Tafuta

Vatican News
2021.05.25  Siku ya Afrika 2021.05.25 Siku ya Afrika  

Siku ya Afrika 2021:Janga la Corona limezidisha shida zilizokuwapo tayari

Katika Siku ya Afrika tarehe 25 Mei,Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres amethitibitisha kuwa utajiri wa utamaduni tofauti na maliasili barani Afrika ni muhimu sana katika maendeleo endelevu ili kupunguza umaskini,kujenga na kudumisha amani.Kwa sasa hakuna uwiano katika usambazaji wa chanjo miongoni mwa nchi na takwimu mpya zikionesha hadi leo nchi za Afrika zimepokea asilimia 2 tu ya chanjo.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Kupitia ujumbe wake uliotolewa tarehe 25 Mei katika kilele cha kuadhimisha siku ya Afrika  2021, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres amesema utajiri wa utamaduni tofauti na maliasili barani Afrika ni muhimu sana katika maendeleo endelevu SDGs,ili kupunguza umasikini na kujenga na kudumisha amani. Bwana Gutteres amesema “utajiri huo unaweza kuweka msingi imara kwa ajili ya maendeleo ya uchumi jumuishi wakati bara hilo kubwa linapoendelea  kukabiliana na changamoto zilizoletwa na janga la virusi vya corona au COVID-19.”  

Kwa mujibu wa  Katibu Mkuu amesema maadhimisho ya siku ya Afrika mwaka huu yamejikita katika kutanabaisha Sanaa, utamaduni na urithi asilia kama chachu ya kujenga Afrika tunayoitaka na kuongeza kuwa lakini janga la COVID-19 limeifanya dunia nzima kuyumba hasa kiuchumi na kwa maana hiyo kuibua juu hatari na pengo kubwa lililopo la usawa. “Janga hilo linahatarisha hatua za maendeleo zilizopigwa barani Afrika na zaidi na kuchochea migogoro kutokana na ongezeko la pengo la usawa, hivyo kudhihirisha hali tete ya serikali nyingi duniani hususan katika kufikisha kwa watu wake huduma msingi kama za afya, elimu,nishati ya umeme, maji na usafi.”

Bwana Guterres amesema athari za janga la COVID-19 zimezidishwa pia na mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kiasi kikubwa yanaathiri nchi zinazoendelea nyingi zikiwemo barani Afrika. Aidha kiongozi huyo  ameiambia dunia kwamba ili kumaliza janga la COVID19, na kusaidia kujikwamua kiuchumi na kutimiza malengo ya maendeleo endelevu  ndiyo muhimu: ”Tunahitaji kuhakikisha fursa na usawa kwa kila mtu katika upatikanaji wa chanjo za COVID-19. Hivi sasa hakuna uwiano katika usambazaji wa chanjo miongoni mwa nchi na takwimu mpya zikionesha kwamba hadi kufikia leo nchi za Afrika zimepokea asilimia mbili tu ya chanjo hizo.”  Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema “Katika siku hii ya Afrika narejea wito wetu kwa nchi Tajiri kushikamana na Afrika katika suala hili.”  

Ikumbukwe kila mwaka ifikapo tarehe 25 Mei uadhimsha Siku ya Afrika, ambayo inakumbuka kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika, UA kunako tarehe 25 Mei 1963 huko mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia. Kunako tarehe 11 Julai 2001, Mkutano mkuu wa UA uliamua kuunda Umoja wa Afrika kama sehemu  ya mkakati wa kukuza na kudumisha Umoja na mshikamano miongoni mwa nchi za Kiafrika na tarehe 9 Julai 2002, Umoja wa Afrika ukazaliwa rasmi! Umoja wa Afrika unataka kuhamasisha na kudumisha umoja katika masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kitamaduni ili kuondokana na ukoloni mamboleo pamoja na ukoloni wa kiitikadi na utamaduni wa kifo, ambao kwa nyakati zetu umenyemelewa mara nyingi kwenye masharti ya misaada kwa Bara la Afrika. Umoja huo lei hii kuliko awali unahitajika sana na hasa dunia inpopambana na janga la virusi vya corona au covid-19 iliyopigisha magoti hata mataifa makubwa kiuchumi  na viwanda.

25 May 2021, 17:50