Tafuta

Rais Mstaafu Dr. Kenneth David Kaunda, AKA KK: 28 Aprili 1924 - 17 Juni 2021. Rais Mstaafu Dr. Kenneth David Kaunda, AKA KK: 28 Aprili 1924 - 17 Juni 2021. 

Dr. Kenneth David Kaunda: 28 Aprili 1924 - 17 Juni 2021: KK

Hayati Dr. Kaunda kuwa miongoni mwa viongozi mahiri na jasiri kuwahi kutokea Barani Afrika, ambapo wakati wa uhai wake alitoa mchango mkubwa kwenye harakati za ukombozi wa Bara la Afrika kwa kushirikiana na viongozi wengine, akiwemo Baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Alikuwa pia ni Muasisi wa SADC ili kuchochea maendeleo Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha Rais wa kwanza wa Zambia, Dr. Kenneth David Kaunda, kilichotokea tarehe 17 Juni 2021 kwenye Hospitali ya Kijeshi ya Maina Soko mjini Lusaka, nchini Zambia akiwa na umri wa miaka 97. Katika kipindi hiki cha maombolezo, bendera zote zitapepea nusu mlingoti. Wakati huo, Rais Samia ametuma salam za rambirambi kwa Rais wa Zambia, Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu, familia ya Marehemu Mzee Kaunda na wananchi wote wa Zambia kwa kumpoteza kiongozi wao mpendwa!

Rais Samia amemtaja Hayati Dr. Kaunda kuwa miongoni mwa viongozi mahiri na jasiri kuwahi kutokea Barani Afrika, ambapo wakati wa uhai wake alitoa mchango mkubwa kwenye harakati za ukombozi wa Bara la Afrika kwa kushirikiana na viongozi wengine, akiwemo Baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Vilelevile, Hayati Dr. Kenneth David Kaunda alikuwa ni miongoni mwa waasisi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC. Kwa namna ya pekee kabisa, Tanzania inamkumbuka Hayati Dr. Kaunda kwa mchango wake katika kukuza na kudumisha uhusiano na ushirikiano wa udugu wa kibinadamu kati ya Mataifa haya mawili, ambao uliyawezesha kutekelezwa kwa miradi mikubwa ya kimakakati, ikiwemo Mamlaka ya Reli Kati ya Tanzania na Zambia, TAZARA pamoja na Bomba la Kusafirisha Mafuta, TAZAMA.

Itakumbukwa kwamba, Dr. Kenneth David Kaunda maarufu kama KK, alizaliwa tarehe 28 Aprili 1924 na kubahatika kuwa ni Muasisi wa Zambia na kuwaongoza Wazambia tangu mwaka 1964 hadi mwaka 1991. Hiki kilikuwa ni kipindi cha vuguvugu la vyama vingi vya kisiasa. Chama cha Movement For Multi-party Democracy (MMD), kilichojulikana pia kama “New Hope MMD” kilishinda uchaguzi mkuu na kuingia madarakani na huo ukawa ni mwisho wa uongozi wa Rais Dr. Kaunda kwa muda wa miaka 27. Katika maisha yake, kunako mwaka 1946 alifunga ndoa na Mama Betty Kaunda aliyefariki dunia tarehe 19 Septemba 2012 akiwa na umri wa miaka 84. Walibahatika kupata watoto 8 katika familia yao. KK alikuwa pia ni mwandishi mzuri wa vitabu. Tarehe 4 Juni 1998 aling’atuka kutoka katika uringo wa siasa.

Zambia KK

 

20 June 2021, 15:52