Tafuta

Shirika la Kazi Duniani, ILO kuanzia tarehe 17-18 linafanya mkutano wake wa 109 pamoja na mambo mengine linapembua athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Shirika la Kazi Duniani, ILO kuanzia tarehe 17-18 linafanya mkutano wake wa 109 pamoja na mambo mengine linapembua athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. 

Shirika la Kazi Duniani, Mkutano wa 109 wa Kimataifa: UVIKO-19

Shirika la Kazi Duniani ILO, kuanzia tarehe 17 hadi 18 Juni 2021 linafanya Mkutano wa Kimataifa wa 109 kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Lengo la mkutano huu ni kupembua athari kumbwa ambazo zimesababishwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 sehemu mbalimbali za dunia. Papa Francisko ni kati ya viongozi waliohutubia mkutano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Kazi Duniani, ILO, kunako mwaka 2019, mambo makuu yafuatayo yalipaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Mosi ni umuhimu wa kazi kama utimilifu wa mtu binafsi, kijamii na kiikolojia. Pili, ni haja ya kutengeneza na kulinda fursa za ajira duniani kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi mintarafu mapokeo, rasilimali muda na teknolojia rafiki. Huu ni muhtasari wa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa mkutano wa 108 wa Shirika la Kazi Duniani mwezi Juni 2019. Shirika la Kazi Duniani ILO, kuanzia tarehe 17 hadi 18 Juni 2021 linafanya Mkutano wa Kimataifa wa 109 kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Lengo la mkutano huu ni kupembua athari kumbwa ambazo zimesababishwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 sehemu mbalimbali za dunia. Wajumbe wanaangalia sera na mbinu mkakati unaoweza kutumika ili kukabiliana na changamoto hii, sanjari na Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza zaidi katika maboresho ya ulimwengu wa kazi kwa sababu kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko, Rais Moon Jae-in wa Korea, Rais Fèlix Antoine Tshisekedi Tshilombo wa DRC, Waziri mkuu Antòno Costa wa Ureno pamoja na Rais Joe Biden wa Marekani ni kati ya viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa ambao wameshirikisha hotuba zao katika mkutano huu. Wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa wa 109 pamoja na mambo mengine wanajadili jinsi ya kugharimia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030. Mpango huu kimsingi ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani! Wajumbe wanayo nafasi ya kujadili kwa kina na mapana athari ambazo zimesababishwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 katika soko la kazi na ajira sehemu mbalimbali za dunia. Ni wakati muafaka kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu Mashirika na Makampuni ya Kimataifa, ili hatua muhimu ziweze kuchukuliwa kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa ulimwengu wa wafanyakazi unaosimikwa katika misingi ya kazi nzuri na haki jamii kwa wote bila ubaguzi. Hizi ni sera zinazopaswa kuwa fungamani na endelevu. Wajumbe pia wanapaswa kupitisha bajeti ya Shirika la Kazi Duniani, ILO, kwa kipindi cha mwaka 2022-2023. Mambo mengine ni pamoja na usalama wa kijamii. Hayati Benjamini William Mkapa, Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania aliwahi kuwakumbusha watanzania kwa kusema kwamba, njia ya maendeleo imejaa jasho na vumbi. Watu wazingatie utamaduni wa kupenda kufanya kazi kwa bidii, maarifa, ubunifu na kujituma. Lawama ni tamu ikitoka mdomoni, lakini peke yake haitapeleka mkono kinywani. Na katika kila mfanyakazi akumbuke kuwa umuhimu si muda anaoutumia kufanya kazi, bali kiasi cha kazi anayoweza kufanya katika muda liopewa.

Shirika la Kazi Duniani

 

 

 

 

18 June 2021, 10:00