Tafuta

Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani 16-20 Oktoba 2023 umefunguliwa rasmi tarehe 16 Oktoba 2023 na Rais Sergio Mattarella wa Italia Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani 16-20 Oktoba 2023 umefunguliwa rasmi tarehe 16 Oktoba 2023 na Rais Sergio Mattarella wa Italia  (ANSA)

Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani Kwa Mwaka 2023

Siku ya Chakula Duniani ilianza kuadhimishwa kunako mwaka 1981 na ilichaguliwa tarehe 16 Oktoba kwa kuwa ni tarehe ambayo mwaka 1945 lilianzishwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO, lenye Makao yake Makuu mjini Roma, nchini Italia. Maadhimisho ya Siku 43 ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Maji ni uhai, Maji ni chakula. Pia kumefanyika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani kwa Mwaka 2023.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Roma, Italia

Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa nchini Italia kuja Tanzania kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa kuwa Tanzania ina malighafi za kutosha pamoja na uwepo wa masoko ya uhakika kutokana na eneo la kijiografia. “Msisitizo wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mkakati wa Serikali ni kuwahamasisha wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa mbalimbali nchini Tanzania waje kuwekeza katika ujenzi na kuzalisha bidhaa hizo nchini ili zipatikane kwa wingi na kwa urahisi.” Ameyasema hayo Alhamisi, Oktoba 19, 2023) wakati akizungumza katika Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia lililofanyika kwenye “Palazzo Regione Lombardia,” Milan nchini Italia. Waziri Mkuu yuko nchini Italia akimuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023, Roma nchini Italia. Mheshimiwa Majaliwa ametaja baadhi ya maeneo ambayo wawekezaji hao wanaweza kuja kuwekeza katika sekta za madini, kilimo, mawasiliano, mifugo, uvuvi, utalii na afya hivyo amewakaribisha wafanyabiashara hao na wawekezaji watumie fursa hiyo na kuwekeza nchini. Aidha, Waziri Mkuu amesema licha ya Tanzania kuwa na maeneo na mazingira mazuri ya uwekezaji pia amesema nchi ina vivutio vingi vya utalii hivyo, amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara, pia Mheshimiwa Majaliwa ameyakaribisha makampuni na mawakala wa utalii waje nchini na kuwekeza katika ujenzi wa hoteli za kitalii katika miji mbalimbali yakiwemo majiji ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma. Mheshimiwa Majaliwa amesema kwa sasa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara, viwanja vya ndege na nishati ya uhakika ili kurahisisha shughuli mbalimbali zikiwemo za uwekezaji.

Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2023.
Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2023.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo ametumia fursa hiyo kuwahakikishia ushirikiano wawekezaji na wafanyabiashara wote kutoka nchini Italia ambao watahitaji kuwekeza na kufanya biashara nchini Tanzania. Jukwaa hilo la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia limehudhuriwa na wafanyabiashara na wawekezaji zaidi ya 300 kutoka mataifa hayo mawili. Pia, mbali na wafanyabiashara na wawekezaji pia limehudhuriwa na Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Taasisi hizo ni pamoja Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ambao viongozi wake walipata fursa ya kutaja fursa za uwekezaji zilizopo nchini pamoja na namna ya kuwawezesha kuyafikia maeneo hayo. Wakati huo huo, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) Dkt. Qu Dongyu amesema kuwa Shirika hilo limevutiwa na mradi wa kuwawezesha vijana unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania wa Jenga Kesho Iliyobora “Building Better Tomorrow” (BBT). “FAO tutaunga mkono mradi huu ili Serikali ya Tanzania iweze kutimiza malengo ya kuwainua vijana na wanawake kwenye sekta ya kilimo kama ilivyo moja ya agenda kwenye mkutano wa FAO wa mwaka 2023.” Ameyasema hayo Jumatano, Oktoba 18, 2023 alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ofisi za Makao Makuu ya FAO zilizopo Roma, Italia. Waziri Mkuu yuko nchini Italia akimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023.

FAO inaunga mkono jitihada za Tanzania katika maboresho ya sekta ya kilimo
FAO inaunga mkono jitihada za Tanzania katika maboresho ya sekta ya kilimo

Aidha, Mkurugenzi huyo amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sekta ya kilimo pamoja na kuboresha mahusiano na mashiriki ya kimataifa. Dkt. Dongyu ameahidi kutembelea Tanzania mwaka 2024 kwa ajili ya kujionea maendeleo katika sekta ya kilimo pamoja na kupanua wigo wa majadiliano kati ya Tanzania na Shirika hilo ili kuendelea kuwezesha zaidi sekta ya kilimo na uchumi wa Bluu. Kwa upande wake, Waziri Mkuu alisema kwa sasa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanza kupanua wigo wa kilimo kutoka cha kutegemea mvua na kujikita zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji, ambapo imetenga shilingi bilioni 900. “Kilimo ndio maisha, kilimo ndio chakula, tunataka kujikita zaidi katika kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia mabwawa yetu/ Tunataka tujiridhishe kuwa hakuna Mtanzania atayekufa kwa kukosa chakula.” Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali inaendelea kufanya maboresho katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na kuhakikisha kinasimamiwa kwa kiwango cha juu ili kuzalisha chakula cha kutosha kwa matumizi ya ndani na ziada kuuza nje. Kadhalika, Waziri Mkuu alisema kuwa mbali na maboresho hayo yaliyofanyika katika sekta ya kilimo, pia Serikali inawasimia wakulima kuanzia hatua za awali za maandalizi ya mashamba hadi kwenye utafutaji wa masoko kupitia maafisa ugani ambao wapo hadi vijijini. Pia, Waziri Mkuu Alisema Serikali imeanza kusajili wakulima katika mfumo wa kidigitali lengo ni kujua idadi ya wakulima, ukubwa wa mashamba pamoja na aina ya mazao wanayolima ili kurahisisha ufikishwaji wa huduma za ugani kwa wakati zikiwemo pembejeo. “Usajili huo hautaishia kwa wakulima pekee bado utaendelea hadi kwa wavuvi, wafugaji pamoja na watumiaji wote wa ardhi.” Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa alitumia fursa hiyo kuishukuru FAO kwa uamuzi wake wa kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa mpango wa BBT ambao unalenga kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki katika kilimo chenye tija.

