Tafuta

Waendesha mjadala mkubwa wa kupinga mkataba wa Bandari nchini Tanzania kuwekwa mikononi mwa Polisi. Waendesha mjadala mkubwa wa kupinga mkataba wa Bandari nchini Tanzania kuwekwa mikononi mwa Polisi. 

Tanzania:Amnesty International inaomba waachiliwe wakosoaji wa mkataba wa bandari

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International linaomba kuachiliwa mara moja Wakosoaji wa mkataba wa bandari nchini Tanzania.Hawa ni Dk.Willibrod Slaa,aliyekuwa mbunge na Balozi wa Tanzania nchini Sweden,Boniface Mwabukusi,mwanasheria na mwanaharakati na Mdude Nyagali,mwanaharakati wa kisiasa,wote walikamatwa kati ya 12 na 13 Agosti.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Azimio la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu ni tamko  la kiUlimwengu la haki za binadamu au Taarifa ya Ulimwengu juu ya Haki za Binadamu(Universal Declaration of Human Rights) lilitolewa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu mnamo  tarehe 10 Desemba 1948. Ilikuwa kati ya maazimio ya kwanza kabisa  ya Umoja wa Mataifa (UN). Msingi wa haki hizo uko katika kifungo cha kwanza kinachosema, “Watu wote wamezaliwa huru, wakiwa na hadhi na haki sawa. Wamejaliwa akili na dhamiri na kupaswa kutendeana kwa roho ya kidugu.” Haki zinaorodheshwa katika vifungu 30 vinavyoeleza haki za msingi ambazo kila mtu anastahili kuwa nazo bila kubaguana kwa rangi, taifa, jinsia, dini, siasa, fikra, asili ya taifa la mtu, mali, kwa kizazi au kwa hali nyingine yoyote. Haki zilizomo katika tangazo hiLo  jinsi zilivyo si sheria ya kimataifa moja kwa moja, lakini zimekubaliwa na kila taifa lililojiunga na UN. Sehemu kubwa ya vipengele vyake imeingia katika mapatano ya kimataifa juu ya haki za kiraia na kisiasa ya mnamo mwaka 1966 na mapatano ya kimataifa juu ya haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ya mwaka 1976 na kwa njia hiyo zimekuwa sehemu ya sheria za kimataifa.

Watetezi wa haki za binadamu waomba kuachiliwa huru wakosoaji

Katika muktadha wa haki hizo, Shirika la kutetea haki za binadamu (Amnesty International), linaomba: “waachilie mara moja Wakosoaji waliozuiliwa wa mkataba wa bandari nchini Tanzania. Hawa ni Dk. Willibrod Slaa, aliyekuwa mbunge na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Boniface Mwabukusi, mwanasheria na mwanaharakati, na Mdude Nyagali, mwanaharakati wa kisiasa, ambao wote walikamatwa kati ya 12 na 13 Agosti  2023, kwa kosa la kukosoa makubaliano kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kuhusu bandari”. Hayo yalisemwa na Shirika la Amnesty International tarehe 14 Agosti 2023, kupitia kwa Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Kanda, Afrika Mashariki na Kusini, Amnesty International. Makubaliano hayo yanaweka mfumo wa kisheria kwa UAE kushirikiana na Tanzania katika maendeleo, usimamizi na uendeshaji wa bandari za Tanzania, kanda maalum za kiuchumi, mbuga za usafirishaji, korido za biashara na miundombinu mingine inayohusiana nayo.

Kwa hiyo: “Ukandamizaji wa mamlaka ya Tanzania dhidi ya wakosoaji wa mpango wa bandari ya UAE unaonesha kuongezeka kwa kutovumilia kwao upinzani. Mamlaka lazima ziache kuwashikilia wanaharakati kiholela kwa sababu tu ya kutoa maoni yao kwa amani na kuwaachilia mara moja na bila masharti wanaharakati hawa ili kuhakikisha kuheshimiwa kwa haki ya uhuru wa kujieleza,” alisisisitiza Tigere Chagutah.

