Tafuta

Tarehe 26 Julai 2021 umefunguliwa mkutano wa utangulizi wa Mifumo ya Chakula mjini Roma: Lengo ni kuwa na uhakika na usalama wa chakula duniani. Tarehe 26 Julai 2021 umefunguliwa mkutano wa utangulizi wa Mifumo ya Chakula mjini Roma: Lengo ni kuwa na uhakika na usalama wa chakula duniani. 

Mkutano wa Utangulizi wa Mifumo ya Chakula Roma, Baa la Njaa!

Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limepelekea baa la njaa kuongezeka duniani. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na Mifumo ya Chakula yenye uhakika sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na uhakika na usalama wa chakula kwa watu wote duniani. Baa la njaa ni tishio kwa watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed, Jumatatu tarehe 26 Julai 2021 amefungua mkutano wa utangulizi wa Mifumo ya Chakula mjini Roma, nchini Italia, na kuzishawishi nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba zinaweka mifumo mizuri zaidi ya chakula ili kuhakikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs yanafikiwa mwaka 2030. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limesababisha mipango mingi kukwama na kurejea nyuma. Bei ya mazao ya chakula duniani imeongezeka maradufu kiasi cha kufikia asilimia 33.9% ikilinganishwa na bei ya mwaka 2020. Hiki ni kielelezo cha madhara ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Uwezo wa wananchi wa kawaida kununua chakula bora umepungua na hivyo kuongeza idadi ya maskini duniani pamoja na lishe duni.

Kwa upande wake, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO linabainisha kwamba, kuna hatari kwamba, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu yakashindwa kufikiwa hapo mwaka 2030. Mchakato huu unapania kuboresha mifumo ya chakula duniani, ili iweze kuwa ni endelevu zaidi, bila kuwaacha watu wengine nyuma ya mchakato huu. Kwa upande wake, Professa Mario Draghi, Waziri mkuu wa Italia ambayo ni mwenyeji wa mkutano huu amesema kwamba janga la UVIKO-19 limepelekea idadi ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa kuongezeka maradufu hadi kufikia watu milioni 130 wanaohitaji chakula cha dharura. Kwa jumla watu zaidi ya milioni 800 wanahitaji chakula cha msaada.

Changamoto hii haina budi kuvaliwa njuga na Umoja wa Mataifa sanjari na chanjo ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Janga hili limepelekea baa la njaa kuongezeka duniani. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na Mifumo ya Chakula yenye uhakika sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na uhakika na usalama wa chakula kwa watu wote duniani. Jambo hili litawezekana, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itashikamana kupambana na magonjwa, njaa na ujinga. Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa pamoja na Benki za Maendeleo zinapaswa kuchangia rasilimali fedha ili malengo haya yaweze kufikiwa

Wakati huo huo, Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD umetoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya mabadiliko muhimu katika Mifumo ya Chakula, ili kuhakikisha kwamba, wakulima na wanawake vijijini wanawezeshwa kikamilifu, ili kupata mahitaji yao msingi, ili kuisaidia Jumuiya ya Kimataifa kuwa na Mifumo endelevu ya chakula duniani.

FAO Roma
27 July 2021, 14:38