Tafuta

Vatican News
Watanzania wataendelea kumkumbuka Hayati Dkt John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Serikali ya awamu ya tano kwa uthubutu wake katika mchakati wa ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Watanzania wataendelea kumkumbuka Hayati Dkt John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Serikali ya awamu ya tano kwa uthubutu wake katika mchakati wa ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi.  (AFP or licensors)

Hayati Dkt. John P. Magufuli: Mchango Wake kwa Tanzania

Kwa hakika amejiwekea amana na hazina ya upendo katika sakafu ya nyoyo za watanzania wenzake. Alionesha maisha ya hofu na uchaji wa Mungu, akawataka watanzania kumtanguliza Mungu katika maisha. Si rahisi sana kuweza kuorodhesha mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini Tanzania katika kipindi cha uongozi wake katika sekta ya ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kwa hakika kifo cha Dkt John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Serikali ya awamu ya tano, kimewagusa na kuwashtua watanzania na watu wenye mapenzi mema sehemu mbalimbali za dunia. Hili limekuwa ni tukio ambalo limefuatiliwa sana kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kiasi cha kuwashangaza watu wa ndani na nje ya nchi kwa bahari na mafuriko ya watanzania, waliokwenda kutoa heshima zao za mwisho! Wachunguzi wa mambo wanasema, maombolezo ya msiba huu mzito ni darasa tosha kabisa kwa viongozi wa Serika ndani na nje ya Tanzania pamoja na wanasiasa wanaopaswa kujipanga vyema kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wao wanaowaongoza. Wale waliolishwa “matango pori kwa habari za kuzusha na kupindisha ukweli, wameshuhudia watanzania wakiandamana kwa boti, mitumbwi, na mashua ili kumsindikiza “Chuma” akienda nyumbani kwake Chato kwa maziko, Ijumaa tarehe 26 Machi 2021.

Watanzania wameomboleza, wakatandaza nguo zao njiani, ili mtu wa haki, aweze kupita katika ukimya, ushuhuda kwamba, kwa hakika, watanzania walimpenda Hayati Dkt. Magufuli kwa upendo wa dhati na moyo mweupe pe, wakamthamini sana. Kwa hakika amejiwekea amana na hazina ya upendo katika nyoyo za watanzania wenzake Dr. John Pombe Magufuli amekuwa ni kiongozi aliyebeba dhamana na wajibu wake wa kuwaongoza watanzania kwa ari, moyo mkuu na utulivu! Akawaonesha watanzania furaha pale walipogusa undani wa maisha yake! Alionesha maisha ya hofu na uchaji wa Mungu na kuwataka watanzania kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza katika maisha yao. Si rahisi sana kuweza kuorodhesha mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini Tanzania katika kipindi cha uongozi wake katika sekta ya ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi.

Watanzania wanaonesha uchungu na majonzi makubwa kwa Shujaa wao aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kurejesha nidhamu na uwajibikaji wa watumishi wa umma, bila kupepesa pepesa macho! Alisimama kidete kupambana na rushwa na ufisadi wa mali ya umma; “wapigaji” wakachezeshwa vidogori na kukiona cha mtema kuni”. Watanzania kutoka vijiji mbalimbali walimiminika barabarani ili kutoa heshima na shukrani zao kwa maboresho makubwa ya huduma ya umeme vijijini. Kutoka asilimia 47% iliyokuwepo mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 69% katika kipindi cha mwaka 2019-2021. Huduma ya maji safi na salama vijijini imeboreka kutoka asilimia 47% katika kipindi cha mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 70.1%. Ikumbukwe kwamba, maji safi na salama ni sehemu ha haki msingi za binadamu kwa sababu maji ni uhai!

Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa “Jembe” la nguvu. Serikali yake, ikajizatiti kutoa elimu ya bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na kufuta michango iliyokuwa inawanyanyasa “watoto wa wakulima”, kwani alitambua kwamba, kwa njia ya elimu makini, hata watoto wa watanzania maskini “wataweza kutoboa” na hatimaye kupata maisha bora zaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba, elimu ni ufunguo wa maisha. Katika uongozi wa Serikali ya awamu ya tano chini ya “Jiwe”, Serikali ya Tanzania iliweza kujenga Zahanati 1, 198, Vituo vya Afya 497 na Hospitali za Wilaya ni 71. Dkt Magufuli alitambua kwamba, afya bora kwa watanzania ni mtaji katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo fungamani ya binadamu.

Wananchi wa Dodoma wamemlilia “Chuma” kwa kusimamia kwa umakini na umahiri maamuzi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kuhamia Dodoma, yaliyotolewa kunako miaka 1973. Serikali ilikuwa imepanga kuhamia Dodoma ifikapo mwaka 1983, lakini haikuwezekana kutokana na sababu mbalimbali. Ni Dkt. Magufuli aliyetia nia ya kuhamia Dodoma na leo hii, Dodoma kumekucha, mwenye macho, akatazame mwenyewe! Uwanja wa michezo na kukamilika kwa uwanja mpya wa ndege, Dodoma, litakuwa ni Jiji la kuotea mbali! Nitakosa fadhila na shukrani kwa Dkt. Magufuli kwa kushindwa kutaja uthubutu wake uliowawezesha watanzania kuingia uchumi wa kati! Mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma mbalimbali umeshuka. Kumekuwepo na ongezeko la Pato Ghafi la Taifa, GNP kutoka asilimia 12.8% kwa mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 14.2% katika kipindi cha mwaka 2020.

Kumekuwepo na usimamizi mzuri na ukusanyaji wa kodi ya serikali kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia shilingi trilioni 1.9. Mchakato huu unaweza kuboreshwa zaidi kwa kujadiliana na wadau mbalimbali. Wachumi wanasema, ongezeko hili ni sawa na asilimia 200%. Kumekuwepo na ujenzi wa viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa 8400. Lengo la Serikali ya awamu ya tano lilikuwa ni kuiwezesha Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda. Uuzaji wa mazao ya biashara nchi za nje umeongezeka maradufu. Shirika la Ndege la Tanzania, limefufuliwa na leo Mwanamke mtanzania anaendesha ndege utadhani “daladala”. Kwa Uncle Magu, amewapatia watanzania ari na uwezo wa kujiamini katika mambo yao. Mtandao wa barabara ya lami umeongezeka maradufu, kiasi cha kufikia km 3, 500.

Kukamilika kwa madaraja mbalimbali kama yale ya: Kigamboni, Mfugale, Ubungo na Busisi ni hatua kubwa katika kuinua uchumi wa nchi kwa kuzingatia rasilimali muda! Reli ya Kisasa ya mwendo kasi ikikamilika, watanzania watakuwa na uhakika wa usafiri kwa muda mfupi! Kumekuwepo na maboresho ya Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ili kukuza na kudumisha uchumi wa ndani pamoja na ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya biashara na usafirishaji. Mradi wa kufua umeme ni hatua nyingine inayotoa matumaini kwa watanzania. Haya ni machache kati ya mengi ambayo watanzania wanayakumbuka kutoka kwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. PKA: “Pumzika Kwa Amani”, Dkt. Jon Pombe Magufuli. Zamani tulikuwa tunaandika RIP.

Mafanikio ya JPM
25 March 2021, 15:47