Kwa mujibu wa taarifa hizi, Dk. W. Slaa, Mwabukusi na Nyagali wote wamekosoa hadharani mpango wa bandari. Mwabukusi aliongoza ombi la mahakama akidai kuwa mkataba wa bandari una vifungu vinavyokiuka Katiba ya Tanzania na kuhatarisha uhuru na usalama wa taifa. Kwa mujibu wa wakili wake, Dk Slaa alikamatwa na askari polisi nyumbani kwake Mbweni, Dar es Salaam, tarehe 13  Agosti majira ya saa 1:00 usiku na kupelekwa Kituo cha Polisi Mbweni. Kisha akarudishwa nyumbani kwake, ambapo polisi walifanya upekuzi na kumpokonya baadhi ya vifaa vyake vya mawasiliano. Baada ya upekuzi huo, polisi walimpeleka Dk Slaa Kituo cha Polisi Oysterbay.

Wakati huo huo Wakili wa Mwabukusi na Nyagali aliiambia Shirika la Amnesty International kwamba alipokea simu ya huzuni kutoka kwa wanaharakati hao wawili walipokamatwa na maafisa wa polisi tarehe 12 Agosti, mwendo wa saa 3:00 asubuhi. Kwa mujibu wa wakili huyo, Mwabukusi na Nyagali walikamatwa karibu na Mikumi mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanzania, walipokuwa wakisafiri kwenda Dar es Salaam kutoka Mbeya, kusini magharibi mwa Tanzania. Emmanuel Masonga, afisa wa chama cha upinzani, pia alikamatwa pamoja nao lakini akaachiliwa siku hiyo hiyo kwa amri ya kuripoti katika Kituo cha Polisi Mikumi tarehe 14 Agosti 2023. Mwabukusi na Nyagali kwa sasa wanashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Mbeya, wakiwa wamehamishwa kutoka Mikumi mchana. Kulingana na wakili wao, wanaharakati hao wawili wamekataa kula wala kunywa chochote tangu wakamatwe.

Kwa nini Mahakama ilitupilia mbali ombi lililowasilishwa?

Hata hivyo tarehe 10 Agosti, Mahakama Kuu ya Tanzania mjini Mbeya ilitupilia mbali ombi lililowasilishwa na Mwabukusi na wenzake wanne lililopinga uhalali wa mkataba wa bandari. Ombi hilo lilidai kuwa makubaliano hayo yanakiuka sheria za Tanzania kwani umma ulipewa siku mbili tu kuwasilisha maoni yao, na kwamba mkataba wenyewe unakiuka sheria za kimataifa na sheria za ndani za Tanzania kwa kukabidhi usimamizi wa maliasili kwa taasisi ya kigeni. "Kwa kuharamisha ukosoaji wa umma wa mkataba wa bandari, mamlaka ya Tanzania ni wazi inajaribu kuzima upinzani. Serikali inapaswa badala yake kuwezesha umma kushiriki katika mijadala ya masuala yote yenye maslahi kwa umma, ikiwa ni pamoja na makubaliano ya bandari ya UAE, na kuhakikisha masuala yote ya mkataba huo yana uwazi ili kuhakikisha ushirikishwaji wa maana wa umma,” alisema haya Tigere Chagutah Usuli Mkurugenzi wa Kanda, Afrika Mashariki na Kusini, Amnesty International.

Tukirudi nyuma kuibuka baadaye kwa sakata hili

Oktoba 2022, Rais Samia Suluhu Hassan na Ahmed Mahboob Musabih, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bandari, Forodha na Ukanda Huru, walitia saini makubaliano ya kusimamia bandari nchini Tanzania kwa niaba ya Imarati ya Dubai. Bunge la Tanzania liliidhinisha makubaliano hayo tarehe 10 Juni 2023, na tangu wakati huo sakati hili linaendelea. Kati ya Juni na Agosti 2023, angalau watu 24 walikamatwa  na baadaye kuachiliwa  kwa kukosoa mpango wa  mkataba wa bandari. Rugemeleza Nshala, mwanasheria, mwanaharakati na Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), naye alitoroka nchini Julai mosi baada ya kukabiliwa na vitisho vya kuuawa kwa kukosoa mpango huo. Mwabukusi na Nyagali hapo awali walikamatwa kuhusu makubaliano ya bandari tarehe 14 Julai, siku chache baada ya kufanya mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo walikosoa makubaliano ya bandari.

