Tafuta

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amefanya ziara katika Bohari ya Dawa (MSD) na kuagiza watu wote wanaohusishwa na tuhuma za ubadhirifu zilizotolewa na CAG wahukuliwe hatua kisheria. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amefanya ziara katika Bohari ya Dawa (MSD) na kuagiza watu wote wanaohusishwa na tuhuma za ubadhirifu zilizotolewa na CAG wahukuliwe hatua kisheria. 

Bohari ya Dawa Kufumuliwa Upya, Watuhumiwa Wa CAG Kuwajibishwa!

Serikali imeagiza wote waliohusishwa na tuhuma za ubadhirifu zilizoainishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wachukuliwe hatua. Mheshimiwa Majaliwa amesema hoja zote zilizotolewa katika ripoti ya CAG lazima zifanyiwe kazi na tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) imeanza kufanyia kazi hoja zote zilizotolewa kuhusu MSD.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, Dar – Es Salaam.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amefanya ziara katika Bohari ya Dawa (MSD) na kuagiza watu wote waliohusishwa na tuhuma za ubadhirifu zilizoainishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wachukuliwe hatua. Mheshimiwa Majaliwa amesema hoja zote zilizotolewa katika ripoti ya CAG lazima zifanyiwe kazi na tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) imeanza kufanyia kazi hoja zote zilizotolewa kuhusu MSD. Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Jumatatu, Mei 09, 2022) wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa MSD baada ya kutembelea viwanda vya kutengeneza barakoa na dawa vilivyopo katika eneo la MSD, Keko jijini Dar Es Salaam. Akizungumzia kuhusu baadhi ya hoja za CAG, Waziri Mkuu amesema MSD ilifanya ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tisa (9) bila ya mikataba halali jambo ambalo si sahihi. Pia, Waziri Mkuu amesema taasisi hiyo ilifanya malipo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.52 kwa wazabuni sita (6) bila ya kufuata utarabu na wala kuitaarifu Bodi ya Zabuni ya MSD. Waziri Mkuu amesema MSD ilifanya zabuni 23 zenye thamani ya shilingi bilioni 8.55 zilifanywa nje ya Mfumo wa Ununuzi wa TANeps unaosimamiwa na PPRA kinyume na matakwa ya sheria ya ununuzi. “MSD ilifanya malipo ya awali kiasi cha shilingi bilioni 14.89 kwa wazabuni watano (5) bila ya mikataba yoyote au makubaliano mengine ambayo yanabainisha msingi wa malipo ya awali.” Amewataja wazabuni hao kuwa ni Keko Pharmaceutical Industry; Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini; Nakuroi Investment Company Ltd.; Technical Services and General na Wide Spectrum (T) Ltd.

Watuhumiwa wote wa CAG wachukuliwe hatua kisheria
Watuhumiwa wote wa CAG wachukuliwe hatua kisheria

Waziri Mkuu amesema taasisi hiyo iliendesha mchakato wa ununuzi na kutoa mkataba wa kusambaza “Liquid Syrup” wenye thamani ya shilingi milioni 898 bila ya kushirikisha Bodi ya Zabuni ya MSD. Amesema taasisi hiyo ilitumia kiasi cha shilingi milioni 215 kwa ajili ya kugharamia posho ya watumishi watatu waliokwenda China kwenye majadiliano ya kuleta mashine za “dialysis” kwa siku 61. “Watumishi watatu wameenda China kufanya majadiliano kwa nini wasimtumie Balozi wa Tanzania nchini China kufanya shughuli hiyo. Si utaratibu kukaa siku 61 kwa ajili ya majadiliano tena bila ya kuhusisha menejimenti ya taasisi.” Mheshimiwa Majaliwa amesema katika taasisi hiyo kuna udhahifu wa usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi licha ya kuwa wamelipwa. “Lazima mjipange vizuri katika utendaji kazi wenu.” Amesema katika idara ya manunuzi kumebainika kuwepo kwa watumishi ambao si wataalamu, hivyo ameagiza wote 16 ambao si wataalamu waondolewe na kuwekwa watumishi wenye taaluma hiyo. Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa MSD, Mavere Tukai afanye tathmini ya utendaji ndani ya MSD na achukue hatua pale atakapobaini kuwepo na dosari. “Ni muhimu kuimarisha eneo la ufuatiliaji.”

Kwa upande wake, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhakikisha Watanzania wanaendelea kupata dawa. “Dawa ni maisha, dawa ni siasa na dawa ni biashara kwa sababu inagusa maslahi ya watu wote, hivyo tutaendelea kutekeleza maelekezo yote ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha dawa zinapatikana.” Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa MSD, Mavere Tukai alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kuwepo na usiri wa bei za bidhaa za afya zinazoamuliwa na wasambazaji walioingia mikataba za wazalishaji. Pia, changamoto nyingine aliyoitaja ni kutokuwepo kwa mfumo wa kupata taarifa za uhakika na uchambuzi wa kina wa masoko ya bidhaa bora na za bei nafuu pamoja na kuwepo kwa udhaifu katika kitengo cha manunuzi. Alisema tayari taasisi imeweka mikakati ya kutatua changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kukijengea uwezo kitengo cha manunuzi, kubadilisha mfumo mzima wa ununuzi kuanzia wazalishaji, intelijensia na tafiti za bei na masoko na mahusiano na washitiri. Mkakati mwingine alioutaja ni kupitia upya muundo wa MSD pamoja na rasilimali watu kwa sababu tayari muundo ulioko sasa umeonesha changamoto hivyo ni lazima ufumuliwe.

