Tafuta

Vatican News
Kifo cha Rais Magufuli wa Tanzania Kifo cha Rais Magufuli wa Tanzania  (AFP or licensors)

Tanzania:Nchi inamlilia Rais Magufuli

Rais ambaye hakupenda urasimu wala ukiritimba wa hapa na pale,bali kutoa uamuzi wa hapo hapo hasa kwa ajili ya wanyonge amerudi kwa Muumba wake jioni tarehe 17 Machi 2021.Ni pengo kubwa ambalo halizibiki.Taarifa za kifo chake zilitolewa na Makamu wake.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Nchi ya Tanzania, imeguswa na msiba mkubwa lakini si tu nchi yenyewe bali nchi za karibu, Afrika na ulimwengu mzima. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Joseph Pombe Magufuli aliaga dunia  siku ya Jumatano jioni jijini Dar es Salaam kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa usiku saa tano masaa ya Afrika Mashariki.

Alikuwa ni Makamu wa rais wa Tanzania Bi Samia Suluhu Hassan aliyetangaza kifo cha Rais wa Jamhuri ya Tanzania akiwapa taarifa hizi ngumu kwa Watanzania kupitia runinga ya kitaifa.

Bi Samia alisema wamempoteza kiongozi wao shupavu aliyefariki mida ya saa kumi na mbili jioni tarehe 17 Machi 2021 kutokana na maradhi ya moyo katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam. Makamu wa  rais  Bi Samia alielezea kwamba marehemu Magufuli alilazwa mnamo tarehe  6 Machi katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete kutokana na tatizo la moyo liitwalo  mfumo wa umeme, ambalo alikuwa nalo kwa miaka kumi hivi.

Bi Samia alisema kuwa aliruhusiwa kutoka hospitali tarehe 7 Machi na kuendelea na majukumu yake, lakini tarehe 14 Machi  alijisikia vibaya na akakimbizwa tena Hospitali hiyo ya Mzena ambako alilazwa hadi umauti yalipomfikia. Bi Samia aidha ametangaza siku 14 za maombolezo ya kitaifa na bendere kubendera kushushwa nusu mlingoti.

Hakika Tanzania inampoteza kiongozi shupavu mtetezi wa Taifa na watu wake. Pengo ni kubwa kwa taifa.

18 March 2021, 10:01