Tafuta

Siyo haki vilio vya watoto na watu wazima huko Gaza Siyo haki vilio vya watoto na watu wazima huko Gaza  (AFP or licensors)

Mashariki ya Kati.Wakurugenzi wa/UNICEF/UNFPA/WHO,mapigani yasitishwe mara moja

Wakurugenzi wa Kanda wa UNICEF,UNFPA na WHO wametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kukomesha mashambulizi dhidi ya huduma za afya huko Gaza.Mashambulizi dhidi ya vituo vya matibabu na raia hayakubaliki na yanajumuisha ukiukwaji wa sheria na Mikataba ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu.Hayawezi kuvumiliwa.

Na Angella Rwezaula, - Vatican

Kutoka katika taarifa ya Adele Khodr, Mkurugenzi wa UNICEF wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini; Laila Baker, Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Umoja wa Mataifa la afya na mpango wa uzazi(UNFPA) kwa Mataifa ya Kiarabu; Ahmed Al-Mandhari, Mkurugenzi wa Afya Ulinguni (WHO )Kanda ya Mashariki ya Mediterania wametoa  wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kukomesha mashambulizi dhidi ya huduma za afya huko Gaza. Wakurugenzi hao wanabainisha kuwa Tumeshtushwa na ripoti za hivi punde za mashambulizi katika maeneo ya karibu na Hospitali ya Al-Shifa, Hospitali ya Watoto ya Al-Rantissi Naser, Hospitali ya Al-Quds na nyinginezo katika Mji wa Gaza na Kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, ambayo yamesababisha wahanga wengi wakiwemo watoto. . Uhasama mkali unaozingira hospitali kadhaa kaskazini mwa Gaza huzuia ufikiaji salama kwa wafanyikazi wa matibabu, waliojeruhiwa na wagonjwa wengine.

Vifo vingi kurekodiwa kwenye vituo vya afya

Watoto waliozaliwa kabla ya wakati (njiti)na wanaosubiri msaada wa maisha wameripotiwa kufariki kutokana na ukosefu wa umeme, oksijeni na maji kukatika katika Hospitali ya Al-Shifa, huku wengine wakiwa hatarini. Wafanyakazi katika hospitali kadhaa wanaripoti uhaba wa mafuta, maji na vifaa vya kimsingi vya matibabu, na hivyo kuweka maisha ya wagonjwa wote katika hatari ya haraka. Katika muda wa siku 36 zilizopita, WHO imerekodi angalau mashambulizi 137 dhidi ya vituo vya huduma za afya huko Gaza, na kusababisha vifo vya watu 521 na majeruhi 686, ikiwa ni pamoja na vifo 16 na majeruhi 38 kati ya wafanyakazi wa afya waliokuwa zamu.

Mashambulizi dhidi ya vituo vya afya hayakubaliki

Wakurugeniz hawa wamesisitiza kuwa Mashambulizi dhidi ya vituo vya matibabu na raia hayakubaliki na yanajumuisha ukiukaji wa sheria na Mikataba ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu. Haziwezi kuvumiliwa. Haki ya kutafuta matibabu, haswa wakati wa shida, haipaswi kukataliwa. Zaidi ya nusu ya hospitali katika Ukanda wa Gaza zimefungwa. Wale ambao bado wanafanya kazi wako chini ya mkazo mkubwa na wanaweza tu kutoa huduma chache za dharura, upasuaji wa kuokoa maisha na huduma za wagonjwa mahututi. Uhaba wa maji, chakula na mafuta pia unatishia ustawi wa maelfu ya watu waliokimbia makazi yao, wakiwemo wanawake na watoto, ambao wanapata hifadhi ndani na karibu na hospitali. 

Ulimwengu hauwezi kukaa kimya katika hali hii

Kwa mujibu wa wakurugenzi wa UNICEF, UNFPA na WHO wanabainisha kuwa Ulimwengu hauwezi kukaa kimya wakati hospitali, ambazo zinapaswa kuwa maficho salama, zikibadilika na kuwa matukio ya kifo, uharibifu na kukata tamaa. Hatua madhubuti za kimataifa zinahitajika ili kupata usitishaji mapigano wa haraka wa kibinadamu na kuzuia upotezaji zaidi wa maisha, pamoja na kuhifadhi mabaki ya mfumo wa afya wa Gaza. Ufikiaji wa bure, salama na endelevu unahitajika ili kutoa mafuta, vifaa vya matibabu na maji kwa huduma hizi za kuokoa maisha. Vurugu lazima iishe sasa! Wanahitimisha wito wao.

13 November 2023, 11:27