Tafuta

Kongamano la Kimataifa la Wakimbizi kwa mwaka 2023 litafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 15 Desemba 2023 huko Palexpo, Geneva, nchini Uswisi Kongamano la Kimataifa la Wakimbizi kwa mwaka 2023 litafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 15 Desemba 2023 huko Palexpo, Geneva, nchini Uswisi  (AFP or licensors)

Kongamano la Kimataifa la Wakimbizi Kwa Mwaka 2023, Kufanyika Uswisi

Kongamano hili la Kimataifa hufanyika kila baada ya miaka minne, lengo ni kusaidia utekelezaji kwa vitendo malengo yaliyowekwa katika Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi: Kupunguza shinikizo kwa nchi zinazowahifadhi wakimbizi, kuimarisha hali ya wakimbizi kujitegemea, kuongeza ufikiaji wa suluhu za nchi ya tatu na kuboresha hali katika nchi wanakotoka. Kongamano hili linatoa fursa kwa Mataifa wadau kutangaza ahadi na michango yao madhubuti kwa wakimbizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kongamano la Kimataifa la Wakimbizi kwa mwaka 2023 litafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 15 Desemba 2023 huko Palexpo, Geneva, nchini Uswisi, na matukio yanayohusiana yatafanyika katika maeneo mengine kuanzia tarehe 12 Desemba na kuendelea. Kongamano hili la Kimataifa hufanyika kila baada ya miaka minne, lengo ni kusaidia utekelezaji kwa vitendo malengo yaliyowekwa katika Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi: Kupunguza shinikizo kwa nchi zinazowahifadhi wakimbizi, kuimarisha hali ya wakimbizi kujitegemea, kuongeza ufikiaji wa suluhu za nchi ya tatu na kuboresha hali katika nchi wanakotoka. Kongamano hili linatoa fursa kwa Mataifa wadau kutangaza ahadi na michango yao madhubuti mintarafu maendeleo yaliyopatikana, kushiriki mazoea mazuri pamoja na kutathmini changamoto na fursa zilizopo. Kongamano la 2023 limeitishwa kwa pamoja na Mataifa matano yaani: Colombia, Ufaransa, Japan, Yordan na Uganda, na kuratibiwa kwa pamoja na Serikali ya Uswisi pamoja na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa,  UNHCR.

Wakimbizi na wahamiaji ni changamoto kubwa ulimwenguni
Wakimbizi na wahamiaji ni changamoto kubwa ulimwenguni

Mashirika ya misaada kwa wakimbizi yamezitupia lawama nchi za Ugiriki, Malta na Italia kwa kushindwa kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuokoa maisha ya wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kupoteza maisha yao kwenye Bahari ya Mediterrania. Kimsingi, “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018” unapania pamoja na mambo mengine: Kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Ingawa Mkataba huu hauzifungi kisheria nchi husika, lakini ni muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa kama chombo cha rejea katika mchakato wa kudumisha uhai na haki msingi za binadamu. Kumbe, haki msingi za binadamu pamoja na mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake ni mambo muhimu sana. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji wote waliofariki dunia pamoja na kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti zaidi ili maafa kama haya yasijitokeze tena kwa siku za baadaye.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linahitaji majadiliano ya kina.
Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linahitaji majadiliano ya kina.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wakimbizi wanawakilisha roho bora zaidi ya kibinadamu. Wanahitaji na wanastahili kuungwa mkono na kupewa mshikamano wa kutosha na wala sio mipaka iliyofungwa na hivyo kulazimika kurudi nyuma walikotoka. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, zaidi ya watu milioni mia moja wanaoishi katika nchi zinazokumbwa na migogoro, kinzani na mipasuko ya kijamii; mateso, njaa pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi wamelazimika kuyahama makazi na nchi zao ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Waathirika wakuu ni watoto na wanawake wanaolazimika kufanya safari ngumu, huku wakikabiliwa na vitendo vya unyanyasi, unyonyaji, ubaguzi na ukatili mkubwa. Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani ni ukumbusho kwa Jumuiya ya Kimataifa kwamba, inawajibu wa kuwalinda na kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji, kwa kuwapatia msaada wa kutosha, makazi na kuwasaidia kujenga upya maisha yao, kwa kutoa kipaumbele kwa utu, heshima na haki zao msingi. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kunahitajika msaada mkubwa kwa nchi zinazowakaribisha wakimbizi na wahamiaji kadiri ya Mtakaba wa Kimataifa juu ya wakimbizi na wahamiaji; kwa kuongeza fursa za elimu bora zaidi, makazi yenye staha, huduma bora za afya na ulinzi wa kijamii sanjari na kuongeza ari na nguvu zaidi katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani, ili hatimaye, wakimbizi waweze kurejea makwao salama salimini. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuunganisha matumaini ambayo wakimbizi wanayabeba nyoyoni mwao, kwa kuunganisha ujasiri wao pamoja na fursa wanazohitaji katika kila hatua ya maisha yao.

Wakimbizi 2023
25 November 2023, 13:15