Tafuta

Wasiwasi wa Shirika la Afya WHO la kutofikia lengo la utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 kwa asilimia 10 barani Afrika ifikapo mwisho mwa Septemba. Wasiwasi wa Shirika la Afya WHO la kutofikia lengo la utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 kwa asilimia 10 barani Afrika ifikapo mwisho mwa Septemba. 

WHO:lengo la kutoa chanjo ya UVIKO-19 kwa 10% barani Afrika litashindwa

WHO imejikita katika utoaji wa ushauri wa sera na miongozo ya kiufundi na msaada kwa nchi za Kiafrika kusaidia kuongeza vifaa pamoja na uwezo wa kupanga na kufuatilia.Pamoja na hayo bara hilo litashindwa kufikia lengo la dharura la ulimwengu katika kutoa chanjo ya UVIKO-19 kwa asilimia 10 ya watu wake kufikia mwishoni mwa Septemba

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi 2 Septemba 2021 mjini Brazzaville nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Cong DRC na shirika la Afya ulimwenguni WHO kanda ya Afrika, imesema kuwa Bara la Afrika litashindwa kufikia lengo la dharura la ulimwengu la kutoa chanjo ya UVIKO-19 kwa asilimia 10 ya watu wake ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba 2021. Kwa mujibu wa takwimu mpya zilizooneshwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) inabainishwa kuwa Mataifa 42 kati ya 54 ya Afrika,  karibu 80% yatashindwa kufikia lengo ikiwa kasi ya sasa ya utoaji wa chanjo haitaongezeka. Mpaka sasa nchi 9 za Afrika ikiwemo Afrika Kusini, Morocco na Tunisia zimeshafikia lengo hilo la ulimwengu lililowekwa mwezi Mei, katika mkutano mkuu wa nchi wanachama wa WHO,  kwa kasi ya sasa inategemewe nchi nyingine 3 huwenda zikafikia lengo ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba 2021. Hata hivyo inawezakana nchi nyingine mbili zitafikia iwapo zitaongeza kasi ya kutoa chanjo kwa wananchi wake.

Kwa mujibu wa Dk. Matshidiso Moeti, Mkurugenzi WHO Kanda wa Afrika amesema kuwa “Zikiwa zimebaki siku chache kufikia mwisho wa mwezi Septemba sasa lengo liangalie Afrika na ulimwenguni kote kwani suala la uhifadhi wa chanjo umeirudisha nyuma Afrika, na tunahitaji chanjo zaidi kwa haraka, lakini kadri dozi nyingi zinavyofika, nchi za Kiafrika lazima zifanye haraka ili kuweza kusonga mbele na mipango sahihi ya kutoa chanjo kwa haraka kwa mamilioni ya watu ambao bado wanakabiliwa na tishio kubwa kutoka kwa UVIKO-19.

Mwezi Agosti, 2021 jumla ya chanjo zilizofikishwa bara la Afrika kupitia mfumo wa utoaji chanjo wa pamoja wa COVAX zilikuwa milioni 21, hili ni ongezeko kubwa ikiwa ni sawa na chanjo zote zilizotolewa katika kipindi cha miezi 4 iliyopita. Chanjo nyingi zaidi zinategemewa kuwasili barani Afrika kutokea mfuko wa COVAX na Umoja wa Afrika kufikia mwishoni mwa Septemba, chanjo za kuweza kutosha kufikia lengo la asilimia 10. Chanjo milioni 143 zimewasili barani Afrika na jumla ya watu waliochanjwa ni milioni 39,  sawa na kusema asilimia 3 ya idadi ya watu wa bara hilo ndio wamepata chanjo tu. Ikilinganishwa na nchini Marekani ambapo asilimia 52 ya watu wake wamepata chanjo, na Bara la ulaya takwimu zikionesha watu aslimia 57% wameshapata chanjo.

Kwa kuongezea amesema Dk Moeti kuwa “Ukosefu huu wa usawa unasumbua sana. Asilimia 2 tu ya dozi zaidi ya bilioni tano zilizotolewa ulimwenguni zimetolewa barani Afrika. Lakini kuongezeka kwa hivi karibuni kwa usafirishaji wa chanjo na ahadi zinazoendelea kutolewa kunaonesha kuwa utoaji chanjo kwa haki zaidi, usambazaji kimataifa wa chanjo unawezekana”. Hata hivyo mkuu huyo wa WHO Afrika amehimiza nchi lazima ziendelee kushughulikia mapungufu ya utendaji na kuendelea kuboresha na kurekebisha kampeni zao za chanjo ya UVIKO-19.  Kati ya nchi 30 ambazo zimewasilisha takwimu zao WHO juu ya utayari wa utendaji kazi wao, ni nchi moja kati ya mbili haijafanya mapitio ya hatua, ambazo ni muhimu kwa kutathmini na kupanga vizuri maendeleo ya utendaji wao. Pia ni nchi mmoja kati ya nchi tatu hawajawasilisha mipango yao ya Kitaifa ya Kusambaza chanjo, ambayo inaonesha  masuala yote ya kampeni ya utoaji chanjo ya UVIKO-19 katika kila nchi.

WHO imejikita katika utoaji wa ushauri wa sera na miongozo ya kiufundi na msaada kwa nchi za Kiafrika kusaidia kuongeza vifaa,pamoja na uwezo wa kupanga na kufuatilia. WHO pia inafanya kazi kushirikisha uzoefu uliopatikana baina ya nchi moja na nyingine. Kwa ujumla wagonjwa wa UVIKO-19 wamepungua kidogo barani Afrika lakini bado wagonjwa wanaendelea kuteseka na janga hilo. Takwimu zinaonesha idadi inayoongezeka ya kesi mpya ni katika Afrika ya Kati, Mashariki na Magharibi ambapo wamefanya idadi kuoneze hadi kukaribia 215 000 katika wiki inayoishia 29 Agosti. Zaidi ya vifo 5500 viliripotiwa katika wiki inayoishia tarehe 29 Agosti.

03 September 2021, 09:57