Tafuta

Juma la Mkutano wa tabianchi jijini Nairobi Kenya. Juma la Mkutano wa tabianchi jijini Nairobi Kenya.  (AFP or licensors)

Juma la mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi barani Afrika 2023

Viongozi wa Afrika wanakutana jijini Nairobi, Kenya wa juma moja uliofunguliwa tatrhe 4 Septemba 2023 unaohusu Mabadiliko ya Tabianchi, Mkutano wa kila mwaka ambao unajadili njia mbalimbali za kupunguza utoaji wa gesi chafuzi huku washiriki wakiwa na mbinu za kuweza kukabiliana na athari za tabianchi.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Katika Mkutano ulioanza Jumatatu ya tarehe 04 Septemba 2023 uliwaleta pamoja watunga sera, viongozi wafanyabiashara na wanaharakati wa mazingira kutoka kila pembe ya bara la Afrika. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Bwana Antonio Guterres ni miongoni mwa waliiohudhuria mkutano huo na ambaye aliuhutubia  katika siku ya kwanza ya mkutano huo. Juma zima la  mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi barani Afrika 2023 uliandaliwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi UNFCCC, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP, shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira duniani, UNEP, na Benki ya Dunia, kwa msaada wa wadau wa kikanda. Mkutano huo umekuja wakati Bara la Afrika linashuhudia kupanda kwa joto kwa kasi zaidi kuliko maeneo mengine duniani, kusababisha matukio ya mara kwa mara ya hali mbaya ya hewa na ukame wa muda mrefu, na kusababisha uhaba wa chakula na watu kupoteza maisha.

Wamasai katika tukio la Mkutano wa Tabianchi Jijini Nirobi 2023
Wamasai katika tukio la Mkutano wa Tabianchi Jijini Nirobi 2023

Kwa mujibu wa UNEP Afrika kwa ujumla inachangia chini ya asilimia 3 ya jumla ya hewa chafuzi duniani. Na katika mkutano huu viongozi ambao waemezungumza wamezidi kutoa wito wao  wa usaidizi wa kifedha ili kusaidia bara hilo kukabiliana na athari ziletwazo na mabadiliko ya tabianchi. Jula la mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi barani Afrika 2023 ni mojawapo ya wiki nne za mikutano ya mabadiliko ya tabianchi za kikanda zilizofanyika mwaka huu 2023. Mkutano huu umeundwa ili kuongeza kasi kabla ya viongozi hao kushiriki katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP28 huko Dubai baadae mwaka  huu 2023.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa WMO

Joto linaongezeka kwa kasi barani Afrika katika miongo ya hivi karibuni na hatari zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi zinazidi kuwa mbaya imesema ripoti kuhusu mabadiliko ya tabianchi iliyozinduliwa tarehe 4 Septemba 2023 na Shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa WMO. Uzinduzi wa ripoti hiyo iliyopewa jina la Hali ya Mabadiliko ya Tabianchi Barani Afrika 2022 ulifanyika jijini Nairobi, Kenya ambako siku hiyo ulianza  mkutano wa Bara la Afrika kujadili masuala ya mabadiliko ya tabianchi. Katibu Mkuu wa WMO Profesa Petteri Taalas amesema licha ya athari ambazo zimeonekana kwa muda mrefu kutokana na ongezeko hilo la joto lakini bado ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko hayo ni tone tu katika baharí ya kile linachohitajika.  “Afrika inawajibika kwa chini ya asilimia 10 ya uzalishaji wa gesi chafuzi duniani, lakini ni bara ambalo ndilo lenye uwezo mdogo zaidi wa kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi.” Amesema Prof Taalas na kuongeza kuwa “Mawimbi ya joto, mvua kubwa, mafuriko, vimbunga vya kitropiki, na ukame wa muda mrefu ni majanga ambayo yana madhara makubwa kwa jamii na uchumi, na namba ya watu walio hatarini ikizidi kuongezeka.

