Tafuta

Vijana wako mstari wa mbele kwa maandamano ya kupinga wakati  Mkutano wa COP26 huko Glasgow ukiendelea. Vijana wako mstari wa mbele kwa maandamano ya kupinga wakati Mkutano wa COP26 huko Glasgow ukiendelea. 

COP26:Bado kuna tofauti za kimtazamo kuhusu utekelezwaji wa maamuzi

Baada ya wiki ya kwanza iliyojaa ahadi kubwa kutoka Uingereza ambayo ndiyo mwenyeji wa mkutano huo za kumaliza ukataji misitu na kuzika kwenye kaburi la sahau matumizi ya mkaa wa mawe, wataalam wanasema mkutano wa COP26 haujapiga hatua yoyote muhimu kutatua masuala yaliyopo.

Na Sr. Angella Rwezaula – Vatican.

Mkutano wa kujadili mabadiliko ya tabianchi COP26 uliingia wiki ya mwisho tangu Jumatatu tarehe 8 Novemba 2021, ambapo bado ni siku mbili tu mkutano huo ufungwe japokuwa nchi zikiwa bado zinatofautiana kimtazamo kuhusu masuala tete na ambayo yanakuwa kama kitendawili cha kutegua. Hii ni kutokana na kwamba mambo mengi yenye ugumu ambayo hadi sasa duniani yamekuwa muktadha wa pembeni , hasa suala la utekelezaji wa mabadiliko ya tabianchi na kwenda pole pole katika kutekeleza na kudhibiti ongezeko la joto ulimwenguni ambalo linatesa walio wengi wasio wahusika wakuu kusini mwa ulimwengu. Vile vile ni pamoja na jinsi gani ya kudhibiti hewa ya ukaa na  kusaidia nchi ambazo tayari zinakumbwa na athari za ongezeko la joto duniani.

Kwa njia hiyo baada ya wiki ya kwanza iliyojaa ahadi kubwa tu kutoka Uingereza ambayo ndiyo mwenyeji wa mkutano huo ya kumaliza ukataji misitu na kuacha matumizi ya mkaa wa mawe, wataalam wanasema mkutano wa COP26 haujapiga hatua yoyote muhimu kutatua masuala yaliyopo. Japokuwa ahadi hizo  hata hivyo ni mategemo kwamba yanaweza kuashiria kwamba wanakaribia muafaka, lakini masuala ni mengi  tete ambayo bado hayajapata ufumbuzi. Kwa mfano, Umoja wa Ulaya unataka uwepo mkakati wa hali ya juu  uchukuliwe ili kupunguza utoaji gesi ya ukaa. Nchi za Afrika zinahitaji fedha zaidi kukabiliana na madhara, huku na nchi ya Australia na Japan kwa upande wao zikitaka zaidi kuendelea kutumia mkaa wa mawe.

Wiki hii katika kikao cha serikali hizi zinatafuta namna ya kupata muafaka wa jinsi ya kuzisaidia vile vile nchi ambazo ziko katika hatari ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuzifidia kutokana na athari ambazo tayari zilitokea. Hilo kwa hakika ni zoezi kubwa kuweza kubaini ikiwa nchi tajiri na maskini zinaweza kumaliza mdodoro kuhusu suala la kifedha. Vijana nao hawakosi kusisitiza na kuhamasisha kwa upande wao kwani maisha ya leo na kesho yanawasubiri wao, na hawawezi kukubali kuona viongozi wa ngazi za juu wanakosa kutoa muafaka unaostahili kuokoa sayari inayozidi kuteketea kwa sababu ya mkono wa mwanadamu. Na maandamano makubwa ulimwenguni kuanzia hata huko Scotland limewaona vijana Ijumaa kama kawaida yao wakiandamana kwa kutaka utekelezaji tu wa matendo na sio ahadi bila matendo. Tarehe 12 Novemba mkutano huo unakunja jamvi lake, je kweli muafaka na utekelezaji utakuwapo? Ni macho yetu na masikio kutazama na kusikiliza utekezaji huo.

10 November 2021, 14:28