Tafuta

WHO yasemaUVIKO-19 si tena dharura ya afya ya kimataifa. WHO yasemaUVIKO-19 si tena dharura ya afya ya kimataifa. 

WHO: Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 si Tena Dharura ya Afya Kimataifa

Shirika la Afya Duniani (WHO), hivi karibuni limetangaza kwamba Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 si tena dharura ya afya ya kimataifa. Takwimu rasmi zinaonesha kwamba, watu milioni 7 walifariki dunia kutokana na UVIKO-19, lakini idadi ya kweli inaweza kufikia vifo vya watu milioni 20 na kwamba, Virusi vya Korona vinabakia kuwa ni tishio kubwa Kimataifa. Kwa sasa Jumuiya ya Kimataifa ina teknolojia na vifaa tiba kupambana na magonjwa ya mlipuko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hivi karibuni ametangaza kwamba Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 si tena dharura ya afya ya kimataifa. Takwimu rasmi zinaonesha kwamba, watu milioni 7 walifariki dunia kutokana na UVIKO-19, lakini idadi ya kweli inaweza kufikia vifo vya watu milioni 20 na kwamba, Virusi vya Korona vinabakia kuwa ni tishio kubwa Kimataifa.  WHO imeonya kwamba, uamuzi wa kuondoa tahadhari ya hali ya juu haimaanishi kwamba hatari imeisha na kusema hali ya dharura inaweza kurejeshwa ikiwa hali itabadilika tena. Kwa sasa Jumuiya ya Kimataifa ina teknolojia na vifaa tiba, fursa ya kujiandaa vyema zaidi kupambana na magonjwa ya dharura. Kumbe, mifumo iliyoundwa kupambana na maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 inapaswa kubaki, ili kukabiliana na dharura endapo itajitokeza tena. Janga la UVIKO-19 lilitangazwa na WHO kuwa ni dharura ya afya ya umma Kimataifa tarehe 30 Januari 2020.

UVIKO-19 si tena dharura ya afya kimataifa
UVIKO-19 si tena dharura ya afya kimataifa

Kwa upande wake, Dk. Mike Ryan, kutoka Mpango wa Dharura wa Afya wa Shirika la Afya Duniani, WHO, alisema dharura hiyo inaweza kuwa imeisha, lakini tishio bado lipo. Ilikuwa ni tarehe 31 Desemba 2019 dalili za kwanza zilipoanza kujitokeza mjini Wuhan, nchini China. Nchi zilizoathirika sana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni pamoja na Italia, Hispania na Uingereza. Desemba 2020 kampeni ya chanjo ikaanzishwa, huku ikikabiliana na upinzani mkubwa wa “NO VAX” Kipindi cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kitakumbukwa na wengi kwa kuacha kumbukumbu za maafa makubwa, huku mamilioni ya watu wakitumbukizwa katika umaskini. Inakadiriwa kwamba, zaidi ya watoto bilioni 1.5 walisitisha masomo yao kutokana na UVIKO-19. Kuna watoto milioni 10 na nusu wamewapoteza wazazi wao kutokana na UVIKO-19 na watoto wengi wameteseka sana kutokana na UVIKO-19.

WHO UVIKO-19

 

 

09 May 2023, 14:11