Shirika la Amnesty International linahusika na nini?

Amnesty International ni shirika la watu zaidi ya milioni 2 waliomo katika nchi 150 ambao hufanya kampeni ya kupigania haki za binadamu. Wanatekeleza haki na usawa na wanapinga ubaguzi. Wanazishinikiza serikali pamoja na makundi mengine yenye nguvu kuwaruhusu watu kuishi katika hadhi ya utu. Amnesty International ni shirika huru, halifungamani na serikali yoyote ile, wala chama chochote kile cha kimataifa au chama cha kisiasa. Hawaungi mkono itikadi yoyote ile, dini yoyote ile, au imani nyingine yoyote ile. Wanatumia viwango vya haki za binadamu vya kimataifa bila ya upendeleo katika hali zote. Shirika lao lina watu binafsi wanaofanya kazi za kuwasaidia watu wengine. Kazi yao inatiwa motisha na watu wote hasa ambao wanateseka au wameshuhudia vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu. Kesi za maisha hasa ya wanaume, wanawake na watoto ndio kiini cha kampeni zao.

Kazi yao  huanza kwa kuchunguza jambo lililotendeka. Ikiwa mtu anaamua kuwaeleza wao kile unachokifahamu, maelezo yako yatawsaidia wao kujua jambo linalotendeka na kuamua ni njia gani bora ya kuingilia kati. Ikiwa  wewe unakubali, inawezekana  wakawaeleza watu wengine kuhusu kisa chako. Watu duniani kote huenda wakajua jambo gani lilitendeka kwako au kwa familia yako. Maafisa wa serikali, watu wa jumuia yako na familia wangeweza kusoma habari zote kuhusu wewe.  Ikiwa unaamua kuwaruhusu  shirika hili kutumia picha yako, watu wengi huenda wangeweza kuona picha yako imechapishwa kwenye ripoti, au kwenye kompyuta.

Ni matumaini ya shirika hili la Amnesty International kuwa kwa kutumia maelezo ambayo unakuwa umewaeleza wao na kwa kuzungumza na wewe kuhusu njia gani bora ya kutumia maelezo yako kutakuwepo na hatua itakayochukuliwa kutatua hali ya mambo, na uvunjaji mchache wa haki za binadamu katika siku za baadaye. Shirika la kutetea haki za binadamu wananakili au kurekodi visa vya watu wengi ambao wanataka kuweleza wao jambo gani limewatokea wao au jambo gani wamelishuhudia.  Wakati mwngine watu wanawaomba wao wasitumie habari hizo hadharani au wasiseme ni wapi wamezipata habari hizo. Kwa hiyo Shirika la  hili la uytetezi wa haki za binadamu Siku zote wanayakubali na kuyaheshimu maombi hayo. Wakati mwngine wanazitumia habari hizo katika kampeni zao.

Hapa wanatoa mfano:

- Wanaweza kuzungumza na serikali kuhusu kesi yako. Hii ni pamoja na serikali yako mwenyewe na serikali nyinginezo.

- Wanaweza kuchapisha kisa chako kwenye vitu vinavyochapishwa kama vile kwenye ripoti, majarida na karatasi za  matangazo na pia kwenye intaneti. Visa ambavyo vimechapishwa vinaweza kuendelea kujulikana kwa muda wa miaka mingi.

- Wanaweza wakawaeleza waandishi wa habari kuhusu kesi yako, kwa hiyo kesi yako huenda ikaelezewa katika vyombo vya habari. Waandishi wa habari huenda wakataka kuzungumza na wewe na kukupiga picha.

Ndugu Msikilizaji wa Vatican News, kwa maelezo hayo unapata picha halisi ya shirika hili la kimataifa la kutetea haki za binadamu liitwalo Amnesty International na jinisi gani linavyo fanyakazi.

Amnesty International na utetezi wa haki huko Tanzania
16 August 2023, 10:07