Tafuta

Viongozi wa Afika walioko Urussi Viongozi wa Afika walioko Urussi 

Viongozi wa Afrika wako Moscow na ajenda ya ushirikiano wa uchumi na ubinadamu

Rais Putin anatafuta washirika wapya na wakati huo huo alishutumu nchi za Magharibi kwa kutumia shinikizo kubwa kujaribu kukatisha tamaa mataifa ya Afrika kuhudhuria mkutano huo.Lakini ni Viongozi 17 na maafisa wakuu 32 wapo katika mkutano wa siku mbili unaofunguliwa tarehe 27 Julai 2023.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Baadhi ya viongozi wa Afrika waliwasili nchini Urussi kwa ajili ya mkutano wa siku mbili uliofunguliwa Alhamisi 27-28  Julai 2023 mjini Mtakatifu Petersburg kwa kuongozwa na mada ya: "Uchumi na Ubinadamu". Rais Vladimir Putin, akitafuta washirika zaidi, aliwasilisha mkutano huo kama tukio muhimu ambalo litasaidia kuimarisha uhusiano na bara la watu bilioni 1.3, linalozidi kuwa muhimu katika eneo la kimataifa. Rais wa Urussi tayari alikutana kando ya tukio hilo  na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, na kutangaza kwamba Moscow itaongeza mara tatu idadi ya wanafunzi wa Ethiopia watakaosoma na itagharamia gharama za masomo yao. Siku ya Jumatano, tarehe 26 Julai 2023, Rais  Putin pia alikuwa na mazungumzo na Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi.

Nchi za Afrika kuwa na kipingamizi cha kura katika UN

Ikumbumkwe Mataifa 54 ya Afrika yanaunda kipingamizi kikubwa zaidi cha upigaji kura katika Umoja wa Mataifa  zaidi ya kanda nyingine yoyote duniani, yamegawanyika linapokuja suala la upigaji kura wa maazimio kadhaa ya Baraza Kuu yanayoikosoa Urussi kwa hatua yake nchini Ukraine. Kwa hiyo Mkutano huo unafuatia Urussi kujiondoa katika makubaliano yaliyoruhusu mauzo ya nafaka kutoka Bahari Nyeusi, ambayo ni muhimu kwa nchi nyingi za Afrika. Akipuuza lawama za kimataifa na wasiwasi kuhusu tishio jipya kwa usalama wa chakula, unaochochewa na mashambulizi ya makombora ya Urussi kwenye bandari za Ukraine na vituo vya kilimo, Rais Putin amerudia mara kwa mara kuzihakikishia nchi za Kiafrika za kipato cha chini, akiziahidi nafaka za bure za Kirussi.

Rais Puttin akihutubia viongozi
Rais Puttin akihutubia viongozi

“Nataka kuhakikisha kuwa nchi yetu ina uwezo wa kuchukua nafasi ya nafaka ya Ukraine kwa misingi ya kibiashara na bure,” alisema Putin katika taarifa yake ya Jumatatu 24  Julai 2023 na kwamba  Urussi ilisafirisha karibu tani milioni 10 za nafaka barani Afrika katika nusu ya kwanza ya mwaka. Kando na ngano, suala jingine ambalo linaweza kuzingatiwa katika ajenda ya mazungumzo hayo ni hatima ya kampuni ya kijeshi ya Wagner ya Urusi inayoongozwa na Yevgeny Prigozhin, baada ya uasi wake wa muda mfupi huko Urussi mnamo  mwezi Juni iliyopita. Mustakabali wa wanamgambo hao utakuwa suala la dharura kwa nchi kama Sudan, Mali na nyinginezo ambazo zimeingia mkataba na kundi la mamluki kwa kubadilishana na kunyonya maliasili. Maafisa wa Urussi na Prigozhin walisema kampuni hiyo itaendelea kufanya kazi barani Afrika.

