Tafuta

Kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu mlipuko wa moto katika bandari ya Beirut nchini Lebano 4.08.2020-4.0.2021. Kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu mlipuko wa moto katika bandari ya Beirut nchini Lebano 4.08.2020-4.0.2021. 

Baada ya mwaka tangu mlipuko wa Beirut,98% ya familia zinahitaji msaada

Tangu mlipuko wa moto kwa bandari ya Beirut nchini Lebanon,mnamo tarehe 4 Agosti 2020,lakini bado mahitaji ya watoto ni makubwa kwani ni asilimia 98 ya familia ambazo zinahitaji msaada.Taarifa hizo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,UNICEF na kutolewa Jumanne tarehe 3 Agosti 2021 mjini Beirut.

Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Mwaka mmoja tangu kutokea kwa milipuko kwenye mji mkuu Beirut, nchini Lebanon, lakini mahitaji ya watoto na familia zao yamesalia kuwa makubwa yakichochewa zaidi na kuporomoka kwa uchumi, ukosefu wa utulivu wa kisiasa na janga la ugonjwa wa UVIKO -19.  Taarifa hizo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na kutolewa Jumanne tarehe 3 Agosti 2021 mjini Beirut. Tathmini hiyo inaonesha watoto kukumbwa na kiwewe sambamba na mahitaji ya msingi yanayokabili familia zao. Kaya 7 kati ya 10 ziliomba misaada ya msingi tangu tarehe 4 mwezi Agosti 2020 na takribani kaya zote hizo hadi leo zinategemea misaada ya kibinadamu kama vile fedha kwa ajili ya kununua chakula.  Theluthi moja ya familia zenye watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 zimesema angalau mtoto mmoja katika familia alikuwa na dalili za kiwewe na msongo wa mawazo huku kwa watu wazima takribani nusu yao wanakumbwa na hali hiyo.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Lebanon Yukie Mokuo anasema, “mwaka mmoja baada ya tukio lile la kutisha na kusikitisha, maisha ya watoto bado yameathirika. Hicho ndicho wazazi wao wanatueleza. Familia zinahaha kupona baada ya milipuko ile mibaya zaidi kuwahi kutokea tena katikati ya janga la kiuchumi na kiafya.”   Milipuko hiyo ilisambarataisha eneo kubwa la mji wa Beirut na kuua zaidi ya watu 200 wakiwemo watoto huku majeruhi walikuwa zaidi ya 6,500 na wakiwemo watoto 1,000. Kwa kuwa biashara zilisambaratishwa, makumi ya maelfu ya wafanyakazi walipoteza ajira na kuwaacha wakihaha kulisha familia zao na kutibu watoto.  Utafiti huo wa UNICEF unasema familia mbili kati ya tatu sawa na asilimia 68.6 hazijaweza kupata huduma za afya tangu mlipuko kutokea. Utafiti huo unatokana na mahojiano kwa njia ya simu yaliyofanyika mwezi uliopita wa Julai na kuhusisha kaya 1,187. Kwa mantiki hiyo UNICEF inatoa wito wa mambo kadhaa ikiwemo watoto kupatiwa kipaumbele na hazi zao za msingi ziheshimiwe. Pili viongozi wa kisiasa Lebanon wamalize tofauti zao na kuunda serikali ya kuhudumia wananchi. Tatu mamlaka zitambue kuwa kuendeleza huduma za umma kwa muda mfupi na mrefu ni muhimu kwa uhai na maendeleo ya mtoto.

Nembo ya Shirikisho la soka ulimwenguni,FIFA
Nembo ya Shirikisho la soka ulimwenguni,FIFA

Shirikisho la soka ulimwenguni, FIFA limezindua kampeni ya kusaidia kuhamasisha jamii kuhusu dalili za ugonjwa wa afya ya akili ili kuwezesha jamii kutafuta msaada wanaohitaji na kuchukua hatua ya haraka kuwa na afya bora ya akili. Kampeni hiyo imepatiwa jina la kiingereza #ReachOut, ambapo kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO na jumuiya ya nchi za kusini mashariki mwa Asia, ASEA itaongeza uelewa wa watu kuhusu afya ya akili. Akizundua kampeni hiyo Jamatatu tarehe 2 Agosti 2021, Rais wa FIFA Gianni Infantino amesema “kampeni hii ni muhimu sana kuongeza uelewa wa watu kuhusu mazingira au dalili za afya ya akili na hivyo kuibua mjadala ambao unaweza kuokoa maisha. Katika dira ya FIFA ya 2020-2023, tunaahidi azma yetu ya kufanya mpira wa miguu uwe kwa ajili ya jamii na nashukuru wachezaji kama vile Bi. Enke ambaye amechangia sana katika mpango huu muhimu.” Mkuu huyo wa FIFA amesema msongo wa mawazo na kiwewe vinaathiri idadi kubwa ya watu duniani kote na vijana wako hatarini zaidi. Mjadala wa kifamilia, marafiki au wataalam wa afya ni muhimu. “FIFA inajivunia kuzindua kampeni hii ikiungwa mkono na WHO na ASEAN.”

Video hiyo ya kampeni ina wachezaji nguli wa sasa na wa zamani pamoja na wageni maalum ambao wanaonesha kuunga mkono afya ya akili. Kampeni hiyo inapatikana kupitia chaneli za FIFA na imesambazwa kupitia vyombo vya habari na vyama shirika 211 vya FIFA. Kampeni hiyo inatoa fursa kwa watu kusikia manguli wa FIFA kama vile Luis García, Shabani Nonda, Patrizia Panico, Fara Williams na Walter Zenga.  Kupitia wavuti wa FIFA, FIFA.com  wachezaji kama vile Marvin Sordell na Sonny Pike wanaelezea mazingira waliyopitia wakati wana msongo wa mawazo Halikadhalika Terese Enke anajadili machungu aliyopitia baada ya mpenzi wake kujiua.

Takwimu za Msongo wa Mawazo na Vifo

Msongo wa mawazo unaathiri zaidi ya watu milioni 260 duniani kote huku nusu ya visa vya afya ya akili huanza pale mtu ana umri wa miaka 14. Kujiua kunashika nafasi ya 4 kwa sababu ya vifo miongoni mwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 29. Miongoni mwa wacheza mpira wa miguu ambao bado wanacheza, asilimia 23 wameripoti kukosa usingizi, ilihali asilimia 9 wameripoti kukumbwa na msongo wa mawazo na asilimia 7 hukumbwa na kiwewe. Na kwa wachezaji ambao tayari wamestaafu, takwimu ziko juu kwa kuwa asilimia 28 wanahaha kupata usingizi, asilimia 13 wana msongo wa mawazo huku asilimia 11 wana kiwewe. Hali ya watu wenye msongo wa mawazo na kiwewe inazidi kuwa mbaya zaidi hivi sasa wakati wa COVID-19 kwa sababu wanashindwa kupata matibabu, ajira zimepungua, kuna kutengwa na kadha wa kadha. Akizungumzia kampeni hii, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema “kadri COVID-19 inavyoendelea kutikisa, ni muhimu kuliko wakati wowote ule kupatia umuhimu afya ya mwili na akili. WHO ina furaha kubwa kushirikiana na FIFA katika kampeni hii ya #ReachOut na inahamasisha watu kuzungumzia afyaya akili.”

03 August 2021, 14:58