Tafuta

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu milioni 117 ambao wameathirika kutokana na baa la njaa duniani na utapiamlo wa kutisha miongoni mwa watoto wadogo. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu milioni 117 ambao wameathirika kutokana na baa la njaa duniani na utapiamlo wa kutisha miongoni mwa watoto wadogo. 

Kuna Watu Milioni 117 Wanaoteseka kwa Utapiamlo Kutokana na Vita na Njaa Duniani

Katika kipindi cha mwaka 2022 watu 376, 400 wameguswa na kutikiswa na baa la njaa nchini Afghanistan, Burkina Faso, Haiti, Nigeria, Somalia, Sudan ya Kusini, Yemen pamoja na nchi zile ambazo migogoro ya kivita imeshika hatamu na hivyo kutishia usalama maendeleo na mafao ya wengi. UN inasema umefika wakati wa kuwekeza katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu kama nyenzo msingi za kupambana na utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vita inaendelea kutishia kuporomoka kwa ukuaji wa uchumi duniani. Mabilioni ya rasilimali fedha iliyokuwa inatumika katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga, maradhi na athari za mabadiliko ya nchi kwa sasa inaelekezwa katika mapambano ya kivita huko nchini Ukraine. Hali hii imepelekea kushuka kwa kiwango cha ubora wa huduma katika sekta ya elimu, afya, mapambano dhidi ya umaskini, ustawi na maendeleo ya jamii. Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine kijeshi kumekuwepo na athari kubwa sana katika medani mbalimbali za maisha ya watu katika Jumuiya ya Kimataifa. Kumekuwepo na athari za kiuchumi, ambako kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta kumepelekea mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma. Tatizo kubwa zaidi kiuchumi ni kwamba, sasa nchi nyingi zinalazimika kutumia fedha nyingi zaidi za kigeni kuagiza nishati ya mafuta kuliko kawaida na hili huathiri akiba ya fedha za kigeni ya nchi nyingi na hivyo kupunguza matumizi ya fedha ambazo zingetumika kwenye mambo mengine muhimu.

Vita ni chanzo kikuu cha umaskini, njaa na magonjwa
Vita ni chanzo kikuu cha umaskini, njaa na magonjwa

Urusi na Ukraine ni wazalishaji na wasambazaji wakuu wa ngano na mazao mengine ya nafaka duniani. Vita hii imesababisha bei ya chakula kuongezeka maradufu katika soko la Kimataifa. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu milioni 117 ambao wameathirika kutokana na baa la njaa duniani na utapiamlo wa kutisha miongoni mwa watoto wadogo. Hayo yamesemwa na “Action Against Hunger, Azione Contro la Fame, AcF” ambalo kimsingi ni Shirika la Kimataifa la kibinadamu linalojikita katika harakati za kuondoa sababu za kimuundo na matokeo ya baa la njaa na utapiamlo wa watoto ulimwenguni kote! Huu ndio ukweli unaojionesha nchini Siria ambayo kwa takribani miaka kumi na miwili inapigana vita ya wenyewe kwa wenyewe! Watu milioni 117 wanaosiginwa kwa baa ya njaa duniani ni wale wanaotoka katika maeneo ya vita na kinzani za kijamii. Kila mwaka watoto zaidi ya milioni mbili wanapoteza maisha kwa sababu ya utapiamlo wa kutisha.

Watu milioni 117 wanakabiliwa na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha
Watu milioni 117 wanakabiliwa na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha

Umoja wa Mataifa unasema, ni kinyume cha Sheria za Kimataifa kutumia baa la njaa kama silaha ya kivita. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna uhusiano wa karibu kati ya vita na baa la njaa duniani. Katika kipindi cha mwaka 2022 watu 376, 400 wameguswa na kutikiswa na baa la njaa nchini Afghanistan, Burkina Faso, Haiti, Nigeria, Somalia, Sudan ya Kusini, Yemen pamoja na nchi zile ambazo migogoro ya kivita imeshika hatamu na hivyo kutishia usalama maendeleo na mafao ya wengi. Umoja wa Mataifa unasema, umefika wakati wa kuwekeza katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu kama nyenzo msingi za kupambana na utamaduni wa kifo unaowatumbukiza watu wa Mataifa kwa njia ya vita, migogoro na kinzani za kijamii.

Baa la Njaa na Vita
08 June 2023, 11:07