Nidhamu, uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha ya umma ni muhimu sana.
Nidhamu, uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha ya umma ni muhimu sana.

Na Habari zaidi kutoka Jijini Mwanza zinabainisha kwamba, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kukamatwa kwa pasi za kusafiria za wataalamu wa Kampuni ya GAS Entec ya Korea Kusini wanaojenga meli ya MV Hapa Kazi Tu jijini Mwanza hadi wakamilishe kazi yao. Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Jumamosi, Mei 7, 2022 wakati akizungumza na wananchi na viongozi wa mkoa huo mara baada ya kukagua ujenzi wa meli hiyo katika eneo la Mwanza South, Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza. "Nimemwagiza Afisa Uhamiaji wa Mkoa akamate pasi zao mara moja na ahakikishe hakuna mtu anatoka nje ya mkoa huu hadi hii kazi ikamilike. Nimeambiwa wako saba, lakini hapa wako watatu. Watafuteni hao wengine wako wapi.” Wenye pasi hizo ni Mkurugenzi wa GAS Entek, Bw. Dong Myung Kwak, na wasaidizi wake Bw. Kyunghan Choi na Bw. Kyuh Yun Kwak ambaye ni mtoto wa Mkurugenzi huyo. “Nimeingia ndani kukagua kazi ya ujenzi lakini sijaridhika nayo. Katika maelezo yao nimebaini kuwa kampuni tuliyoingia nayo mkataba ya GAS Entec imeuza “share” zake bila Serikali kuarifiwa. Waliouziwa, walipokuja walishangaa kuona ujenzi wa meli kwa sababu suala la ujenzi liko nje ya mauziano yao." Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Mwanza kwa ziara ya siku moja, amesema Serikali imeshalipa asilimia 80% ya gharama za ujenzi wa meli hiyo lakini kazi iliyofanyika kwa mujibu wa mkataba ni asilimia 65% tu. Amesema taarifa alizonazo zinaonesha kuwa wafanyakazi walikuwa 118 lakini sasa wamebakia 22 tu.

"Haiwezekani tuwalipe hela hiyo, kazi haiendi kama ilivyopaswa. Tena wamepunguza Wafanyakazi kutoka 118 hadi 22, tunajuaje kama kesho watawaondoa hao 22 na wao wenyewe wapande ndege kurudi kwao, au waende Nairobi kupanda ndege." Amesema ameshawasiliana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye ameridhia hatua hiyo. “Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuridhia hatua hii.” “Hawa watu wasiondoke hadi kazi ikamilike na kama wataondoka basi atakayewadhamini ni Balozi wao. Serikali tutaendelea kuwasiliana na Balozi wa Korea Kusini na tunaamini kazi hii itakamilika. Wizara husika simamieni na kuhakikisha kazi inakamilika kwa mujibu wa mkataba.” Waziri Mkuu amesema hakuna mradi wa kimkakati ambao utakwama. “Mheshimiwa Rais ameagiza tusimamie hii miradi, nasi ndiyo maana tuko tuko barabarani kila siku Ninawaomba Watanzania muamini kuwa Serikali yenu iko imara. Na pia niwahakikishie viongozi wa Chama cha Mapinduzi mliopo hapa kwamba Ilani yetu itatekelezwa kwa zaidi ya asilimia 90,” amesema.

Miradi ya Kimkakati haina budi kukamilika kwa wakati.
Miradi ya Kimkakati haina budi kukamilika kwa wakati.

Mapema, Mkurugenzi wa GAS Entek, Bw. Kwak alimweleza Waziri Mkuu kuwa amelazimika kupunguza wafanyakazi kwa sababu ana makontena matatu bandarini ambayo anataraji yataanza kutoka baada ya wiki mbili. Kauli ya Bw. Kwak ilikanushwa na Meneja Mradi ambaye pia ni Mhandisi Mkazi, Lt. Col. Vitus Mapunda kwamba makontena matatu ni sehemu ndogo sana ya kazi iliyobakia na ambayo inatakiwa kuwa imefikiwa. Gharama za ujenzi wa meli hiyo ni dola za Marekani milioni 39 sawa na sh. bilioni 80. Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa baada ya kukagua ujenzi wa Meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu alielekea kwenye eneo la Kigongo Busisi kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la JPM lenye urefu wa kilomita tatu. Akiwa katika eneo hilo ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ikutane na watendaji wa Idara ya Kazi mkoa wa Mwanza ili kuhakikisha watumishi katika mradi huo wanalipwa stahiki zao ipasavyo. Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mbunge wa Sengerema, Bw. Hamisi Tabasamu aliyedai kuwa licha ya mradi huo kuendelea lakini watumishi wamepungua na wanakimbilia katika mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR). "Mkandarasi aimarishe utendaji kazi ili ujenzi wa daraja hili ukamilike. Pia wananchi nawaomba mtoe ushirikiano kwa mkandarasi ili kazi iendelee vizuri." Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi huo Mhandisi Benjamin Michael alisema awali kulikuwa na wafanyakazi 813 na sasa wamebaki 744 baada ya wengine kuacha kazi.

10 May 2022, 10:25