Tafuta

Wanawake nchini Tanzania wanahamasishwa kuwekeza katika elimu ili waweze kujikomboa: kiuchumi, kiutu na kijamii. Wanawake nchini Tanzania wanahamasishwa kuwekeza katika elimu ili waweze kujikomboa: kiuchumi, kiutu na kijamii. 

Wanawake Wekezeni Katika Elimu Kujikwamua Kiuchumi na Kijamii!

Wanawake wanatoa mchango mkubwa kwenye shughuli za kimaendeleo lakini pia idadi kubwa ya watu wote Tanzania ni wanawake ambao ni asilimia 51.04 ya Watanzania wote. Kwa kutambua nafasi yao, Serikali imetunga sera, sheria pamoja na kuridhia mikataba ya kikanda na kimataifa ambavyo ni miongoni mwa mambo yanayochangia kuwainua kwenye hatua kubwa kimaendeo.

Na Georgina Misama – MAELEZO, - Dodoma.

Chai ya rangi ni kinywaji maarufu duniani kama kifungua kinywa ingawa kimekuwa kikitumika nyakati tofauti kutegemea na mazingira na pengine hali ya hewa ya eneo husika. Unapozungumzia chai ya rangi, majani ya chai ndio kila kitu, mtumiaji anahitaji maji ya moto tu, kutengeneza chai yake. Ni katika muktadha huo, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anawakumbusha wanawake wa Tanzania nguvu iliyo ndani yao kwa kuifananisha na majani ya chai kwa  kumnukuu mke wa mmoja wa aliyekuwa Rais wa Marekani Bi Eleanor Roosevelt aliyesema kwamba, mwanamke ni kama kipakiti  kidogo cha majani ya chai, huwezi kujua nguvu yake mpaka ukitumbukize kwenye maji ya moto  “A woman is like a tea bag, you can’t tell how strong she is until you put her in hot water” Eleanor Roosevelt.Hivi karibuni Rais Samia alifanya mkutano na  baadhi ya wanawake Jijini Dodoma,ambao waliwawakilisha wanawake wote wa Tanzania ni katika mkutano huo, Rais Samia aliwata wanawake wakakoleze rangi kila mmoja kwa nafasi yake ili kujikwamua kiuchumi.

Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete ulihudhuriwa na wanawake zaidi ya 14,000 ndani na nje ya ukumbi huo. Rais Samia alisema kwamba mkutano huo ni mwendelezo wa utaratibu aliojiwekea wa kukutana na Watanzania katika makundi mbalimbali. “Leo ni zamu yenu wanawake katika utaratibu niliojiwekea, tayari nimeshakutana na viongozi wa dini hapa Dodoma, Wazee wa mkoa wa Dar es salaam, viongozi wa sekta binafsi na wiki ijayo nitazungumza na vijana  mkoani Mwanza kwa niaba ya vijana wote nchini”, alisema Rais Samia. Aliongelea mambo mbalimbali kuhusu wanawake na jamii kwa ujumla kubwa akionesha juhudi zinazofanywa na Serikali katika kumnyanyua mwanamke akitambua kwamba wanawake wanatoa mchango mkubwa kwenye shughuli za kimaendeleo lakini pia idadi kubwa ya watu wote Tanzania ni wanawake ambao wanachukua asilimia 51.04% ya Watanzania wote. Alibainisha kwamba katika kutambua nafasi ya wanawake, Serikali imetunga sera, sheria pamoja na kuridhia mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa ambavyo ni miongoni mwa mambo yanayochangia kuwainua kwenye hatua kubwa kimaendeo.

Aidha, aliongelea vipengele kama uwiano wa jinsia katika vyombo vya maamuzi na ajira, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kutokomeza vitendo vya unyanyasaji kijinsia na ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Kipengele kingine ni pamoja na elimu na miundombinu ya usafiri. “Unapozungumzia masuala ya kumkomboa mwanamke, elimu ni kigezo kikubwa kwani ni msingi wa maisha ya mwanadamu yoyote iwe mwanamke hata mwanaume. Kwa hapa nchini hakuna tofauti kubwa ya uwiano kwenye usajili kati ya watoto wa kike na wa kiume kuanzia ngazi ya shule ya msingi mpaka chuo kikuu, takwimu zinaonesha katika wanafunzi wote wa shule ya msingi, asilimia 50.4 ni wasichana ambapo idadi yote ya wanafunzi wa shule ya sekondari wasichana ni asilimia 43.9”, alifafanua Mhe. Samia. Aidha, katika vyuo vya ufundi asilimia 47.8 ni wasichana ambapo kwa upande wa chuo kikuu idadi ya wasichana ni asilimia 43.0 katika jumla ya wanafunzi wote. Takwimu hizi zinaonyesha kwamba kuna idadi kubwa ya watoto wa kike wanaosajiliwa katika elimu ya msingi,ambapo suala la elimu bure linatajwa kama kigezo kimoja wapo kilichotoa msukumo huo. Bahati mbaya, idadi hyo inaenda ikipungua kwenye kila hatua ya elimu mpaka kufikia chuo kikuu. 