Wajumbe wa Mkutano wa FAO
Wajumbe wa Mkutano wa FAO

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) limeahidi kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo. Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zina mipango ya kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula ndani ya nchi na ziada kuuza nje ifikapo 2030. Waziri Mkuu ameyasema hayo Jumatatu, Oktoba 16, 2023) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023. Waziri Mkuu amehutubia mkutano huo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Kabla ya ufunguzi wa mkutano huo uliowahusisha Wakuu wa nchi na Serikali, Waziri Mkuu alishiriki katika Maadhimisho ya miaka 78 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO). "Pamoja na jitihada ambazo tumeziweka ndani za kushirikisha vijana na wanawake kuhakikisha kwamba tunaongeza teknolojia, kutumia mbolea kwenye kilimo, pamoja na ushirikishaji wa sekta binafsi, tumeamua kuungana na FAO kupitia Mkurugenzi Mkuu na wameahidi kutuunga mkono kwenye Sekta ya kilimo." Amesema Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara na nishati vijijini ili kurahisisha shughuli za kilimo. “Maboresho mengine ni ujenzi wa viwanda vya kuzalisha pembejeo za kilimo na kuhamasisha wakulima kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji.”

Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia
Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dkt. Qu Dongyu amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kuendeleza sekta ya kilimo na uchumi wa bluu, hivyo Shirika lao liko tayari kushirikiana na Tanzania katika kutoa msaada wa kitaalam pamoja na kukuza mifumo ya uzalishaji wa chakula. Naye, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamata Shaame Hamisi alisema kwa sasa Serikali inafanya maboresho makubwa katika sekta ya kilimo na miongoni mwa maboresho hayo ni utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji ambayo inalenga kuimarisha upatikanaji wa chakula. Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema Serikali imeendelea kuwashawishi vijana kushiriki katika shughuli za kilimo kwani mbali na kuongeza uzalishaji wa chakula, pia kilimo ni miongoni mwa sekta zinazotoa ajira nyingi, hivyo watakuwa wamejihakikishia ajira. Mkutano huo ulifunguliwa na Rais wa Italia Mhe. Sergio Mattarella na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Ireland Mhe. Michael Higgine, Rais wa Iraq Mhe. Abdul Latif Rashid, Mfalme wa Lesotho, Viongozi wa Ujumbe kutoka Nchi Wanachama, Viongozi Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (FAO, IFAD & WFP). Waziri mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na watumishi wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, ambapo pamoja na mambo mengine amewataka waendelee kuimarisha mahusiano ya kihistoria yaliyopo kati ya Tanzania na Italia. Mheshimiwa Majaliwa amesema nchi inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo, elimu, mifugo, afya hivyo wao waendelee kufanya kazi kwa bidii, weledi pamoja na kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini ili Taifa linufaike na uwepo wao nchini Italia. Ameyasema hayo Jumanne, Oktoba 17, 2023) wakati akizungumza na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia alipotembelea ofisi hizo zilizopo jijini Rome. Waziri Mkuu alikuwa nchini Italia akimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan. Katika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023.

Mlima Kilimanjaro ni kati ya vivutio vikubwa vya Utalii, Tanzania
Mlima Kilimanjaro ni kati ya vivutio vikubwa vya Utalii, Tanzania

“Nchi ipo salama, uchumi unaendelea kukua na lugha yetu kwa sasa ni maendeleo ya nchi na Serikali inaendelea kuimarisha sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo ambayo inawanufaisha Watanzania wengi na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza watendaji wawe wabunifu katika kuboresha sekta hiyo, hivyo endeleeni kufanya kazi mkiwa na amani.” Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wafanyakazi hao waendelee kuwatambua na kuwaunganisha Watanzania wote waishio nchini Italia pamoja na sehemu nyingine ambazo ubalozi huo unazihudumia. Pia amewataka watumishi hao waendelee kufundisha lugha ya Kiswahili kupitia darasa walilolianzisha kwani ni fursa muhimu katika kulitangaza Taifa na utamaduni wa Watanzania Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo amemshukuru Mheshimiwa Majaliwa kwa kufanya ziara katika ofisi hizo za Ubalozi wa Tanzania nchini Italia na kwamba wamepokea maelekezo na ushauri alioutoa na wataufanyia kazi kwa maendeleo ya Taifa. Tanzania na Italia zina ushirikiano wa kimaendeleo tangu kuanzishwa uhusiano rasmi wa kidiplomasia, ambapo Tanzania ilifungua Ubalozi wake mjini Roma mwaka 1972 na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania ulifunguliwa rasmi mwaka 1961.

21 October 2023, 09:45