Tafuta

Mkutano wa 42 wa Shirika la Chakula na Kilimo  la Umoja wa Mataifa. Mkutano wa 42 wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa. 

Mkutano wa 42 wa FAO: Baa la Njaa Duniani na Athari Zake

FAO kuanzia tarehe 14 hadi 18 Juni 2021 linafanya Kikao chake cha 42 kwenye Makao yake Makuu mjini Roma. Mkutano huu pamoja na mambo mengine, unajielekeza zaidi katika sera na mikakati ya uhakika na usalama wa chakula duniani kwa kupembua taarifa za hali halisi ya chakula kutoka katika Kanda mbalimbali za FAO. Ni fursa ya kuunda Tume itakayoshughulikia wadudu waharibifu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO kuanzia tarehe 14 hadi 18 Juni 2021 linafanya Kikao chake cha 42 kwenye Makao yake Makuu mjini Roma. Mkutano huu pamoja na mambo mengine, unajielekeza zaidi katika sera na mikakati ya uhakika na usalama wa chakula duniani kwa kupembua taarifa za hali halisi ya chakula kutoka katika Kanda mbalimbali za FAO. Ni fursa ya kuunda Tume itakayoshughulikia masuala ya mapambano dhidi ya wadudu waharibifu pamoja na mapendekezo ya kuanzishwa kwa maadhimisho ya Siku za Kimataifa. Ni mkutano unaopanga pia Bajeti ya FAO kwa mwaka wa fedha 2022-2023, bila kusahau masuala ya kisheria, utawala na fedha.  

FAO inabainisha kwamba, hata kabla ya kuzuka na hatimaye kupamba moto kwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 tayari kulikuwa na mamilioni ya watu waliokuwa wanasiginwa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha sehemu mbalimbali za dunia. Changamoto mamboleo kubwa kwa sasa ni uhakika na usalama wa chakula duniani, hali ambayo inapaswa kwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na maboresho ya maisha ya watu duniani. FAO inapenda kuwekeza zaidi katika teknolojia rafiki, utunzaji bora wa takwimu, utawala bora pamoja na maboresho ya taasisi mbalimbali zitakazosaidia katika mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani.

Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umesababisha kuyumba kwa mfumo wa uzalishaji na ugavi wa chakula duniani, kwani hapo awali FAO ilipania kuwawezesha wakulima wadogo wadogo ili kusaidia katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo duniani. Walengwa wakuu walikuwa ni watu wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, ili waweze kuunganisha nguvu katika mapambano dhidi ya baa la njaa duniani.

Mkutano wa FAO

 

16 June 2021, 08:08