Tafuta

Katika kuelekea Siku ya Kiswahili Duniani tarehe 7 Julai ya kila mwaka,Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni linaenzi siku hii. Katika kuelekea Siku ya Kiswahili Duniani tarehe 7 Julai ya kila mwaka,Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni linaenzi siku hii. 

UNESCO:Kiswahili ni daraja baina ya Afrika na Dunia

Kiswahili ni lugha ya umoja na mawasiliano kwa watu wengi sana barani Afrika na nje ya Afrika lakini tunataka kuonesha kwa jinsi gani Kiswahili kilivyo na uwezekano mkubwa katika zama za kidijitali,alisema hayo Afisa Uhusiano wa UNESCO akiojiana na Mwandishi wa Habari wa Umoja wa mataifa kuelekea kilele cha Siku ya Kiswahili Julai 7.

Na Angella Rwezaula,-  Vatican.

Maadhimisho ya II ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani yatakayofanyika tarehe 7 Julai 2023, yameanza kuandaliwa katika kila kona ili kuhamasisha siku hiyo ambayo imepewa uzito mkubwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO), lakini pia kutumika kama Jukwaa la kuziunganisha jamii ambazo sio kwa Afrika tu, zinazozungumza Kiswahili, bali na nyinginezo zinazokumbatia kiswahili. Haya yameelezwa na Estelle Zadra, Afisa Uhusiano wa ofisi ya UNESCO akihojiana na Flora Nducha, Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani tarehe 26 Juni 2023.

Mijadala ya kilele cha Siku ya Kiswahili kutoka , Paris, Dar Es Salaamu hadi Nairobi

Katika mahojiano hayo, Bi Zadra kwa kuenzi kilele cha siku hiyo alieleza kwamba “kuna mambo mengi yatakayojiri katika siku hiyo, kuanzia hapa New York hadi Paris, Dar es salaam hadi Nairobi na katika miji mbalimbali ya Afrika tutakuwa na mijadala na matukio ya kitamaduni ili kuwafanya washiriki kuwa sehemu ya lugha hii iliyosheheni ya Kiswahili. Mbali ya matukio ya kijamii kama mazungumzo na mijadala tutakuwa na hafla mbalimbali za kitamaduni, kama dansi, muziki na hata chakula cha kiutamaduni.”

Jamii zetu sasa zimeunganishwa sana kidijitali

Mwandishi Flora Nducha akitaka kufahamu Kauli mbiu ya mwaka huu 2023 na kwa nini wamechagua hayo Bi  Estelle alifafanua kuwa: “Kiswahili ni lugha ya umoja na mawasiliano kwa watu wengi sana barani Afrika na nje ya Afrika lakini tunataka kuonesha kwa jinsi gani Kiswahili kilivyo na uwezekano mkubwa katika zama za kidijitali, hivi sasa jamii zetu zimeunganishwa sana na ni muhimu kila mtu kuwa na fursa ya nyenzo hizo na tunazihitaji kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na mijadala katika jamii zetu na kila mtu kushiriko hivyo maudhui ya mwaka huu  ambayo ni: “Kuibua uwezo wa Kiswahili katika zama za kidijitali kwa sababu tunauhakika kwamba Kiswahili kinaweza kutumika kama daraja kuunganisha jamii mbalimbali na kuwezesha ujumuishwaji katika ulimwengu wa kidijitali.” Alisisitiza.

Lengo kuu kuwafikia vijana wajasiliamali katika matumizi ya kidijitali

Na ili kuhakikisha maudhui haya yanatimia Mwakilishi wa UNESCO alisema wanashirikiana kwa karibu na nchi zote za Afrika Mashariki na za Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa afrika (SADC)  ambazo pia zimekikumbatia Kiswahili lakini pia amesema lengo kuu ni kuwafikia vijana hususan wajasiriamali ambao wana hamu ya kutumia nyenzo za kidijitali kujiendeleza na lugha kwao ni Kiswahili. Nahatimaye  Mhusika  wa ofisi hiyo alithibitisha kuwa   ujumbe wa UNESCO kwa dunia kuhusu siku hiyo ni kwamba,  “Kiswahili sio lugha tu bali ni mkusanyiko mahiri wa urithi uliosheheni wa kitamaduni wa Afrika Mashariki na tunadhani kwa kukumbatia Kiswahili katika zama za kidijitali tunatoa fursa ya kubadilishana utamaduni, kuchagiza ukuaji wa uchumi na uwezeshaji wa kielimu.” 

Kiswahili kina nafasi kubwa katika mawasiliano

Ikumbukwe Siku ya lugha ya kiswahili duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo  tareje 7 Julai tangu ilipopitishwa rasmi na UNESCO miaka mwili iliyopita 2022 ambapo katika afla hiyo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, yaliyoandaliwa kwa pamoja na ujumbe wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa AFrika, SADC, Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC na wadau wengine kutoka nchi zinazozungumza Kiswahili. Kuzungumza Kiswahili ni kurahisisha mawasiliano na kuunganisha watu wa mbalimbali. Kiswahili ni kielelezo cha kipekee cha desturi na utamaduni wa kiafrika na  ustaarabu pamoja na fikra za watu.  Kiswahili kina nafasi kubwa katika mawasiliano, sayansi na teknolojia kwa sababu kinawezesha kupata habari, elimu, mawazo mapya pamoja na kumiliki sayansi na teknolojia. Kwa njia. Baraza Kuu la UNESCO lilipitisha mwezi Novemba mwaka 2021 bila kupingwa azimio la kutangaza tarehe 7 Julai kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.

Radio za kimataifa ikiwemo Radio Vatican kuna idhaa ya kiswahili

Katika miaka mingi, kuanzia 1960 mashirika ya kimataifa yamekuwa katuma watu wake katika nchi ya Tanzania na Kenya kujifunza lugha ya Kiswahili, na wakati huo huo, kwenye mataifa mbali mbali, vyuo vikuu vimeanza kuweka hata kozi za lugha ya Kiswahili kwa mfano Ulaya na Marekani na kuwatuma wanafunzi wao ili kuwa na uzoefu zaidi kwa nchi husika kujifunza Lugha kwa ufasaha. Radio mbali mbali mbali za Kimataifa kama vile  Radio  VATICAN,  BBC, DW, VOA RADIO UFARANSA, JAPAN, CHINA, RADIO YA UMOJA WA MATAIFA,  SAUTI YA JAMHURI YA KIISLAMU IRAN, na nyingine zina idhaa ya kiswahili!

Ubalozi wa Tanzania nchini Italia unaendesha kozi ya Kiswahili tangu 2022

Kwa kukomaa kwa lugha yoyote ile kwa hiyo ni kutokana na mambo kadhaa hasa yanayojikita kwenye jamii kama vile mashindano ya michezo, mikutano ya kisiasa shughuli za kiuchumi, warsha, Maonesho ya Biashara za kimataifa, makongamano, utume wa kimisionari na mengineyo mengi. Kwa njia hiyo katika kuelekea kilele cha Siku ya II ya Kiswahili duniani, tarehe 7 Julai,  hatuna budi kukuza lugha hii kama lugha nyinginezo duniani ambazo zinapendwa. Kwa mfano katika Ubalozi wa Tanzania nchini Italia umeanzisha tangu 2022 kozi ya lugha ya kiswahili. Toleo lijalo tutakuwa na mengi ya kufahamu kuhusu shule hiyo katika ubalozi wa Tanzania nchini Italia.

tarehe 7 Julai ni Siku ya Kiswahili duniani
01 July 2023, 16:45