Tafuta

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameshinda kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 ingawa vyama vya upinzani vinasema kulikuwepo na mizengwe kibao! Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameshinda kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 ingawa vyama vya upinzani vinasema kulikuwepo na mizengwe kibao! 

Waziri Mkuu wa Ethiopia Ashinda Kwa Kishindo Uchaguzi Mkuu 2021

Abiy Ahmed, Chama chake cha Prosperity kimeshinda kwa kujipatia viti 410 kati ya viti 436, na hivyo kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 ambao ulicheleweshwa. Waziri mkuu Ahmed, amepata ridhaa ya kuwa madarakni kwa kipindi cha miaka mitano. Hii ilikuwa ni changamoto kubwa ya kuweza kufanya uchaguzi mkuu unaosimikwa katika misingi ya haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Tume ya Uchaguzi Nchini Ethiopia, Jumamosi tarehe 10 Julai 2021 imemtangaza Bwana Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia kuwa Chama chake cha Prosperity kimeshinda kwa kishindo kwa kujipatia viti 410 kati ya viti 436, na hivyo kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 ambao ulicheleweshwa nchini humo. Kutokana na ushindi huu, Waziri mkuu Abiy Ahmed, amepata ridhaa ya kuwa madarakni kwa kipindi cha miaka mitano. Hii ilikuwa ni changamoto kubwa ya kuweza kufanya uchaguzi mkuu unaosimikwa katika misingi ya haki na amani. Tangu Novemba 2020, Ethiopia imekumbwa na machafuko ya kisiasa ambayo yamepelekea watu wengi kupoteza maisha na wengine wengi kutumbukia katika hali ya umaskini, njaa na magonjwa. Uchaguzi huu mkuu ulipaswa kufanyika tarehe 29 Agosti 2020, lakini ukasogezwa mbele kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Itakumbukwa kwamba, Waziri mkuu Abiy aliingia madarakani April 2018 kufuatia maandamano makubwa ya kupinga serikali ya muungano iliyokuwa na viongozi wengi kutoka kundi la “Tigray People's Liberation Front (TPLF) hali iliyotikisa misingi ya usalama, umoja na mshikamano wa Kitaifa nchini Ethiopia. Hata hivyo, vyama vya upinzani nchini Ethiopia vinawalalamikia maafisa wa Serikali waliovuruga maandalizi ya uchaguzi mkuu na matokeo yake, wamepata viti vichache vya wawakilishi. Waziri mkuu Abiy Ahmed anatarajia kuunda Serikali mpya panapo majaliwa mwezi Oktoba 2021 kwa lengo la kuendelea kuimarisha umoja wa Kitaifa na mafungamano ya kijamii ili kuondokana na ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Ethiopia.

Uchaguzi Mkuu
13 July 2021, 14:53