Jeshi la Niger limempindua Rais Bazoum na kutangaza kusimamishwa taasisi zote
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Kinachojiri huko Niger ni kwamba kundi la wanajeshi wa Niger limetangaza kumuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum wa nchi hiyo, saa chache baada ya rais huyo kuzuiliwa ikulu na kikosi cha walinzi wa rais kinachoongozwa na Jenerali Omar Tchiani. Katika taarifa iliyosomwa na Kanali Amadou Abdramane kupitia televisheni ya taifa Usiku Jumatano 26 Julai 2023 huku pembeni yake wakiwa na wanajeshi wengine tisa, imeeleza kuwa vikosi vya ulinzi na usalama vimeamua kuuondoa utawala uliopo madarakani kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama, utawala mbovu na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii. Kwa mujibu wa Kanali Abdramane, mipaka ya nchi imefungwa na amri ya kutotoka nje imetangazwa nchi nzima, na huduma katika taasisi zote za umma zimesitishwa, hadi hapo taarifa nyingine itakapotolewa. Wanajeshi hao pia wameonya kuhusu uingiliaji wowote ule wa kigeni. Hata hivyo, kundi la wanajeshi hao linalojiita Baraza la Kitaifa la Kulinda Nchi, limesema liko tayari kufanya mazungumzo na jumuia ya kitaifa na kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bwana Antony Blinken ametoa wito wa kuachiwa mara moja kwa Rais Bazoum. Blinken alisema wanalaani matukio yanayoendelea Niger ya kunyakua madaraka kwa kutumia nguvu, ambayo yanaivuruga katiba ya nchi hiyo, pamoja na kudhoofisha utendaji kazi wa serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Jumatano Blinken alizungumza kwa njia ya simu na Bazoum na kumueleza wazi kwamba Marekani inamuunga mkono kwa dhati kama rais aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Amesema msaada wa Marekani kwa Niger unategemea utawala wa kidemokrasia. Blinken pia amewataka raia wa Marekani kuepuka kwenda kwenye maeneo yaliyoko hatarini nchini Niger.
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ambaye ameonesha uungaji wake mkono kamili pamoja na mshikamano na Rais Bazoum, alilaani matukio yanayoendelea Niger. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, alisema Bwana Guterres alizungumza kwa njia ya simu na Bazoum. "Guterres alilaani vikali juhudi za kunyakua madaraka kwa nguvu na kudhoofisha utawala wa kidemokrasia, amani na utulivu". Amewataka wote wanaohusika "kujizuia na kuhakikisha wanaheshimu na kuilinda katiba. Rais Patrice Talon wa nchi jirani ya Benin, alisema yuko njiani kuelekea Niger kutathmini hali ilivyo, baada ya kukutana Jumatano 26 Julai na Rais wa Nigeria Bola Tinubu, ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS.
Umoja wa Afrika na ECOWAS
Umoja wa Afrika na ECOWAS wameliita tukio hilo "kama jaribio la mapinduzi", na wamewataka waliopanga njama kumuachia huru Rais Bazoum bila masharti yoyote na warejee kwenye kambi zao. Matukio yanayoendelea Niger yamelaaniwa pia na Umoja wa Ulaya, Ufaransa na Benki ya Dunia ambazo zimesema kuwa zinafuatilia kwa karibu hali hiyo ambayo inaleta wasiwasi mkubwa. Taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais ya Niger usiku wa kuamkia alhamisi 27 Julai 2023, imeeleza kuwa Bazoum na familia yake wako salama, bila ya kutoa maelezo zaidi. Bazoum, alichaguliwa mnamo mwaka 2021 kuiongoza nchi hiyo isiyo na utulivu.