapato inahitaji uaminifu na uadilifu. “Wakati Serikali inakimbizana kukusanya mapato, wako watu wengine wanatushika mashati na kutuvuta tusiende mbele.”

Nidhamu, maadili na utu wema ni muhimu katika uwajibikaji serikalini
Nidhamu, maadili na utu wema ni muhimu katika uwajibikaji serikalini

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) za mkoa wa Songwe katika eneo la Nselewa Mlowo, wilayani Mbozi. Ujenzi wa ofisi hiyo ambao ulianza Februari 16, 2023 unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 8.98 na utakamilika Juni 17, 2024. Akizungumza na viongozi mbalimbali na wananchi waliohudhuria, Ijumaa, Novemba 24, 2023, Waziri Mkuu alisema mkoa huo ni mkoa tegemeo kwenye makusanyo kwani siku za karibuni Serikali inatarajia kujenga kituo cha forodha katika eneo la Isongole, wilayani Ileje, jirani na mpaka wa Malawi. “Haya ni maandalizi ya miundombinu ya kuwasaidia wao wapate huduma bora zaidi. Niwasihi Watanzania msisahau kulipa kodi. Mkakati wa Serikali ni kuongeza mapato ya bajeti hadi asilimia 95 na kama mtu atataka kutuunga mkono iwe ni nyongeza tu,” alisema. Akizungumza na mafundi wanaofanya kazi hiyo, Waziri Mkuu alisema mkakati wa Taifa ambao Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameusisitiza ni kuhakikisha mafunzo ya ujuzi yanafikishwa hadi kwenye ngazi za chini na ndiyo maana kila wilaya inapelekewa VETA. “Naamini mkimaliza ujenzi huu, lazima mtakuwa na ujuzi na ufundi ambao mtaweza kuutumia katika siku zijazo,” alisema. Mapema, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa miundombinu kwenye shule mpya ya msingi ya Dkt. Samia iliyoko kata ya Mlowo, wilayani Mbozi, mkoani Songwe. Akizungumza na walimu, baadhi ya wazazi na wanafunzi waliokuwepo, Waziri Mkuu alisema shule hiyo ni ya viwango vya hali ya juu na akawapongeza kwa kutumia vizuri fedha za mradi huo.

Ripoti ya CAG Mbozi ifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo
Ripoti ya CAG Mbozi ifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo

“Ni shule ya pekee, nimevutiwa na ofisi ya mwalimu mkuu, nimekagua madarasa ni mazuri, nimetembelea madarasa ya awali na kukuta kuna michezo na zana za kufundishia. Nampongeza Mwalimu Mkuu kwani amesimamia vizuri sana mradi huu.” Akisoma taarifa ya ujenzi wa miundombinu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Bw. Abdallah Nandonde alisema uamuzi wa Serikali ya awamu ya sita kuanzisha mpango wa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, ulisababisha kuongezeka kwa uandikishaji wa wanafunzi katika shule mama ya msingi ya Lutumbi kutoka wanafunzi 1,650 mwaka 2015 na kufikisha wanafunzi 2,259 mwaka 2023. “Ongezeko hilo la uandikishaji lilileta changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa 28. Kupitia Mradi wa Kuboresha Sekta ya Elimu (BOOST), Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ilipokea shilingi milioni 538.5 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuongeza ufanisi katika ufundishaji na kujifunzia,” alisema. Alisema ujenzi wa mradi huo ambao umetekelezwa kwa njia ya "Force Account" ulianza Mei 3, 2023 na kukamilika Julai 20, 2023. “Mradi umekamilika kwa asilimia 100 na ulihusisha ujenzi wa madarasa 14 ya wanafunzi wa shule ya msingi, madarasa mawili ya awali, matundu sita ya vyoo vya wanafunzi wa awali, matundu 18 ya vyoo vya wanafunzi wa msingi, matundu mawili ya vyoo vya walimu, jengo la utawala na kichomea taka.”

Maeneo ya kufundishia hayana budi kuwa na mvuto kwa wanafunzi
Maeneo ya kufundishia hayana budi kuwa na mvuto kwa wanafunzi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi na wananchi wa Vwawa wilayani Mbozi, mkoani Songwe wabuni vyanzo vipya vya mapato na wachangamkie fursa za uwekezaji. Ametoa wito huo, Ijumaa, Novemba 24, 2023 wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji huo waliojitokeza kwenye viwanja vya Malori kumsikiliza akiwa katika ziara ya siku tatu mkoani humo kukagua shughuli za maendeleo. Aliwashauri wajenge kituo cha kulaza malori ili yanapopaki yaweze kulipa ushuru lakini pia madereva wa hayo malori wakihitaji kufanya service au matengenezo ya magari yao, watakaotoa hizo huduma watakuwa ni wana-Mbozi. “Tengeni ekari 50 ziwe za maegesho ya magari, wekeni uzio na mle ndani kuwe na huduma za akinababa lishe na mamalishe. Hawa wenye magari watakula, watanunua vinywaji baridi lakini wakitaka huduma za magari yao kama grisi, oil, watapata huduma hizo humohumo,” alisema. “Vilevile, jengeni nyumba za kulala wageni na mahoteli ya viwango tofauti tofauti. Madereva wakija kupaki malori yao, watataka kulala kwenye Guest Houses badala kulala kwenye magari. Hatua hiyo itasaidia kuchangia mapato ya Halmashauri lakini pia kipato cha mtu mmoja mmoja kitaongezeka,” alisisitiza.

Mazingira bora ya kufundishia ni muhimu kwa watoto wa shule
Mazingira bora ya kufundishia ni muhimu kwa watoto wa shule

Mapema, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasenkeya aliwaeleza wakazi hao kwamba Serikali italipa fidia ya sh. bilioni 4.8 kwa wakazi 494 wa kijiji cha Iboya, kata ya Ihanda waliofanyiwa tathmini kupisha ujenzi wa kituo cha kimataifa cha ukaguzi wa magari yanayofanya safari za nje ya nchi. Alisema Serikali ya awamu ya sita inataka kujenga Kituo cha Kimataifa cha Mizani (One-stop Inspection Station) ambacho kitakuwa na ofisi mbalimbali na panafanyika ukaguzi wa magari yanayoenda Tunduma. “Kituo kitakuwa na barabara zenye urefu wa km. 2.5 kwa pande zote za barabara na itachukua mita 300 kila upande wa barabara. Kikikamilika, kitapunguza sana msongamano wa magari kwani wakishamaliza kukaguliwa na kupima, wanaenda moja kwa moja hadi upande wa pili wa mpaka,” alisema wakati akielezea sifa za mradi huo. “Miaka ya nyuma tulifanya tathmini na kupata sh. bilioni 3.1 zinazotakiwa kulipa fidia kwa wakazi hao lakini tathmini ya hivi karibuni imefanyika na kubaini kuwa jumla ya fidia yote ni sh. bilioni 4.8. Na sasa hivi jedwali la malipo liko kwa Mlipaji Mkuu (HAZINA) ili kuthibitisha wanaostahili kulipwa,” alisema. Naye, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema kuwa wamekwishalipa sh. bilioni 23.54 kwa wananchi waliouza mazao yao kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA). “Tulitenga sh. bilioni 23.9 na tumeshalipa sh. bilioni 23.54 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amenithibitishia kwamba kiasi kilichobakia cha sh. milioni 360, kitalipwa kabla ya Jumatano, na baada ya hapo, tutaanza tena kununua mazao ya wana-Mbozi,” alisema.

25 November 2023, 09:21