Mwakilishi Maalum John Kerry wa Marekani akihutubia Septemba 5 katika Mkutano wa Tabianchi huko Nirobi Kenya
Mwakilishi Maalum John Kerry wa Marekani akihutubia Septemba 5 katika Mkutano wa Tabianchi huko Nirobi Kenya

Zaidi ya watu milioni 110 barani Afrika waliathiriwa moja kwa moja na hali ya hewa, mabadiliko ya tabianchi na hatari zinazohusiana na maji mwaka 2022 na kusababisha uharibifu wa kiuchumi wa zaidi ya dola bilioni 8.5. Kuliripotiwa vifo 5,000, ambavyo asilimia 48 vilihusishwa na ukame na asilimia 43 vilihusishwa na mafuriko, kulingana na Hifadhidata ya Matukio ya Dharura. Hata hivyo imeelezwa kuwa takwimu halisi zinaweza kuwa juu zaidi kwa sababu ya utoaji wa ripoti kuwa wa kiwango cha chini. Mkuu wa WMO amebainisha kuwa Kuna mapungufu makubwa katika uchunguzi wa hali ya hewa barani Afrika na huduma za utoaji wa taarifa za hadhari mapema upo chini kwa kiasi kikubwa. “Tumedhamiria kuziba mapengo hayo na kuhakikisha kuwa taarifa za kutoa maonyo ya mapema ya kuokoa maisha yanamfikia kila mtu,” akasema. Kwa mujibu wa Kituo cha Sera ya Hali ya Hewa ya Afrika cha UNECA, gharama ya hasara na uharibifu barani Afrika kutokana na mabadiliko ya tabianchi inakadiriwa kuwa kati ya dola za Marekani bilioni 290 na dola bilioni 440, kulingana na kiwango cha ongezeko la joto.

Mjadala kuhusu tabianchi huko Nairobi Kenya
Mjadala kuhusu tabianchi huko Nairobi Kenya

Kilimo ni tegemeo kuu la maisha ya Afrika na uchumi wa kitaifa, kilimo kinasaidia zaidi ya asilimia 55 ya nguvu kazi. Lakini ripoti hii iliyozinduliwa  ilieleza kuwa ukuaji wa tija katika kilimo umepungua kwa asilimia 34 tangu mwaka 1961 kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Kupungua huku ni kwa kiwango cha juu zaidi ikilinganishwa na kile ambacho mabara mingine duniani yamepitia. Inakadiriwa kuwa uagizaji wa chakula wa kila mwaka kwa nchi za Kiafrika unatarajiwa kuongezeka kwa takriban mara tatu, kutoka dola za Kimarekani bilioni 35 hadi bilioni 110 ifikapo mwaka 2025. “Kwa kuzingatia athari hizi Afrika inazopata, udhaifu na uwezo mdogo wa kubadilika, athari za mabadiliko ya tabianchi watu wanatarajiwa kuhisi ukali zaidi wa athari hizo. Afya za watu, amani, ustawi, miundombinu, na shughuli nyingine za kiuchumi katika sekta nyingi barani Afrika zinakabiliwa na hatari kubwa zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi".

Mamasai walifanya maandamano
Mamasai walifanya maandamano

Aliyendika ripoti hiyo ni Balozi Josefa Leonel Correia Sacko, Kamishna wa Kilimo, Maendeleo ya Vijijini, Uchumi wa Bluu na Mazingira Endelevu katika Tume ya Muungano wa Afrika. Ripoti hii kwa hiyo inajumuisha maoni kutoka Tume ya Muungano wa Afrika, Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika, na michango kutoka kwa Mamlaka za Kitaifa za Hali ya Hewa na Uhaidrolojia barani Afrika, Vituo vya Hali ya Hewa vya Kikanda vya WMO, mashirika maalumu ya Umoja wa Mataifa, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Kundi la Ushauri la Utafiti wa Kilimo wa Kimataifa, na wataalamu na wanasayansi wengi.

08 September 2023, 11:32