Tafuta

Chanjo dhidi ya Virusi vya UVIKO-19 wazee wapewa kipaumbele cha kwanza. Chanjo dhidi ya Virusi vya UVIKO-19 wazee wapewa kipaumbele cha kwanza. 

Chanjo Dhidi ya UVIKO-19 Wazee Wapewa Kipaumbele Tanzania!

Wakati huu ambapo Dunia inapambana na maambukizi ya UVIKO-19 makundi mbalimbali yanatakiwa kushiriki kikamilifu kuhakikisha kwamba, yanapamba fika dhidi ya janga hilo. "Kupitia mabaraza ya Wazee, wawahamasishe Wanachama wao kujitokeza kwa hiari kupata chanjo hiyo." Wazee ni kundi ambalo lipo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya UVIKO-19! Amua Sasa!

Na Mwandishi Wetu, Dodoma, Tanzania.

Wazee nchini Tanzania wameshauriwa kutumia fursa ya chanjo dhidi ya ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Korona UVIKO-19 ili kuimarisha kinga ya miili yao kipindi hiki ambacho Serikali imewapa kipaumbele cha kwanza. Wito huo umetolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu wakati akizungumza na Wajumbe wa Chama cha Wanasheria Wanawake Nchini Tanzania, TAWLA waliomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma. Dkt. Jingu amesisitiza kuwa wakati huu ambapo Dunia inapambana na maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 makundi mbalimbali yanatakiwa kushiriki kikamilifu kuhakikisha kwamba, wanapamba fika dhidi ya janga hilo. "Kupitia mabaraza ya Wazee, wawahamasishe Wanachama wao kujitokeza kwa hiari kupata chanjo hiyo" alisema na kuongeza kuwa Wazee ni kundi ambalo lipo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya UVIKO-19 hivyo Jamii ihamasishe Wazee wote kwenda katika vituo vya kutolea chanjo na kupata huduma hiyo amesisitiza Dkt. Jingu.

Ameongeza kuwa Wazee ni tunu ya Taifa hivyo Jamii ina wajibu wa kuwalinda na majanga mbalimbali ikiwemo kuimarisha usalama wa Afya zao. "Uzee na kuzeeka unaambatana na changamoto ya kupungua kwa kinga ya mwili hivyo Serikali inatoa wito kwa Wazee wote nchini kujitokeza kutumia fursa ya chanjo ya UVIKO-19". Aidha, Dkt. Jingu amewataka Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii wote kuhakikisha Wazee wanaokwenda kupata chanjo kwenye vituo katika maeneo yao wanapata huduma zote wanazostahili bila usumbufu wa aina yoyote.  Wakati huo huo, Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na watoa huduma katika sekta ya Afya nchini wameelekezwa kutimiza wajibu wao kitaaluma kwa kuelimisha umma wa Watanzania kuhusu umuhimu wa kupata Chanjo ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ili waweze kufanya maamuzi sahihi. Agizo hilo limetolewa hivi karibuni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis katika mkutano wake na waandishi wa Habari.

Mhe. Mwanaidi amesema miongoni mwa majukumu ya maafisa hao ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii katika masuala mbalimbali ikiwemo suala la chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. "Mtakumbuka kuwa, mnamo tarehe 28 Julai, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alizindua mpango wa chanjo ya UVIKO-19 Kitaifa kwa kuonesha njia na kuchanjwa dhidi ya ugonjwa huo, hivyo nampongeza Rais wetu kwa hatua hiyo muhimu ya kupambana na maambukizi mapya ya UVIKO-19" alisema Naibu Waziri Mwanaidi. Aidha amesisitiza umuhimu wa kuwalinda na kuwaelekeza wazee namna ya kupata chanjo ya UVIKO-19 kutokana na umuhimu wao katika maendeleo ya taifa ndio maana Serikali kwa wamu ya kwanza ya kutoa chanjo imewapa kipaumbele. “Nitumie nafasi hii kuwaagiza Maafisa Ustawi na Maafisa Maendeleo ya Jamii kote nchini kuhakikisha wanawahamasisha wazee kupitia majukwaa mbalimbali yakiwemo mabaraza ya wazee yaliyoko katika maeneo yao, kutumia vyombo vya habari hasa redio za kijamii ili wapate elimu kuhusu namna ya kupata chanjo hiyo katika vituo vilivyopangwa” alisema Mhe. Mwanaidi.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanaidi ametumia nafasi hiyo kuwahimiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa chanjo kwa kuwa kupitia wao, elimu sahihi itawafikia wananchi kwa wakati na kuwa na uzalendo wa kuhamasisha wananchi katika suala hilo la kuchanjwa kwa hiari” alihimiza Mhe. Mwanaidi. Aidha, ameyahimiza Mashirika na Asasi za kiraia zinazotoa huduma kwa wazee kuandaa na kuendesha Programu mbalimbali za kuhamasisha wazee kwenda kupata chanjo ya UVIKO-19 kwa hiari yao ili kuimarisha kinga katika miili yao. Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Shilungu Ndaki amesema kuwa Serikali itahakikisha kundi la wazee linasimamiwa vizuri katika kupata huduma ya chanjo ya UVIKO-19 ili kulilinda kundi hilo ambalo ni muhimu kwa ustawi wa jamii.

Chanjo UVIKO-19
11 August 2021, 14:03