Shinikizo la Magharibi

Huu ni mkutano wa pili kati ya Urussi na Afrika tangu 2019, lakini idadi ya wakuu wa nchi waliohudhuria imepungua kutoka 43 hadi kufikia 17 leo hii  kutokana na kile ambacho Urussi ilikitaja kuwa shinikizo kubwa la Magharibi la kuyakatisha tamaa mataifa ya Afrika kuhudhuria. Msemaji wa Urussi Bwana  Dmitry Peskov alielezea kuwa ni “uingiliaji kati usiokubalika na wa wazi wa Marekani, Ufaransa na mataifa mengine kupitia ujumbe wao wa kidiplomasia katika nchi za Afrika, na majaribio ya kuweka shinikizo kwa uongozi wa nchi hizi kuzuia ushiriki wao kikamilifu kwenye jukwaa. “Ni ya kuchukiza kabisa, lakini haitazuia kwa vyovyote mafanikio ya mkutano huo,” Peskov alisema kwenye simu ya mkutano na waandishi wa habari. Na Mshauri wa mambo ya nje wa Putin Yuri Ushakov alisema wakati wakuu wa nchi 17 pekee watahudhuria mkutano huo, nchi nyingine 32 za Afrika zitawakilishwa na maafisa wakuu wa serikali au mabalozi.

Wachambuzi:Afrika inatakiwa kuwa makini zaidi

Kwa upande wa wachambuzi wanasema kwamba "majaribio ya Urussi ya hivi karibuni ya kuimarisha mahusiano na mataifa za Afrika yanaonekana kuwa na maslahi ya kisiasa zaidi." Na kwamba " hii ni tofauti na huko nyuma ambapo ushirikiano wa Moscow na bara hilo la kiafrika kwa kiasi kikubwa uliegemea itikadi zilizofungamana na ukoloni wa Magharibi na ubeberu. Katika enzi ya baada ya ukoloni, Urussi imeonekana kushirikiana na bara la Afrika kwenye nyanja za kiuchumi zaidi, ingawa hata hivyo kumekuwepo na hatua kidogo zilizofikiwa". Lakini mtaalamu kutoka kituo cha mahusiano ya kimataifa kilichoko Abuja, nchini Nigeria Ovigwe Eguegu yeye alisema kuwa msukumo wa sasa wa Moscow katika kuimarisha uhusiano barani Afrika unachochewa na siasa. 

Bensah: Mataifa ya Kiafrika lazima yawe na mikakati

Na Mchambuzi mwingine kutoka kituo cha mahusiano ya Afrika kilichopo Accra, nchini Ghana Emmanuel Bensah alisema kuwa "mataifa ya Afrika yanatakiwa kuwa na mikakati".  Na zaidi "wanatakiwa kuwa makini sana wanapoamua kushirikiana na Urussi." Kwa upande wa mchambuzi wa masuala ya siasa wa huko Luanda, nchini Angola Olivio N'kilimbu alisema suala kuuwa: “hapa ni uaminifu wa mataifa ya bara hilo kwa Urussi na hasa kutokana na msaada wake wakati wa mapambano ya uhuru barani Afrika”.  Kwa upande anaona kuwa: “ziko fikra bado kwamba mataifa ya Afrika bado yana deni kubwa, kwa kuwa Urussi iliyasaidia kwenye harakati zao za ukombozi na sasa Afrika haina ubavu wa kusema chochote juu ya uvamizi wake nchini Ukraine.” Wachambuzi kwa wastani ni wengi sana wa masuala ya kisiasa.

Mkutano huko Mtakatifu Peterburg Urussi kwa fiongzo wa Afrika na Urussi
Mkutano huko Mtakatifu Peterburg Urussi kwa fiongzo wa Afrika na Urussi

Kimsingi mataifa barani Afrika iwapo watasikiliza maonyo kadhaa ambayo wamekwisha pewa ya kuwa makini na masharti ya misaada ambayo hisiwafunge au kuwaongiza katika hatari za walio wanyonge. Mungu ibariki Afrika, Mungu wabariki viongozi wetu na pia Dunia nzima.

27 July 2023, 10:54