Kenya: Viongozi wa kidini wameomba amani kufuatia na matokeo ya uchaguzi
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Viongozi wa dini nchini Kenya wametoa wito ili kuwepo amani na utulivu kutokana na uwepo wa mvutano mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais uliomalizika hivi karibuni ambao ulifanyika tarehe 9 Agosti. Mnamo Jumatatu 15 Agosti 2022 mara baada ya siku kadhaa za kura kugawanywa, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC), Wafula Chebukati, alimtangaza Naibu Rais, William Ruto, kuwa rais wa tano wa Kenya katika kinyang'anyiro kikali cha urais dhidi mpinzani mkuu, Bwana Raila Odinga.
Bwana Ruto alishinda kwa tofauti ndogo ya ushindi, akiwa na zaidi ya kura milioni saba, huku Odinga akipata chini kidogo ya milioni saba. Ruto alipata asilimia 50.49% ya kura, huku Odinga akipata asilimia 48.85%, kulingana na IEBC. Machafuko yalitokea kabla ya kutangazwa tu kwa matokeo, huku kukiwa na mizozo na madai ya kuibwa kwa kura katika kambi ya Bwana Odinga. Wajumbe wanne kati ya saba wa tume ya uchaguzi walijitenga na matokeo ambayo yangetangazwa, huku wakisema kwamba jinsi kura zilivyoshughulikiwa hazieleweki. Waangalizi wengi wanashuku kuwa matokeo ya uchaguzi yanaweza kuwa kivuli cha changamoto la mahakama.
Katika kikao na wanahabari baada ya Ruto kutangazwa kuwa rais mteule, viongozi wa dini waliomba amani nchini Kenya. Askofu Mkuu Anthony Muheria wa Nyeri aliwaalika viongozi wote wa kidini na waamini wote kusali na kuiweka nchi mikononi mwa Mungu, huku akiwatia moyo wa kupeana zawadi kuu ya amani. "Mpendwa Mkenya, tunza amani. Amani iwe kwenu. Viongozi wote hawa, tunawatumia amani. Katika majeraha yenu tuwapa amani", alisema Askofu Aidha Askofu Mkuu pia alihutubia kwa wagombea wawili wakuu wa nafasi ya kwanza ya nchi, huku akitoa amani kwa rais mteule na kumtaka awape amani wao na wapinzani wake. Askofu Mkuu Muheri alitoa pia amani kwa Bwana Odinga, huku akimwomba apokee amani hiyo katika moyo wake na kuirejesha kwa taifa zima.
Hali kadhalika, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kenya, Askofu Mkuu Martin Kivuva, alikaribisha amani iliyoashiria kipindi cha kabla na wakati wa upigaji kura, pamoja na siku za kutangazwa kwa matokeo ya mwisho. Hata hivyo, alikiri “maumivu ambayo mtu angepitia ikiwa wangetazamia jambo tofauti,” kwa kuzingatia matokeo na akasali kwa ajili ya utulivu na amani. Katika hali kama hiyo, na mkuu wa Kanisa la Kianglikani la Kenya (ACK), Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit, aliwaalika wale ambao hawakuridhishwa na mchakato wa uchaguzi kutafuta njia za kisheria kupitia mchakato wa kawaida na sio kupitia mkatisho kwa sababu hiyo itaharibu Kenya ambayo sote tunataka kuijenga.” Pia alimweleza rais mteule, akimtaka “kukumbatia kila mtu, wale waliomchagua na wale ambao hawakumchagua, kwa sababu Kenya ni yao wote.
“Tunataka pia kuhimiza kwamba nchi nzima iwekwe pamoja ili tuweze kuwa taifa ambalo litaendelea kustawi,” alisema Askofu Mkuu Ole Sapit. Askofu Mkuu wa Kianglikani alisema: “Kumbuka kwamba unajihesabu kuwa mshindi tunapodumisha amani kwa sababu ni kwa amani ndipo tunaweza kukua na kustawi pamoja. Mungu ibariki Kenya.”