Miongoni mwa sababu alizozitaja kama changamoto zinazopunguza idadi ya watoto wa kike kwenye mifumo ya elimu nchini ni muindombinu isiyo rafiki kwa wanafunzi, hii inajumuisha vyoo vichache, upungufu wa maji, ukosefu wa mabweni pamoja na umbali kutoka kwenye makazi hadi shule ama vyuo. Ukiziangalia changamoto hizo utaona zinawaathiri wanafunzi wote pasipo kujali jinsia, lakini ukweli ni kwamba watoto wa kike wanaathiriwa zaidi na mazingira hayo na hivyo kuna idadi kubwa ya watoto wa kike wanaokatisha masomo kuliko ya watoto wa kiume. Serikali katika kuhakikisha inatatua changamoto zinazomkabili mtoto wa kike ikiwa ni pamoja na ufaulu mdogo kwenye masomo ya sayansi imekuja na mradi wa ujenzi wa shule maalum za bweni za sekondari kwa ajili ya watoto wa kike. “Kuanzia Julai mwaka huu, Serikali itaanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa shule moja ya sekondari yenye mabweni kwenye kila mkoa kwa ajili ya kufundisha masomo ya sayansi kwa wasichana”, alisema Rais Samia. Aliendelea kusema kuwa, Serikali imekuwa ikiweka fedha katika mfuko wa elimu ya juu ili kusaidia kuongeza idadi ya wasichana vyuoni. “Jamii yetu bado ina suasua linapokuja suala la kutoa fedha kumlipia mtoto wa kike katika kujiendeleza kielimu, kwa kutambua hilo mfuko huu umekuwa ukiongezewa fedha mwaka hadi mwaka. Kwa mwaka wa fedha 2020/21 mfuko ulipewa bilioni 464 wakati mwaka huu wa fedha 2021/22 fedha imeongezwa kufikia Bilioni 500”.

Kwa upande wake wake, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alisisitiza umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike akiwa kwenye hafla ya uchangiaji fedha kwa ajili ya kujenga shule maalum ya wasichana katika wilaya ya Kisarawe mwaka 2019 na kusema kwamba Serikali itajenga maabara ya fizikia katika shule hiyo maalum na itatoa vifaa vyote vya maabara, lengo likiwa kuhamasisha na kuongeza fursa za watoto wa kike Kisarawe na kwingineko nchini. “Naipongeza wilaya ya Kisarawe kwa kuja na kampeni ya ‘Tokomeza Ziro’ yenye lengo la kuboresha elimu katika wilaya hii ambapo mkazo umewekwa katika kumwondolea mtoto wa kike changamoto anazokabiliana nazo wakati wa kujifunza kwa kuhakikisha anapata mazingira rafiki na salama ya kujifunzia”, alisema Prof. Ndalichako. Akizungumzia usawa wa elimu katika ngazi mbalimbali kwenye jamii, Mhandisi Maida Waziri alisema kuwa watoto wanapaswa kundaliwa kuja kuwa watu fulani baadaye toka wanapokuwa wadogo ambapo hilo ni jukumu la msingi la wazazi. “Tuwaandae watoto wetu toka wanapokuwa wadogo ili kuhakikisha wanakuja kuchukua nafasi mbalimbali katika jamii hapo wanapoanza kujitegemea.  Tusibague michezo wala kazi ndogondogo za nyumbani kwani hata watakapokuwa watu wazima hakuna kazi ya mwanaume na mwanamke”, alisema Mhandisi Maida

Aidha, aliendelea kusema kuwa yeye ni Mhandisi mzuri na pia kiongozi katika eneo lake la kazi anaona jinsi kina mama wanavyopambana kutimiza majukumu yao na wanafanya vizuri sana. Kwa kuzingatia usawa wa majukumu alimuandaa binti yake toka akiwa mdogo na binti huyo sasa ni mhandisi bora na sio bora mhandisi. Mdau mwingine wa maendeleo ya elimu kutoka mkoa wa Mbeya, Amani Mwansansu alisema kuwa wakati umefika kwa Serikali kutoa nafasi ya upendeleo kwa mtoto wa kike anayeishi maeneo ya pembezoni kwani mbali na changamoto kubwa inayotajwa kiuchumi kwenye familia wanazoishi, lakini elimu ina umuhimu mkubwa na jamii nayo inahitaji kuelimishwa. Tangu kuanzishwa kwa mpango wa elimu bila malipo, Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita zimekuwa zikiweka mkazo upatikanaji wa elimu bora hasa kwa mtoto wa kike ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia ili kuleta matokea chanya katika sekta ya elimu.

28 June 2021, 07:49