Tafuta

Italia ni Mabingwa wa Kombe la Ulaya UEFA EURO 2020 Italia ni Mabingwa wa Kombe la Ulaya UEFA EURO 2020 

Italia Mabingwa wa Kombe la UEFA EURO 2020! Yaani Hadi Raha!

Ushindi huu umepokelewa kwa heshima na taadhima baada ya Italia kushinda Kombe la Ulaya kwa mara ya kwanza kunako mwaka 1968, yaani miaka 53 iliyopita! Kwa hakika hili ndilo gumzo la Italia kwa siku hizi! Jumapili tarehe 11 Julai 2021 Italia ikamliza Mwingereza aliyekuwa na matumaini makubwa ya kushinda akiwa anacheza nyumbani kwao! Italia yaichezesha Uingereza vidogoli

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Wachezaji wa Timu ya Soka ya Italia maarufu kama “Gli Azzuri” Jumatatu tarehe 12 Julai 2021wamerejea Roma na kupokelewa kwa shangwe na bashasha. Jumatatu wamekutana na Rais Sergio Mattarella wa Italia pamoja na viongozi wakuu wa Italia, ili kuwapongeza wachezaji hawa baada ya kuwatoa machozi Waingereza kwa kuwachakaza kwa matuta 3-2 kwenye Uwanja wa Michezo wa Wembley, Jijini London, Uingereza. Hili ni tukio ambalo limefuatiliwa na mashabiki wa soka kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Ushindi huu umepokelewa kwa heshima na taadhima baada ya Italia kushinda Kombe la Ulaya kwa mara ya kwanza kunako mwaka 1968, yaani miaka 53 iliyopita! Kwa hakika hili ndilo gumzo la Italia kwa siku hizi! Jumapili tarehe 11 Julai 2021 Italia ikamliza Mwingereza aliyekuwa na matumaini makubwa ya kushinda akiwa anacheza nyumbani kwao! Lakini kama yasemavyo Maandiko Matakatifu, Nabii hakosi heshima isipokuwa kwa watu wa nyumbani kwake. Italia ilizimia kana kwamba, imepigwa sindano ya ganzi baada ya kufungwa bao moja na Uingereza!

Dakika ya 67, Italia ikacharuka na kusawazisha, jambo ambalo liliwaamsha hata wale waliokuwa wameanza kukata tamaa na kusinzia. Muda wa ziada ukaongezwa na kumalizika kwa timu zote mbili kufungana bao moja kwa moja! Wachezaji maarufu wa Uingereza kama Marcus Rashford, Jadon Sancho pamoja na Bukayo Saka, hawakufua dafu, wakashindwa kuliona goli la Italia! Wachezaji wa Italia ambao wamejizolea umaarufu katika mashindani haya ni Domenico Berardi, Leonardo Bonucci pamoja na Federico Bernardeschi, waliowasimasisha Waitalia kwa kuwafunga Waingereza kwa matuta, 3-2 katika mashindano ya Shirikisho la Soka Barani Ulaya, UEFA EURO 2020. Kocha wa Italia Roberro Manchini ameonesha furaha isiyokuwa na kifani kwa ushindi huu. Lakini kwa kocha Gareth Southgate, kimekuwa ni kilio chake! Mlinda mlango wa Italia Gianluigi Donnarumma alifanya kazi ya ziada kuokoa mikwaju miwili ya penati kutoka Uingereza na ametangazwa kuwa mchezaji bora wa mashindano ya Shirikisho la Soka Barani Ulaya, UEFA EURO 2020. Anakuwa ni mlinda mlango wa kwanza kutunukiwa heshima hii katika historia ya Soka Barani Ulaya! Ukiwa na roho nyepesi katika mechi kama hii unaweza kukuta umeandikiwa. RIP Brother, na watu wakaendelea na maisha kama kawa!

Euro 2020

 

 

12 July 2021, 15:33