Tafuta

Dr. Philip Isdor Nzabhayanga Mpango ateuliwa na kuthibitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni Makamu wa Rais wa Tanzania kwa usindi wa tsunami yaani kura 363 sawa na asilimia 100% Dr. Philip Isdor Nzabhayanga Mpango ateuliwa na kuthibitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni Makamu wa Rais wa Tanzania kwa usindi wa tsunami yaani kura 363 sawa na asilimia 100% 

Dr. Philip Isdor Mpango Makamu wa Rais Nchini Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan, tarehe 30 Machi 2021, alimpendekeza Dr. Philip Isdor Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jina likapigiwa kura na wabunge 363 na hakuna zilizoharibika na kwamba, Makamu wa Rais mteule Dr. Philip Isdor Nzabhayanga Mpango akakwangua kura zote 363 sawa na asilimia 100% ya kura zote zilizopigwa. Ushindi wa Tsunami!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Jumanne tarehe 30 Machi 2021, alimpendekeza Dr. Philip Isdor Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jina likapigiwa kura na Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania akatamka kwamba, kura halali zilizopigwa na wabunge ni 363 na hakuna zilizoharibika na kwamba, Makamu wa Rais mteule Dr. Philip Isdor Nzabhayanga Mpango amepata kura 363 sawa na asilimia 100% ya kura zote zilizopigwa. Kutokana na ushindi huu wa Tsunami, tarehe 31 Machi 2021 majira ya saa 9:00 kwa saa za Afrika Mashariki ataapishwa Jijini Dodoma na hivyo kuwa ni Makamu wa Saba wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Hizi ni dalili njema kwamba, watanzania wana imani na uongozi mpya chini ya Mama Samia Suluhu Hassan. Dr. Mpango katika hotuba yake ametoa shukrani zake za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupendekeza jina lake na kuridhiwa na Chama cha Mapinduzi na hatimaye, kuletwa Bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa na Bunge. Hii ni heshima kubwa sana maisha mwake, na wala hakuwahi kuota kupata nafasi kama hii!

Wachunguzi wa mambo ya siasa wanasema, Dr. Philip Isdor Nzabhayanga Mpango ni kiongozi mwenye msimamo thabiti katika maisha yake; ni mwadilifu na mchamungu; mkweli na muwazi; anayezingatia kanuni maadili na utu wema; nidhamu na uwajibikaji. Ni kiongozi mwenye maono mapana, anayefahamu vyanzo vya umaskini wa watanzania, vikwazo vinavyokwamisha ukuaji wa uchumi; umuhimu wa ugawanyaji wa rasilimali za taifa kwa usawa ili kuleta ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi! Kwa ufupi kabisa, itakumbukwa kwamba, Dr. Philip Isdori Nzabhayanga Mpango, alizaliwa tarehe 14 Julai 1957 Kijiji cha Kasumo, Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, nchini Tanzania. Amewahi kuwa Mchumi Mwandamizi wa Benki ya Dunia, Mkuu wa Kamati ya kumshauri Rais Jakaya Kikwete wakati huo, kuhusu masuala ya uchumi, Katibu binafsi wa Rais anayeshughulikia masuala ya uchumi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, kabla ya kuhamishiwa Tume ya Mipango, Ofisi ya Rais. Nyadhifa hizi zote amezishika wakati wa uongozi wa Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete!

Hayati Rais Dkt John Pombe Magufuli alipoingia madarakani kunako mwaka 2015 alimteua Dr. Philip Isdor Nzabhayanga Mpango kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na baada ya siku chache akamteuwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango. Dr. Mpango ndiye aliyepanga na kufanikisha mipango ya kuwainua watanzania hadi kufikia uchumi wa kati. Kwa hakika watanzania wana imani na matumaini makubwa chini ya uongozi wa Rais Samilia Suluhu Hassan ambaye ameanza uongozi wake, kwa kuonesha makali yake. Jeshi la Polisi nchini Tanzania kwa kushirikiana na TAKUKURU imemtia mbaroni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mhandishi Deusdedith Kakoko aliyekutwa na kiasi cha dola 3,000 na shilingi za Kitanzania milioni 1.5. Brigedia Jenerali John Mbungo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU amethibitisha tukio hili na kusema kwamba, anashikiliwa na Polisi ili kufanya uchunguzi vizuri zaidi. Taratibu zote za upekuzi kisheria zilizingatiwa na kwamba, TAKUKURU tangu mwezi Machi 2020 ilikwisha kuanza uchunguzi na sasa inakaribia kukamilisha uchunguzi huu, ili wale wote watakaobainika "kumung'unya fedha ya umma" wafikishwe panapohusika ili sheria ishike mkondo wake.

Dr Mpango
30 March 2021, 16:08