Tafuta

Huko haiti kuna ukosefu wa chakula na ghasia ambazo zinawakumba watoto na wanawake. Huko haiti kuna ukosefu wa chakula na ghasia ambazo zinawakumba watoto na wanawake. 

Ghasia zaongezeka Haiti,wanawake na watoto 300 walitekwa nyara ndani ya miezi sita

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto ulibainisha ongezeko la kutisha la utekaji nyara nchini Haiti huku kukiwa na visa zaidi ya 300 kuanzia Januari hadi Juni 2023 zaidi vinatazama watoto na wanawake.Wakati huo huo,maelfu ya raia wanaendelea kupinga kuvunjika kwa usalama wa nchi ya Haiti.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Taifa la Haiti  huko Carribbean linazidi kushikwa na hali ya ukosefu wa usalama na ghasia. Kwa njia hiyo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limetoa tahadhari kuhusu ongezeko la utekaji nyara wa wanawake na watoto. Kesi 300 zimethibitishwa katika miezi sita ya kwanza ya 2023, karibu mara mbili ya jumla ya mwaka 2022 na mara tatu ya 2021. Kulingana na UNICEF, katika hali nyingi watoto na wanawake wanachukuliwa kwa nguvu na vikundi vyenye silaha kwa faida ya kifedha au faida ya kimbinu. Waathiriwa ambao wanaweza kurudi nyumbani wanapaswa kukabiliana na makovu ya kina ya kimwili na ya kisaikolojia ambayo yanaweza kudumu kwa miaka mingi.

Kuna ongezeko la ghasi,uporaji na vizuizi vya barabani 

UNICEF pia inaripoti kuwa mifumo ya afya mahalia iko kwenye hatihati ya kuporomoka na shule zinakabiliwa na mashambulizi. Kuongezeka kwa ghasia, uporaji, vizuizi vya barabarani na kuwepo kwa makundi yenye silaha kunapunguza kwa kiasi kikubwa juhudi za msaada wa kibinadamu, na kufanya kuwa  kazi vigumu kusambaza misaada inayohitajika kwa jamii zilizoathirika. Kadiri miezi inavyosonga, hofu inaongezeka na hii inaelemea hasa mazingira ambayo tayari ni magumu kwa wale wanaotoa misaada ya kuokoa maisha. Umoja wa Mataifa unaelezea hali hiyo kwa ujumla kama janga. Hadi sasa, inakadiriwa watu milioni 5.2, karibu nusu ya wakazi wote wa nchi ya Caribbean, wanahitaji msaada wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na karibu watoto milioni tatu.

UNICEF inatoa wito kuachiliwa kwa usalama watu wote waliotekwa nyara

Historia tunazosikia kutoka kwa wafanyakazi wenzetu wa UNICEF na wabia katika uwanja huo ni za kushtua na hazikubaliki. Ongezeko la utekaji nyara na utekaji nyara unatia wasiwasi sana, unatishia watu wa Haiti na wale walioko kuwasaidia...nimeona ustahimilivu wa ajabu wa watoto, wanawake na familia za Haiti wanakabiliwa na changamoto zinazoonekana kuwa ngumu, kukataa kukata tamaa, hata hivyo, ujasiri wao unakuja dhidi ya ugaidi unaokua na usiofikirika. Hili lazima likome sasa,” alisema Gary Conille, Mkurugenzi wa UNICEF wa Kanda ya Amerika ya Kusini na Karibiani, katika taarifa yake. Kwa kuzingatia ukweli huu, UNICEF imetoa wito wa dharura wa kuachiliwa mara moja na kurejea salama wale wote waliotekwa nyara nchini Haiti. Hali mbaya ya usalama pia ikawa kiini cha maandamano ya mitaani kwa mfano tarehe 6 Agosti katika mji mkuu wa Haiti wa Port-au-Prince, ambapo maelfu ya watu waliandamana kudai ulinzi dhidi ya magenge yenye silaha ambayo yana hasira bila kupingwa.

watu 73,500 walimbia Haiti kwa mwaka 2022

Ghasia za magenge zimezidisha hali ya maskini na nchi hiyo inasubiri uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu uwezekano wa kutumwa kwa jeshi la kimataifa. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi linasema takriban watu 73,500 walikimbia Haiti mwaka 2022 kutokana na kuongezeka kwa ghasia na umaskini. Licha ya changamoto hizi kubwa, UNICEF inaendelea kukabiliana na mzozo huo, ikitoa msaada muhimu kwa watoto na wahasiriwa ambao wamenusurika na utekaji nyara huu. Shirika la Umoja wa Mataifa linafanya kazi pamoja na washirika wengine, kutoa usaidizi wa kuokoa maisha, kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matibabu, usaidizi wa kisaikolojia na maeneo salama ambapo watoto wanaweza kuanza mchakato wa uponyaji na kupona.

Haiti iko katika hali mbaya kijamii na kiuchumi
09 August 2023, 14:22